jueves, 17 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 33 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 33 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 11:4-12

Zab/kit: 144:1, 2, 9-10

Injili: Lk 20:27-40

Nukuu:

“Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi,” Ufu 11:4

 “Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua,” Ufu 11:7

 “Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama,” Ufu 11:11

wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:36

Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake,” Lk 20:38 

TAFAKARI:Wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo Yesu anawatoa wasiwasi wale waliomuuliza juu ya nani hasa atakaye kuwa mume baada ya maisha haya ya duniani ikiwa mwanamke huyo aliolewa na kurithiwa na ndugu saba wa familia moja. Yesu anawajibu na kuwaambia, “Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi,” Lk 20:34-35. Tukiwa hapa duniani ni wakati wa kuyafanya yote katika wema na haki. Hivyo, kesho yetu ni matokeo ya leo yetu.

Mahitaji yetu tuwapo hapa ulimwenguni ni tofauti na mahitaji yetu tukiwa mbingu kwenye uzima wa milele. Hivyo walioko huko kwenye uzima wa milele, “wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:36. Kwa sababu hiyo mahitaji ya kimwili hayana nafasi tena kwani tutakuwa na miili iliyotukuka na takatifuzwa, yaani, miili ya ufufuko.

Miili hii ya ufufuko inathibitisha ukweli kwamba Mungu wetu, si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake,” Lk 20:38. Ndugu yangu, kesho yako katika mikono salama ya Mungu inategemea leo yako katika mikono ya Mungu iliyo salama. Hivyo mtafute Bwana ungali hai kwani anapatikana, Isa 55:6-7.

Hata hivyo ipo gharama yake ya kuufikia mwili huo uliotuka na takatifuzwa, yaani, mwili wa ufufuko. Gharama yake na hasa katika mazingira yetu ya leo ambayo walio na nguvu ujiinua na kujifananisha na Mungu, ni kusimama katika kweli na haki. Ni kutokukubali kuogelea katika mkondo wa maji yao. Ni kutokufurahia wanayofurahia kwa sababu ni chukizo kwa Mungu mpenda haki, kweli, na mwenye kuthamini utu wa mtu kwa sababu kwa upendo wake alimuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake.

Na pale utakapo simama katika kweli na haki dhidi ya utawala wowote ule wa giza na dhalimu uwe tayari kuteseka, kuteswa, na hata kupoteza uhai wako. Na hili ndilo alisemalo Yohana katika somo letu la kwanza kuonyesha mfanano wa watu hao walio tayari kuifia kweli na haki, kwamba, “Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi,” Ufu 11:4. Watu hawa ishi yao, na hata kufa yao ni mpango wa Mungu kwa sababu kupia wao mapenzi yake Mungu hutimia. Katika kweli hii Mtume Paulo anasema, “kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8.

Na katika kuwa mikononi mwa Mungu bila kujibakiza, kwayo usalama upo. Hivyo “Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa,” Ufu 11:5. Lililo jema, na ambalo Mungu kalianzisha ndani ya watu hawa, Mungu ulisimamia hadi mwisho. Hivyo binadamu jeuri na asiyekuwa na hofu ya Mungu hatoweza zuiya mpango wa Mungu kwa watu wake. Na moja ya mpango wa Mungu kwa watu wake ni ile hali ya uhuru aliwapa ambayo hakuiondoa hata baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza. Je, wewe ni nani basi mwenye kutaka kuwaweka wana wa Mungu katika mifuko yako?

Kwa vile watu hawa walioyakabidhi maisha yao mikononi mwa Mungu, naye Mungu huwatumia kufikisha ujumbe wake na takwa lake, watu hawa “wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo,” Ufu 11:6. Kwa maneno mengine, Mungu huwapa nguvu na maono ya ajabu dhidi ya ufalme wa giza na dhuluma.

Mara nyingi, na hasa tuitazamapo historia ya Kanisa letu, mwisho wa wa watu hawa wasimamao katika kweli na haki huwa wa mateso makubwa. Ukweli ni kwamba, penye upendo wa kweli kuna mateso kwa sababu upendo utupeleka katika ukamilifu ambao wengi hatuutaka kutokana na hali ile ya umimi. Hivyo,  “Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua,” Ufu 11:7. Mnyama hapa yamaanisha mtu jeuri, tawala dhalimu, au falme za giza. Kuuawa kwao siyo kushindwa bali ni ushindi uliotukuka kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba, “chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazoa mengi,” Yoh 12:24.

Hivyo ukimya wao baada ya kuondolewa pumzi yao na mnyama huyo kutoka kuzima ni swala la muda tu. “Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa,” Ufu 11:8. Hali na mazingira haya ya ukimya kama siku ile ya Ijumaa Kuu ni muda wa kuzama katika tafakari ya kina. “Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini,” Ufu 11:9. Ni tafakari yenye kutupeleka katika mabadiliko ya kweli. Ni wakati wa kufanywa upya mwili, roho, na hata fikra zetu. Na ndio wakati wa kuona weupe na weuzi wa mnyama huyu alitoka kuzimu.

Kwa upande mwingine tendo la kuuawa hawa wasimamiao haki na kweli hutoa furaha kwa watesi wao kwa sababu kwa kutokuwepo watetezi hawa kwao ni wakati wa kupumua na kuufurahia udhalimu wao. Hata hivyo hili ni swala la muda mfupi sana. Mungu hawezi kamwe kuliacho chozi la kweli na haki lipotee bure. Na ndiyo maana kusema,  “Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi,” Ufu 11:10.

Ndugu yangu, mwisho wa jambo jema hata katika hali ya mateso na kifo, ni mwanzo mpya na nuru mpya ya kule tuendapo na kukutamani. Na hili ndilo linalomaanisha upya huo na ushindi wa mwenye haki dhidi ya uovu na dhuluma, kwamba,  “Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama,” Ufu 11:11. Naam, na mwisho wa mtu jeuri, asiye na hofu ya Mungu, na mwenye kujiinua sawa na Mungu, kwake kiama ni kikubwa!

Nao wateule wa Mungu walioutoa ushuhuda wa kweli na haki kwa maisha yao ndipo watakapo sikia “sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama,” Ufu 11:12. Na hili ndilo taji na ile mede tupasayo kuichuchumilia kila siku ya maisha yetu. Mede na taji hili ni tokeo la gharama ile uitoayo ili kuupata mwili huo uliotukuka na takatifuzwa, yaani, mwili wa ufufuko, hali ya Utakatifu, na ndicho cheo chako.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama,” Ufu 11:11

Tusali:-Ee Yesu tupiganie dhidi ya ufalme wa giza na uovu wake. Bila Wewe hatutoweza chochote. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario