ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-C
Somo:
Ufu 5:1-10
Zab/kit: 149:1-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Lk 19:41-44
Nukuu:
“Kisha nikaona katika
mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu
kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1
“Na mmojawapo wa wale
wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la
Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,”
Ufu 5:5
“akisema,
Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa
yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42
“watakuangusha
chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu
hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk
19:44
TAFAKARI:
“Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii,
yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
bila shaka jamii yetu leo imehathirika na
ugonjwa huu wa “UDHAHAMO,” Upungufu wa Dhamira Hai Moyoni. Iweje leo unaona
binadamu mwenzako anauwawa kikatili nawe waona jambo hili ni sawa na halisemi
kitu chochote ndani ya nafsi yako? Inaingiaje akili leo kwa mkono wako unamwua
binadamu mwenzako kikatili na bado unajiona upo sawa? Unajionaje upo sawa pale
unapotoa ushauri juu ya kumdhuru mwenzako na hata kupoteza uhai wake? Wengi
husema mtu fulani kauliwa kinyama.
Mnyama
hawezi kumwua mnyama mwenzake wa familia ile ile kikatili hivyo. Huwezi kuona
Simba akimwua simba mwenzake kikatili kama anavyofanya binadamu kwa binadamu
mwenzake. Tuyaonayo kwa wanadamu leo ni ugonjwa wa UDHAHAMO. Binadamu aliyekufa
dhamiri ni sawa na Gari jipya lisilokuwa na breki. Hata kama dereva wake kafuzu
vizuri katika fani ya udereva lolote laweza kutokea njiani na kuwashangaza
wengi.
Mshango
kama huo unamkuta Yesu anapoutazama mji wa Yerusalemu na wakazi wake na uzuri
wa Hekalu. Kipindi cha Yesu, Wayahudi wengi hawakuwa wanaishi yale yaliyokuwa
yanampendeza Mungu. Torati haikufuatwa kama ilivyo, bali walifuata tafsiri ya
Torati na masimulizi ya wazee, TALMUD, ambao ulikuwa ukweli wa Mungu
ulipotoshwa. Yesu alijua mwisho wa kila kitu kuhusu mji huu wa Yerusalema na
fahari yake. Aliutazama, “akisema, Laiti
ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa
machoni pako,” Lk 19:42.
Salama
ya mji huu wa Yerusalemu ilikuwa ni kupatanishwa na Mungu kwa kuyaacha matendo
yao mabaya na kumrudia Mungu. Hekalu lenyewe lilikuwa kituo cha biashara. “Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale
waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia,
Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa
pango la wanyang'anyi,” Lk 19:45-46. Michanganyo katika Imani ni hatari sana.
Hata Yesu hakupenda michanganyo hiyo.
Ni
jukumu na wajibu wako na wangu kuishi imani ya kweli, na yeye kuenenda na
matendo. Na kadiri tuishivyo ndivyo hivyo hivyo tunavyojiandalia hukumu yetu ya
mwisho. Na siku hiyo ya mwisho kitakacho tokea ni hakikisho tu juu ya yale yote
tuliyoyaishi hapa duniani. Hakikisho hili ndilo litakalo amua uwe upande upi wa
Mwana-Kondoo. Kristo Yesu ndiye atakaye kuwa hakimu wetu wa haki na kweli. Hali
na mazingira hayo juu ya siku ile ya mwisho ndiyo anayotusimulia Yohana katika
maono yake, nakusema, “Kisha nikaona katika mkono wa kuume
wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na
nyuma, kimetiwa muhuri saba,” Ufu 5:1. Aliye keti juu ya kiti cha enzi ni Mungu
mwenyewe.
Simba wa Yuda, na Shina
la Daudi, ambaye ndiye mwana wa Adamu, ndiye mwenye kukifungua kitabu kile
ikiwa ni pamoja na mihuri yake saba, kama alama ya ukamilifu. Huyu ndiye mwenye
kuisoma hukumu ya haki na kweli. Hapata kuwa na uonevu wowote, kwani epuko la
kutokuingia hatia ni idadi ya miaka uliyopewa kuishi hapa duniani. Kila siku ni
mwaliko kwako na kwangu kuanza maisha mapya na yenye kumpendeza Mungu. Na hali itakuwa hivi, “Na mmojawapo wa wale
wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la
Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba,”
Ufu 5:5. Huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu.
Hukumu hii itashuhudiwa
na walio safi, na waliohesabiwa haki tayari, yaani, malaika na wateule wa
Mungu, Watakatifu. Naye Yohana anasema, “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi
na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama,
alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho
saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote,” Ufu 5:6. Yesu Kristo,
Mwana-Kondoo, ndiye atakaye kitwa “kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye
aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi,” Ufu 5:7. Kwa vile hakutakuwa na utetezi
zaidi ya hakikisho kwa yale uliyotenda, zoezi hili litasindikizwa na burudani.
Kwa walio haki baada ya
hakikisho hilo watafurahia milele, na wasio haki baada ya hakikisho hilo
itakuwa huzuni yao milele. Huzuni hii ni kiu au tamanio la kile ukipendacho
lakini hutokuwa na uwezo wa kikipata katika umilele wake. Na hali itakuwa hivi
juu ya burudani hiyo; na “Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na
wale wazee ishirini na wane wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao
ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya
watakatifu,” Ufu 5:8. Hakika ni furaha na masikitiko! Furaha kwa wenye haki, na
masikitiko kwa wasio haki.
Na ujumbe wa wimbo huo
mpya usindikizao hukumu hiyo ni huu; “Wastahili
wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa,
ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi,”
Ufu 5:9-10. Wimbo huu umebeba wasifu wa Mwana-Kondoo, Yesu Kristo, na hasa
ukitukumbusha thamani ya sadaka yake aliyoitoa kwa ajili yako na yangu pale
Msalabani. Ndugu yangu, wimbo huu uziamshe dhamiri zetu zilizolala au kufa.
Amina!
Tumsifu Yesu Kristo!
“watakuangusha
chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu
hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk
19:44
Tusali:-Ee Yesu, yaongoze
maisha yetu katika dhamiri njema kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario