IJUMAA WIKI YA 31 YA MWAKA-C
Somo:
Flp 3:17-4:1
Zab/kit: 122:1-2, 4, 5
Injili: Lk 16:1-8
Nukuu:
“Maana wengi huenenda,
ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi,
kuwa ni adui za msalaba wa Kristo,” Flp 3:18
“mwisho wao ni
uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo
ya duniani,” Flp 3:19
“Kwa maana sisi,
wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu
Kristo,” Flp 3:20
“atakayeubadili mwili
wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao
kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake,” Flp 3:21
“Basi, ndugu zangu,
wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni
imara katika Bwana, wapenzi wangu,” Flp 4:1
“Toa
hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena,” Lk 16:2b
“Yule
bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa
ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru,”
Lk 16:8
TAFAKARI:
“Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa
huwezi kuwa wakili tena.”
Wapendwa katika Kristo,
Injili ya leo inatupatia hali halisi kuhusu hesabu yetu siku ya mwisho. Yesu
analisema jambo hilo akitolea mfano wa Tajiri mmoja na Wakili wake dhalimu. Bila kujua siku wala saa, Wakili huyu dhalimu
anatakiwa na Tajiri yake kutoa hesabu ya uwakile wake, baada ya Tajiri yake
kupata habari ya kutapanywa kwa mali zake, Lk 16:1. Alichokifanya kwa haraka
Wakili yule ni kurejesha uhusiano wa haraka na wateja zake ambao ndio hatma ya
maisha yake kwa sasa.
Katika jambo hili ilimpasa kutoa msamaha
wa madeni bila kuhathiri utajiri wa Tajiri yake. Hivyo, “Yule bwana akamsifu
wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu
katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru,” Lk 16:8. Kwa
kuyasema haya, Yesu anatuacha na swali zito la kujibu. Swali hilo ni hili: Mimi
na wewe tunasubiri nini kurejesha uhusiano wetu na Mungu kwa muda na nafasi
tuliyonayo sasa tukiwa bado kwenye nuru, yaani, kwa ubatizo wetu na agano letu
katika maisha, iwapo Wakili huyu na udhalimu wake aliweza kurejesha uhusiano
wake na wateja zake?
Somo letu la kwanza sote kama mawakili
wa Bwana wetu Yesu Kristo tu na dhamana juu ya imani yetu. Hivyo Mtume Paulo
anatufundisha wewe na mimi namna ya kuurejesha uhusiano huo ndani ya nafsi
yako, jirani zako, na Mungu. Na kama tunashindwa namna ya kufanya tumtazame
yeye (historia yake awali na maisha yake baada ya kuongoka, Flp 3:17; Gal
1:13-23). Hapo mwanza kabla ya kumjua Kristo alilihujumu Kanisa haswa kwa
sababu alifikiri kufanya hivyo ni kulinda na kutetea mila na desturi za
Kiyahudi ambazo kwa uwepo wa Kristo na Wakristo ilikuwa ni tishio katika ustawi
wake.
Kwa maneno mengine kabla la kuongoka
kwake, Paulo alikuwa mpinga Kristo si kwa maneno tu bali kwa matendo yake, Mdo
9:1-2. Hivyo leo akiwa huru ndani na katika Kristo Yesu anatoa mang’amuzi yake
na kusema, “Maana wengi huenenda, ambao
nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa
ni adui za msalaba wa Kristo,” Flp 3:18. Paulo sana yupo ndani ya nuru ya Yesu
Kristo, na anaona faida kubwa ya kuwa na uhusiano naye. Kuna hasara kubwa kujua
kweli hii na mwisho wa siku ukaacha kujenga uhusiano na Kristo aliye njia,
kweli, na uzima.
Leo na kama ilivyokuwa
nyakati za Mtume Paulo, yapo mambo mengi ambayo yanayoturudisha nyumba na hata
kutokuwa tayari kuujenga uhusiano huo na Kristo. Wengi walishindwa kuujenga
uhusiano huo na Kristo kwa sababu, “mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika
fedheha yao, waniao mambo ya duniani,” Flp 3:19. Vishawishi hivi alivyovitaja
Mtume Paulo licha ya kupita zaida ya miaka 2000 havijabadili kwa kizazi cha leo. Ni kwa sababu ya
tumbo-ubinfsi uliokidhiri, utukufu wa kutaka kuogopwa na kuabudiwa kama Mungu,
fedha na utajiri, na kuupenda ulimwengu na mambo yake katika ufahari wake, leo
wengi tumejikuta katika mtego huu. Maisha ni dhamana na ipo siku wewe na mimi
tutatakiwa kutoa hesabu.
Ukweli ni kwamba,
maisha ya hapa duniani licha ya vishawisho hivyo, ni ya muda mfupi sana. Hapa
sipo mwisho na kusudi la kuumbwa kwetu. Tumeumbwa tuishi milele, na hapa sipo
penye hayo kao ya milele. “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka
huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo,” Flp 3:20. Na katika mantiki
hii, ni Kristo Yesu tu “atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na
mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu
vyote viwe chini yake,” Flp 3:21. Haya yote tunayoyaangaikia usiku na mchana
licha ya uzuri wake na mafaa yake, hayawezi kuubadili mwili wetu wa unyonge
ufanane na mwili wa Kristo wa Utukufu.
Mwito wa Mtume Paulo
kwako na kwangu leo ni huu: “simama imara katika Bwana,” Flp 4:1. Na kusimama
katika Kristo Yesu ni kuenenda kama wana wa Nuru na siyo wa giza. Matendo yetu
mema yawe chumvi pale tulipo, na maadili yetu mema yawe taa na mwanga pale
tulipo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko
mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo,” Flp 3:20
Tusali:-Ee
Yesu na Mkombozi wetu, tujalie mwanga na nuru katika maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario