ALHAMISI WIKI YA 34 YA MWAKA-C
Somo:
Ufu 18:1-2, 21-23, 19:1-3, 9a
Zab/kit:
100:2, 3, 4, 5
Injili: Lk 21:20-28
Nukuu:
“Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka,
umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho
mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza,” Ufu 18:2
“kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki,”
Ufu 19:2a.
“Hapo
ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na
utukufu mwingi,” Lk 21:27
“Basi mambo hayo
yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu
umekaribia,” Lk 21:28
TAFAKARI:
“Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, Mungu huyu aliye hai anaonekana katika
uhalisia wake kupitia kazi za Mwanaye Yesu Kristo Mkombozi wetu. Huyu ndiye
aliyetumwa kukomboa kile kilicho anguka kwa sababu ya dhambi. Huyu ndiye
Mwana-kondoo wa Mungu, na “Heri walioalikwa karamu ya arusi ya
Mwana-Kondoo.
Hivyo,
pamoja na mambo mengi ya kutisha mwisho wa nyakati, na hasa kuharibiwa kwa
hekalu la Yerusalema na watu wake kuteswa na kupelekwa utumwani, Mungu hata acha
kamwe kuonyesha Nguvu na Utukufu wake. “Hapo
ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na
utukufu mwingi,” Lk 21:27.
Na hii ndiyo
itakayokuwa ishara ya mwisho kwetu kuhusu mwisho wa nyakati. “Basi
mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa
ukombozi wenu umekaribia,” Lk 21:28. Huu ni ule ukombozi wa siku ya mwisho,
licha ya kweli kwamba kila siku tunapewa nafasi ya ukombozi huo.
Basi ndugu yangu
tutumie fursa tunazopewa na Mama Kanisa kila siku na hasa kupitia Masakramenti
yake ili tupata wokovu huo. Kiama kina hofu
kwa wale wasio mwamini Mungu aliye hai.
Kuna anguko kubwa sana
kwa wale wanaojikweza na kujifananisha na miungu ilhali wao ni binadamu tu. Na
hiki ndich alichokitabiri Nabii Isaya na kusema, “Macho ya mwanadamu
yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa naye
Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana
wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka;
nayo yatashushwa chini. Isa 2:11-12.
Yohana analiona anguko
hilo la mwanadamu anayejiinua na kujilinganisha na Mungu, lililoashiriwa na
Malaika aliyelia “kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu;
umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila
ndege mchafu mwenye kuchukiza,” Ufu 18:2. Si vyema kujikweza na kuwakweza
wengine kwa matendo yetu yasiyo na mafaa wala ufahamu. Sote tu mavumbi, na
mavumbinu siku moja tutarudi.
Makwazo kwa wanyofu wa
moyo ni chukizo kubwa sana kwa Mungu. Na katika jambo hili Yesu anasema, “Na ye
yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe
jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Mk 9:42. Kufungwa jiwa na
kutupwa baharini kunamaanisha hakutakuwa na uwezekana wowote ule wa wewe
kunusurika na hata kuoneakana katika maana ya kuelea juu baada ya kufa maji.
Yote haya ni kuonyesha uzito wa kuwakwanza wengie, na hasa wale walio na imani
changa, na wanyofu wa moyo kama watoto wadogo.
Hili nalo analiona
Yohana katika maono yale na kusema, “Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua
jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi,
kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena
kabisa,” Ufu 18:21. Hata hapa hakutakuwa na uwezekano wa kuonekana tena kwa
sababu ya dhambi hii ya makwazo.
Viashirio vyote hivi kuhusu mwisho wa nyakati
vinatuelekeza kufanya mabadiliko ya mwili na roho, leo na sasa. Kengele
ikishagongwa, yaani, ukishavuta pumzi yako ya mwisho, na mbaya zaidi pasipo
mabadiliko hayo, kifuatacho ni kulia na kusaga meno, Lk 13:28. Kwa maana hiyo, “Wala sauti ya wapiga
vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu,
haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yo yote
hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa
ndani yako tena kabisa,” Ufu 18:22. Hakuta kuwa tena na muda. Na mtego mbaya
kupita yote, na ndiyo njia anayoitumia yule mwovu ni kukusadikisha kwamba bado
una muda wa kutosha, na yote utayafanya tu. Kesho nyingine ipo, wala hakuna haraka.
Ndugu yangu, yatupasa kukesha tukiwa na taa
zetu zinawaka na zikiwa na mafuta tusije dondoka katika mtego ule wa wanawali
wale watano wapumbavu waliobeba taa zao wasibebe na mafuta, Mt 25:1-12.
Yatupasa mara zote kuishi pasipo hatia, yaani, kuishi maisha yasiyo na
pingamizi, huku taa zetu zikiwa zinawaka muda wote ikiwa ni pamoja na
kuyashiriki masakramenti katika hali ya usafi.
La siyo ndugu yangu
tutapigwa butwaa Yesu atakapotujibu, “amini, nawaambia, siwajui ninyi, Mt
25:12. Kwa jibu hili ya Yesu, “wala nuru
ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na
bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako
walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako,”
Ufu 18:23. Ndugu yangu, ngoja ngoja yako mwisho wa siku itakuumiza tumbo!
Wote wale watakaokutwa
wakiishi pasipo hatia, yaani, bila pingamizi, na taa zao zinawaka na zina
mafuta ya kutosha, kwa maana nyingine, wanashiriki vyema neema na baraka za
Mungu kupitia Masakramenti yake, hawatakuwa na sababu ya kuogopa. Hawa
wataisikia sauti ya wateule wale wa Mungu ikisema, “Haleluya; wokovu na utukufu
na nguvu zina BWANA MUNGU wetu,” Ufu 19:1
Katika kweli hii na
mazingira haya, hakuna hata mmoja wetu atakaye onewa kwa sababu kila sekunde ya uhai wewe na mimi tunapewa muda wa
kufanya mabadiliko, “kwa kuwa hukumu zake (Mungu) ni za kweli na za haki,” Ufu
19:2a. Je, wausubiri mwisho usioujua, na ambao haupo chini ya uwezo wako? Kwa
nini basi nashindwa kuchukua hatua sana ningali bado na ufahamu wa kutosha?
TAFAKARI NA CHUKUA HATUA!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi mambo hayo yaanzapo kutokea,
changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia,” Lk
21:28
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie neema na nguvu ili nitumie vyema rasilimali muda unayonipa kila
siku ya maisha yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario