JUMANNE WIKI YA 1
YA MAJILIO MWAKA-A
Somo: Isa 11:1-10
Zab: 72:1-2, 7-8, 12-13, 17
Injili: Lk 10:21-24
Nukuu:
“Basi
litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi
yake litazaa matunda,” Isa 11:1
“Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa
ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali
pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10
Saa
ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa
mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili;
umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk
10:21
“Akasema,
Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala
hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk
10:22
TAFAKARI:
“Kwake itasimama kweli, haki, Amani, na Upendo.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kumkomboa mwanadamu kutoka hali yake ya mateso, mahangaiko na
dhambi, Mungu aliye Kweli, Haki, Amani, na Upendo kwa makusudi makubwa anapenda
kuanzisha uhusiano na yule aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Tendo
hili la kuujenga uhusiano wa karibu nasi linamshusha Mungu chini kabisa katika
hali ya mwanadamu. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Kipindi hiki cha majilio ni
kipindi cha kutafakari upendo huu wa ajabu Mungu anaokwenda kutufanyia. Ikiwa
zawadi hii ni kubwa sana kwetu hatuna budi kujiandaa vizuri mwili na roho ili
atakapokuja atukute tupo safi na wenye afya njema hasa roho zetu.
Kufanikisha
mpango huu, Mungu huyu aliye Alfa na 0mega atachukua hali yetu ya kibinadamu,
na hivyo atazaliwa ikiwa ni moja ya kushiriki hali yetu ya kibinadamu. Jambo
hili linatabiriwa na Nabii Isaya. “Basi
litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi
yake litazaa matunda,” Isa 11:1. Je huyu
atakayezaliwa ataongozwa na mamlaka gani? Hakika kwa vile anakuja kuusimika
ufalme wa kweli, haki, amani, na upendo, “roho
ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza,
roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2. Hivi ndivyo vitendea kazi vyake.
Ujio wake kwetu ni hukumu pia ambayo itasimama katika haki. Hivyo, “kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya
wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4
Ujio wa mfalme huyu ni
ujio wa neema na baraka. Anakuja na kusimika mfumo wema na kuufifisha mfumo wa
uovu. Anakuja kuondoa sintofahumu zetu kati yetu wanadamu na viumbe vingine
alivyoviumba. Huyu hakika ni mfalme wa Amani. Hakutakuwa tena na sintofahumu
kati ya wanyama aliowaumba. “Mbwa-mwitu
atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na
mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza,” Isa 11:6.
Mwanadamu ataishi kwa amani na hofu haitakuwepo tena. “Na
mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia
mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8.
Uwepo
wa Mfalme huyu wa kweli, haki, amani na
upendo utajidhihirisha kwa utukufu wake.
Mataifa yote watamfuata alipo kwa sababu kuna Utukufu. “Na itakuwa
katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye
ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na
utukufu,” Isa 11:10. Haya ndiyo atakayoyafanya na kuujenga tena uhusiano wetu
ulioharibiwa na dhambi zetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, pamoja na hayo mazuri yote yaliyotabiriwa na Nabii Isaya kuhusu
Mfalme huyu tunayemsubiri kwa hamasa kubwa, yatawezekana tu kama tutakuwa
tayari kutoa ushirikiana naye. Mungu atukokoti kama Jemedari katili na mwenye
silaha za kutisha. Utawala wake ni utawala wa Upendo. Mungu hapendi kuondoa
uhuru na utashi wetu wa kumfuata. Ametuachia haya yote akijua kabisa kwamba kwa
kuyatumia vizuri ni njia rahisi ya kumfikia, hata pale tutakapoyatumia vibari
itakuwa njia rahisi pia ya kumrudia tukifanya toba ya kweli na majuto. Kwa
hiyo, ‘aliyekuumba wewe pasipo wewe hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,’ Mt.
Agustino wa Hippo.
Siri
ya ukweli huu wa kutoa ushirikia na
Mungu ili kuwa sehemu salama anausema Yesu katika Injili ya leo. Siri
hii ni kuwa kama watoto wachanga. Mtoto mchanga huamini yote kuwa salama
anapokuwa mikono mwa wazazi wake. Mtoto mchanga kamwe hawezi kuacha kutabasamu
hata kama akiwa mikononi kwa mtu mwovu. Maana yake ni kwamba, mtoto mchanga mara
zote anamtazamo chanya. Hii ndiyo hekima iliyofichwa ndani ya watoto wachanga.
Yesu anatutaka kuwa na unyenyekevu huu katika kuamini yote kuwa salama mikononi
mwa Mungu. Naye Yesu, “Saa ile ile
alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na
nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto
wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21.
Ndugu yangu
uliyesafiri nami katika tafakari hii, leo Yesu anatufunulia jambo la pekee sana.
Kwanza kabisa ni Yeye tu aliyekabidhiwa yote na Mungu. Pili hatuwezi kumjua
Mungu Baba pasipo Yeye mwana, yaani,
Yesu Kristo. Kwa maana hiyo, kuwa na Yesu ni kuwa kwenye mikono salama.
Naye Yesu, “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna
amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye
Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22. Je, ulipo na ulipojikabidhi kuna usalama?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Jina
la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama,” Mit 18:10
Tusali: Ee Yesu
Mwana wa Adam, nakuamini. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario