JUMATATU WIKI YA 33 YA MWAKA-C
Somo:
Ufu 1:1-4; 2:1-5a
Zab/kit: 1:1-2, 3, 4, 6
Injili: Lk 18:35-43
Nukuu:
“Heri
asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa
humo; kwa maana wakati u karibu,” Ufu 1:3
“Nayajua matendo yako,
na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya,
tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo,” Ufu 2:2
“Lakini nina neno juu
yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza,” Ufu 2:4
“Basi, kumbuka ni wapi
ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza,” Ufu 2:5a
“Akapiga
kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:38
“Basi
wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza
sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:39
“Yesu
akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema,
Bwana, nipate kuona,” Lk 18:40-41
“Yesu
akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya,” Lk 18:42
TAFAKARI:
“Upewe kuona; imani yako imekuponya.”
Wapendwa wana wa Mungu,
miongozo ya kibinadamu na mwonekano wake unaweza
kutunyamazisha hapa na pale kwa kuikandamiza dhamiri iliyo hai na safi kuelekea
lililo kweli na haki. Kelele hizo kamwe zisiwe kizuio cha kiu na kweli iliyopo
ndani ya mioyo yetu. Leo katika Injili tunaona watu wachache wakijaribu kuzuia
dhamiri iliyo hai na safi ya mtu mmoja kipofu aliyekuwa ameketi kando ya njia
wakati Yesu akipita. Aliposikia habari ya Yesu alipiga kelele na kusema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:38.
Jitihada
za huyu kipofu zinajaribiwa na kuelekea kuzimwa na baadhi ya watu. “Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze;
lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:39.
Dhamiri iliyo hai na safi ya Kipofu huyu ikiongozwa na imani aliyokuwa nayo,
inakuwa sababu ya uponyaji wake. “Yesu
akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema,
Bwana, nipate kuona,” Lk 18:40-41. Imani hii
iliyothabiti na yenye kuongozwa na dhamiri hai na iliyosafi juu ya Mwana wa
Mungu, Kristo Yesu, inakuwa uponyaji wake. “Yesu
akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya,” Lk 18:42.
Dhamiri hai na safi
hukuzwa na kuelimishwa hasa pale tunapopenda kutenda mema kwa vile twatambua
jambo jema ni jema kama lilivyo na linastahili kutendwa na kila mmoja wetu na
hasa zaidi mwenye hofu ya Mungu.
Somo letu la kwanza
tunaona mateso na kudhulumiwa wa Kanisa la mwanzo na wale wampingao Kristo.
Falme nyingi na hasa zile zilizojichukulia nafasi ya Mungu, na kujifanya miungu
watu hazikupenda kabisa kusikia au kuona habari njema za wokovu, na Ufalme wa
Mungu ukishamiri. Katika hali na mazingira yale ilimpasa mmoja asema na
kusimama katika kweli na haki. Na hapa ndipo Kanisa lilisimama imara kwa kile
lilichokuwa likiamini na kuhubiri.
Na huu ndio unabii wa
Yohana, “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno
ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu,” Ufu
1:3. ‘Wakati u karibu’ kulimaanisha mwisho wa nyakati, na wakati huo huo
kulimaanisha ni muda muhafaka wa kusimama imara katika imani kadiri ya mashambulio
ya wampinga Kristo na Ufalme wake.
Yohana hakuona woga
wowote zaidi ya hofu ya Mungu kusimama katika kweli na haki juu ya kile
alichokiamini na kukuishi. Leo kati yetu pamoja na uhuru tulionao wa kuabudu na
kuishi imani pasipo hofu, bado si mashuhuda wa imani hiyo. Huwezi kuwa shuhuda
wa kile ukiaminicho kama huna uwezo wa kukishirikisha kile ukiaminicho kwa
watu. Huwezi pia kukishirikisha ukiaminicho kwa sababu hujafanya tafakari ya
kina kuhusu neno lile ya uzima. Na huwezi kulitafakari neno hilo kwa sababu
hukulipokea. Hukulipokea neno hilo kwa sababu hukutaka kulisikia.
Ni dhahiri akisemacho
Yohana na kukitolea ushuhuda ni neno lile la uzima alilolisikia, kulipokea,
kulitafakari, kulishirikisha, na mwisho ndilo analolitolea ushuhuda pasipo woga
zaidi ya hofu ya Mungu. Na hivi ndivyo mambo yalivyokuwa; “Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko
Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako
na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha
enzi,” Ufu 1:4. Kwa Kanisa lile la Efeso, Yohana analiona hili: “Nayajua
matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na
watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa
waongo,” Ufu 2:2. Hata pamoja na ukweli na juhudi hizo, bado wanaweza kufanya
vizuri zaidi.
Na kufanya kwao vizuri
ni kuurejea upendo ule wa kwanza, yaani, nguvu na neema zile walizokuwa nazo
baada ya kulisikia na kulipokea neno la uzima. Na hivi ndivyo asemavyo Yohana,
“Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza,” Ufu 2:4.
Na kurejea upendo ule wa kwanza ni kuangalia ni wapi waliojikwaa. “Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu,
ukayafanye matendo ya kwanza,” Ufu 2:5a. Kufanya tathmini katika maisha ni
jambo la muhimu kama kweli twataka kusonga mbele na kwenye mwanga zaidi.
Bila shaka jambo lolote
lile liwe zuri au baya katika maisha ya kila siku, ni alama wazi ya
kuyatafakari matendo yetu ikiwa ni pamoja na kuyahusisha na kusudi la kuumbwa
kwetu, na uwepo wetu hapa duniani. Matukio hayo (mazuri na mabaya) katika jamii
yetu yakufanye na kukupa uwezo wewe na mimi wa ‘kusikia, kupokea, kutafakari,
kushirikishana, na mwisho kutoa ushuhuda katika kweli na haki.’ Huko tuendako
pasipo sisi kupajua kwa asilimia 100% hapawezi kuwa salama kama hatutafanya
zoezi hilo la dhamiri njema nililolisema. Maisha kila siku ni darasa. Hivyo
tujifunze kadiri tunavyopewa pumzi hii ya bure na Mungu Mwenyezi. Na “tutapewa
kuona tena” kama tupo tayari katika NENO-kusikia, kupokea, kutafakri,
kushirikishana, na kutoa ushuhuda wa kweli na haki kama tokeo la ishi yetu
katika hofu ya Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza,” Ufu 2:5a
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, niwezeshe kuona tena. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario