sábado, 19 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 34 YA MWAKA-C, SIKUKUU YA YESU KRITO MFALME


JUMAPILI WIKI YA 34 YA MWAKA-C

Jumapili ya Mwisho wa Mwaka

Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme

Somo I: 2Sam 5:1-3

Zab: 122:1-2, 3-4a, 4b-5

Somo II: Kol 1:12-20

Injili: Lk 23:35-43

Nukuu:

Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako,” 2Sam 5:1

Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli,” 2Sam 5:3 

 "Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16

“Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake,” Lk 23:35

“Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa,” Lk 23:41

 Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura,” Lk 23:34

Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati,” Lk 23:44-45 

TAFAKARI: “Huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Na kama tu wana wa Mfalme Yesu Kristo, na ndivyo tulivyo, tufanane naye na tuenende katika Haki na Uzima, Utakatifu na Neema, Upendo na Amani.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya “34” ya Mwaka “C” wa Kanisa. Leo ni Dominika ya mwisho ya mwaka “C” katika mzunguko wake kadiri ya mpango wa kiliturjia. Ni kwenye Dominika hii ya mwisho ya Mwaka, Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme.

Wapendwa wana wa Mungu, wana wa Israeli hawakukata tamaa kwa anguko la Mfalme Sauli. Wote kwa umoja wao wanaona bado yapo matumaini kwa Mungu na mtu wa kuwavusha katika taabu na maangaiko yao ni Daudi. “Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako,” 2Sam 5:1. Kuwa sehemu ya mifupa na nyama ya Daudi kulimaanisha imani waliyokuwa nayo juu ya Daudi.

Kwa maana nyingine wana wa Israeli wapo tayari kushirikiana na Mfalme Daudi kwa kila jambo na bila usaliti. Hivyo “Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye Mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli,” 2Sam 5:3. Daudi anakuwa Mfalme wa Israeli na yupo tayari kutumika kwa manufaa ya watu na Taifa lake.

Ufalme wa Bwana wetu Yesu Kristo ni tofauti na falme nyingine zote zilizowahi kutokea na zitakazo tokea katika ulimwengu huu. Ufalme wa Kristo ulijidhihirisha kile atakachokuwa kuanzia pale alipomwilishwa na mwisho kuyatoa maisha yake kwa ajili ya dhambi zako na zangu, yaani, kifo cha msalaba. “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Msalaba Mtakatifu kwa sasa ndicho kiti chake cha hukumu ya Haki na Amani, Utakatifu na Neema, na Mapendo na Amani.

Kofia yake ya kifalme ni taji lake la miiba. Taji hili la miiba, kofia yake ya kifalme, ya yaiweka wazi tabia ya Ufalme wa Kristo, yaani, uvumilivu kwa kila aliyeridhia ufalme wake, unyenyekevu katika kuyajali maslahi ya wengine kwanza kabla ya kwako na yangu, huruma katika kuchukuliana na kusamehana ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kusikiliza hisia na maumivu ya wengine hata kama hayana ukweli na maana kwako. Hili ndilo taji la miiba!

Kwa kumwilishwa, yaani, neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yesu alikubali kuchukuwa mwili na hali ya mwanadamu bila kupoteza asili yake ya kimungu ili awe mkombozi wako na wangu. Hakika kwa kazi hii ilipaswa azaliwe kwenye mahekalu ya dhahabu na yaliyopambwa na nakshi za gharama kubwa. Badala yake tunaambiwa kwamba wachungaji walikimbilia Bethlehemu baada ya kuambiwa na malaika. “Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini,” Lk 2:16. Mfalme huyu anazaliwa horini kama alama na uthibitisho wa kutumika na siyo kutumikiwa.

Hali na mazingira ya kuzaliwa Mkombozi na Mfalme wetu, Yesu Kristo, yanatukumbusha na kutufundishwa mimi na wewe unyenyekevu katika maana ya kujitoa zaidi kwa wengine kuliko kujitazama wenyewe. Hapa mimi na wewe tunafundishwa upendo wa kweli unaojidhihirisha katika kujishusha chini kabisa katika hali halisi za watu. Upendo huu unafikia kilele chake pale msalabani ambapo Mfalme huyu Yesu Kristo anautoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake ambao ni wewe na mimi. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Huyu ndiye Kristo Mfalme tunayemsheherekea leo aliyekubali kutumika na kutaabika hadi toni la mwisho.

Katika tendo hili la kutojihurumia kuliko kwa hiari na upendo, katika kweli hii Yesu Kristo anadhihirisha kuwa yeye ni shahidi na mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, aliyetayari kutuosha dhambi zetu kwa damu yake, na kutufanya kuwa ufalme na makuhani wa Mungu. “Mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wawatakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:12-15

Huu ni upendo wa ajabu sana kwetu. Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele,” Ufu 1:5-6. Kwa nini basi nashindwa kupenda kama Kristo alivyonipenda?

Mamlaka ya Kristo ni ya milele na hivyo kumtenga na falme za leo na sasa. Ufalme wake ni ufalme usioangamizwa. “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Yesu akiwa kesha wambwa msalabani, Wayahudi wakiwemo na wakuu, wanahoji kwa kejeri asili na mamlaka ya Ufalme wa Yesu. “Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake,” Lk 23:35. Ni dharau na kejeli ya hali ya juu kwa kiumbe kumdhihaki muumba wake. Je, ingekuwe wewe ni Yesu katika hali na mazingira haya ungefanya nini?

Hata pamoja na kejeli hizi,  majeraha yake na uchungu wa mateso aliokuwa anaupata, Yesu hakujibu kwa jeuri, bali alikuwa tayari kutoa msamaha na kusema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura,” Lk 23:34. Huyu ndiye mfalme wa huruma. Leo baadhi yetu tena tuliopewa dhamana na umma kwa muda mfupi tu, tukikosolewa kidogo tu, tena kwa ukosoaji ule wa kujengana hatupo tayari kujirekebisha na badala yake tunakomoana kwa kuswekana jela. Kila kikichwa twafikiri namna ya kutengeneza mazingira ya kutokuguswa ili tuendele na umangi na ufalme meza. Kumbe ni vizuri ukampenda yule anayekuambia umekaa vibaya kabla ya kusanyiko kubwa la watu, ili kusanyiko kubwa hilo litakapotokea usije ambulia aibu na fedheha.

Mwisho wa pumzi yake hapa duniani, Yesu alituachia ishara ya utayari wake wa kuanza upya na kila mmoja wetu kwa kuvitoa vizuizi vyote ambavyo havikulandana tena na historia zetu, mila na tamaduni zetu, familia na koo zetu. Na ishara hiyo ndiyo hii; Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati,” Lk 23:44-45. Tangu kutokea kwa tukio hilo, hakuna tena ukuta wa kutuzuia kukutana na Mwokozi wetu, zaidi ya mali yako, na ukuta wako mwenyewe, yaani, dhambi zako. Kristo sasa ndiye mlango na daraja la kwenda ng’ambo ile tunayoitamani, yaani, uzima ule wa milele.

Hata pamoja na tendo hilo tendo hilo kubwa kulifanya wako na kwangu, Kristo Yesu, Mfalme wa haki, kweli, upendo, na mshamaha, “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8. Ee Yesu, na Mwokozi wangu, kwa tendo hili la upendo wako kwangu, nijisikie aibu na huzuni kwa dhambi zangu,  na mara nifanye kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi zangu ninapo tafakari upendo huu wa ajabu ulionitendea.

Tendo hilo la kukubali kudhalilishwa kiasi hicho, hakikumwondolea Bwana wetu Yesu Kristo Ufalme wake, mamlaka yake, wala Umungu wake. Badala yake, tendo hilo limejeuka kuwa ponya yetu na uhuru kwetu. Tendo hili ladhihirisha gharama na dhamani  kubwa ya kukombolewa kwako na kwangu, yaani, kwa damu yake Takatifu.

Wewe na mimi leo tuna thamani kubwa sana mbele ya Mungu kwa sababu tumekombolewa kwa gharama ya damu yake Yesu. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 18-19. Tendo hili pia licha ya kutufanya kuwa na thamani kubwa sana mbele ya Mungu, limetufanya na linatufanya matajiri. Kristo Yesu ni Mfalme mwenye nia thabiti ya wote wenye kumridhia kuwa wafalme kama Yeye (haki, upendo, msamaha, unyenyekevu, kweli, na amani)

Kwa tendo hili la kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, Kristo amekubali kuwa masikini ili wewe na mimi tuwe matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ni kwa ajili ya mambo haya makuu Kristo ni Mfalme na alizaliwa kwa ajili hiyo.

Kuja kwake ulimwenguni ni kuusimika ufalme huu na kweli yake. Yesu anamjibu Pilato swali lake la kejeli kuhusu kuwa yeye ni Mfalme. “Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu,” Yoh 18:37. Ndugu yangu wasimama katika kweli? Kama sivyo, basi elewa huisikii sauti ya Kristo. 

Wapendwa katika Kristo, Ufalme wa Kristo ni ufalme wa haki na uzima, ufalme wa utakatitifu na Neema, ufalme wa mapendo na amani. Nasi kwa upendeleo mkubwa tu wana wa ufalme huu kwa sakramenti ya ubatizo. Kwa sakramenti hii tu wana na warithi wa Ufalme wa Kristo na Mungu wetu hasa pale tunapoishi ahadi zetu za ubatizo. Hivyo mimi kama mwana wa Mfalme Yesu Kristo, nifanane naye na kusimama katika Haki na Uzima, Utakatifu na Neema, Upendo na Amani.

Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa lengo la kwanza la kuumbwa kwetu na kukombolewa kwetu lililenga kujenga mahusiano mazuri na muumba wetu, basi lengo la pili tuwapo hapa duniani ni kuudhihirisha ufalme wake. Hapa ninaudhihirisha ufalme wake Kristo kwa kuishi na kusimamia ufalme wa haki na uzima kwa kuyafanya mazingira ninayoishi yawe ya haki na kuchanua kwa uzima wa roho na mwili. Niudhihirishe ufalme wa Mungu kwa kuishi maisha ya utakatifu na neema.

Maisha hayo yawe chachu kwa wengine wamwone Kristo kupitia kwangu, na kuwa barua ya kusomwa na wengine. Mtume Paulo anawaambia wakristo wa Korintho, Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama,” 2Kor 3:2-3.

Kuishi tena na tena ni ‘kupenda bila kipimo kama mizania halisi ya upendo,’ na ndivyo atufundishavyo Mtakatifu Augustino wa Hippo. Kielelezo cha upendo huu ni Kristo mwenyewe. Naye Yesu anasema, Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Kumbe nisipokuwa tayari kwa ‘upendo sadaka,’ ishi yangu inaulakini mkubwa. Palipo na upendo kuna maumivu kwa sababu lengo la upendo ni kuufikia ukamilifu katika uzima wake, na siyo vipande vipande katika ubinafsi wa kitu. Maumivu huja kwa sababu upendo ukubandua katika vifungo vya umimi na kukurejesha katika sura halisi ya Mungu, na hivi ndivyo ulivyo umbwa, yaani, kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Kristo kwa kutupenda upeo, Yoh 13:1, aliutoa uhai wake ili mimi na wewe tuishi na kuhesabiwa haki kama wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake wa milele. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni,” Kol 1:19-20. Ndugu yangu, huyu ndiye Kristo Mfalme tunaye msheherekea leo.

Wapendwa wana wa Mungu, mamlaka aliyokuwa nayo Yesu (Nguvu na Uweza) ni vita dhidi ya uovu hapa duniani. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa jina lake tunapata uponyaji wa kweli. “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6.  Mamlaka ya Yesu yamejengwa chini ya mamlaka ya Mungu, naye ni Mungu, na pasipo Yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika, Yoh 1:1-3.

Hivyo hakuna jambo lolote alifanyalo Yesu lisilo kuwa na uhusiano na Mungu, huku jambo lile likifunua siri ya Mungu kila kukichwa. “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16. Kwa nini basi nakuwa na mashaka juu ya utendaji wa Kristo katika maisha yangu?

Mwisho, nikiwa hapa duniani yanipasa kuudhihirisha Ufalme wa Upendo, Haki na Amani. Ili mazingira ninayoishi na ulimwengu ninaoishi na kunizunguka uwe na mapendo, haki na amani, yanipasa muda wote nijihangaishe kwa ajili ya kuwa mpatanishi. Yesu hasemi ‘heri wenye upendo, au heri wanaojua kupenda wataitwa wana wa Mungu,’ bali ‘heri wapatanishi.’ “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9. Hivyo kuudhihirisha ufalme wa mapendo, haki na amani, yanipasa kuwa mtapatanishi na ndipo nitaiwa mwana wa Mungu na mrithi wa ufalme wake.

Kutafuta amani siyo KUEPUKA MGOGORO, kukimbia mgogoro, kujifanya hakuna TATIZO au kuogopa kuliongelea tatizo kwa kuwadhibiti watu. Huo ni woga na mwisho wa siku ujeuka kuwa uasi. Yesu, mfalme wa amani, hakuogopa kamwe migogoro. Mara nyingine aliuchochea ukatokea kwa faida ya wote. Wakati mwingine tunatakiwa kuepuka migogoro, wakati mwingine kuisababisha, na wakati mwingine tunahitaji kuitatua. Lengo liwe kwa faida ya wote. Ndiyo maana tunapaswa kuomba uongozi wa Roho Mtakatifu daima.

Kuleta amani siyo KUTULIZA HASIRA. Mara nyingi itakubidi kukubaliana katika kweli na haki. Kuwa kama jamvi kwa nia ya ujamvi tu, na kuwaruhusu wengine wakukanyage sivyo alivyokusudia Yesu. Alikataa kuacha mambo kama yalivyo, na akachukua msimamo mbele ya upinzani wa waovu.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii; Ni heri kwenda Mbinguni ukiwa na suruali iliyotoboka makalio kwa sababu ya kuhangaika kwa ajili ya kuwa mpatanishi, kuliko kwenda jehenamu ukiwa umevalia suti na tai.

Ni kwa maana hiyo, heri kwenda mbinguni na kuufurahia Ufalme wa Mungu ukiwa na kandambili zilizo kwisha kisigino, kuliko kwenda kwenye mateso jehenamu ukiwa umevalia mokasini zenye kisigino cha chuma ya dhahabu.

Ni heri kwenda mbinguni ukiwa na jina la Lofa kwa sababu ya kupigania haki za wanyonge, uzima na usalama wao, kuliko kwenda jehenamu kwa jina la Luatani.

Ni heri kwenda mbinguni na kuufurahia Ufalme wa Mungu ukiwa mikono mitupu na maisha ya neema, kuliko kwenda jehenamu ukiwa milionea.

Ndugu yangu, hakuna dharau au kukashifiwa kuliko pindukia, na matusi ya kila aina ambayo Yesu hakuyapata. Aliyakubali yote kwa sababu alitupenda upeo ili leo mimi na wewe tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi. Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote,” Zab 145:13

Tusali:-Ee Yesu Mwema na Mfalme wangu, nijalie neema ili nisijitenge na Ufalme wako. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario