viernes, 4 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 31 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 31 YA MWAKA-C

Somo: Flp 4:10-19

Zab/kit: 112:1-2, 5-6, 8a, 9

Injili: Lk 16:9-15

Nukuu:

Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa,”12 

“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” Flp 4:13

 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia,” Lk 16:10

Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Lk 16:13

Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu,” Lk 16:15

TAFAKARI: "Mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.”

Wapendwa wana wa Mungu, Injili yetu ya leo yatutafakarisha juu ya kweli hii, ‘mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.’ Sehemu hii ya Injili ni mwendelezo wa Injili tuliyosoma jana tulipotafakari neno hili, ‘Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.’ Ndugu yangu, unapokuwa na malengo thabiti katika maisha yako hukujengea msisitizo na uaminifu wa jambo hilo unalolifanya. Mafanikio ya mtu ni moja ya tokeo la namna alivyojiwekeza katika kitu hicho. Mkusanyiko wa pamoja wa nguvu zako, akili zako, na juhudi zako zisizo jigawagawa hukupatia matokeo mazuri kwa kile ukifanyacho.

Katika jambo hili la kujigawagawa Yesu anatupa angalizo na kusema, Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Lk 16:13. Kama wataka kumtumikia Mungu fanya hivyo kweli pasipo kujibakiza. Kufikia hatua hii katika mwono huu wa maisha, ni kufanya tathimini ya kina juu ya maisha yako kama asemavyo Mtume Paulo, Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa,” Flp 4:12. Matokea ya tathmini hii katika maisha ni makubwa sana, faida yake nikubwa sana, yaani, hapa duniani na Mbinguni uzima wa milele.

Ila ukijitumikisha tu kwa sababu ya mali, utapata faida ya muda mfupi hapa duniani na kukosa faida ya milele Mbingu, yaani maisha ya uzima na umilele wake. Pamoja na hayo yote niliyoyasema,  mafanikio yako husukumwa na uaminifu wako mwenyewe kwa kile unachofanya hata katika udogo wake. Katika hili, Mtume Paulo anatoa ushuhuda wa uaminifu wake kwa jumuiya ile ya Wafilipi na kusema, “Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu,” Flp 4:15. Mtume Paulo hakujibakiza katika ushiriki wake na watu wake. Aliwaona kama alivyojiona yeye mwenyewe, na alikuwa sehemu ya jumuiya ile katika kufikiri, kuamua, na kutenda pamoja. Naye anawaambia, “mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu,” Flp 4:14

Ndugu yangu, tunapojitoa kwa watu na kwa ajili yao, kamwe hawawezi kutuacha katika yote. Ushiriki wetu na watu katika shida zao kwa lengo la kufanya hali na mazingira yale yawe sehemu nzuri zaidi ya kuishi, huwajengea ujari wale unaowaongoza na kwako pia kwani matokeo yake huyaona na kuyaishi. Hivyo Wafilipi hawakumtupa Mtume Paulo. Walimjali hata nyakati zile ambazo hakuwa nao. Naye Mtume Paulo anawakumbusha ukarimu wao kwake na kusema, “hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja,” Flp 4:16. Ni vibaya sana pale tunapokosa shukrani kwa yale watutendeayo watu kwa upendo wao. Na moyo usio na shukrani ukausha mema yote. Hata kama watutendeayo watu ni madogo, hatupungukiwi chochote kwa kusema neno “ASANTE.”

Ndiyo maana leo Yesu anatuambia, Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia,” Lk 16:10. Hapa Yesu anatukumbusha kuwa maisha ni dhamana. Na kama maisha ni dhamana juu ya yale tuliopewa uwakili, basi yatupasa kuthamini kama yalivyo katika ukubwa na udogo wake. Leo Mtume Paulo anatufundisha namna ya uwakili baada ya kutambua thamani ya yale tuliyo wekwa dhamana nayo. Naye anasema, “Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu,”Flp 4:18. Ni yule tu mwenye hofu ya Mungu ndani yake anayeweza kuyasema haya toka moyoni mwake kwa ujasiri. Mara nyingi na tulio wengi, ‘kwenye mafanikio huzinyanyua nafsi zetu, na penye hasara au kushindwa huwalaumu wengine.’

Wewe na mimi tukiwa tu wafuasi wa Kristo na ndiyo maana tunaitwa Wakristo, hofu yetu katika kufikiri, kuamua, na kutenda ni KRISTO anayeyajenga maisha yetu kila siku. Na hii ndiyo siri ya mafanikio ya Mtume Paulo kama asemavyo, Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” Flp 4:13. Je, nguvu na jeuri yako msingi wake ni nini? Je, ni umaarufu ulio nao? Cheo ulicho nacho? Utajiri na fedha ulizo nazo? Je, ni afya uliyo nayo? Hayo yote ni upepo bila Mungu kwa sababu yote ni mali ya Mungu. Tumeazimwa tu kwa muda, kwani tulivikuta, na mwisho wa siku tutawaachia wengine kwa sababu hatukuja navyo.  Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha,” Zab 24:1-2. Je, bado una jeuri?

Mtume Paulo anatufundisha wewe na mimi leo kwamba tuwapo ndani na katika Kristo Yesu yote mema na mazuri yanawezekana kwani huyo ndiye Mungu anayemtumikia. Naye anasema, “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu,” Flp 4:19.

Hivyo ndugu yangu ni kukumbushe tena neno hili kwamba, “Moyo usio na shukrani ukausha mema yote. Na mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.” Kristo Yesu ndiye jibu kwa sababu ndani na katika Yeye ipo njia, kweli, na uzima, Yoh 14.6. Amina

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” Flp 4:13
Tusali:-Ee Yesu Mwema, yaongoze maisha yetu ili tuweze kabiliana na changamoto

No hay comentarios:

Publicar un comentario