ALHAMISI WIKI YA 1 YA MAJILIO
Somo: Isa 26:1-6
Zab: 118:1, 8-9, 19-21, 25-27a
Injili: Mt 7:21, 24-27
Nukuu:
“Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani
kamilifu, kwa kuwa anakutumaini,” Isa 26:3
“Mtumainini
Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele,” Isa 26:4
“Si kila mtu
aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye
afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21
“Basi
kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye
akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25
TAFAKARI:
“Afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni ndiye atakayeingia katika ufalme
wa mbinguni.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kila kitu chenye uhai kwacho chenyewe au kundi huongozwa na
mamlaka fulani. Ni kweli pia hata kwa upande wa mwanadamu katika ishi yake
ikiwa ni pamoja na fikiri yake, tenda yake, amini yake, husukumwa na kitu
fulani. Ukweli huu ni pamoja na kundi la watu ambao pia kwa kukaa pamoja
husukumwa na nguvu ya mfumo fulani. Nguvu hizi au misukumo hii tunapoitimiza
kama ilivyo ndiyo kwa namna hiyo tunalandana nayo na kujishikamanisha nayo.
Huku ndiko kuwa na utii wa kweli katika mamlaka hizo kwani kwa kupitia utii huu
tumeshikamanishwa na kile kinachotusukuma (mamlaka) kufanya hivyo.
Ndugu
zangu katika Kristo, Injili ya leo inatuweka wazi kwa kutufunulia ni kipi
kipasacho kusukuma maisha yetu. Kitu hicho ndicho kinachotakiwa kuwa na mamlaka
juu ya maisha yako. Yesu anatupa angalizo na kusema, “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Kwa maana
nyingine unaweza kuwa Mbwekaji mzuri sana kwa kuwapendezesha watu
wanaokuzunguka kwa kuwaaminisha pasipo kumaanisha, ukawa kama Mbwa anayebweka
usiku kucha kumwaminisha tajiri yake kwamba ulinzi upo, kumbe ni woga wa miluzi
ya upepo. Kumbe ukweli ni kwamba, ni yule tu “afanyaye
mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni (Mungu) ndiye atakayeingia katika ufalme
wa mbinguni.” Je, kufanya mapenzi ya Mungu kunamaanisha nini?
Wapendwa
wana wa Mungu, kufanya mapenzi ya Mungu ni “kukaa katika pendo” la Mungu. “Nasi
tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo,
naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake,”
1Yoh 4:16. Ni kuwa tayari kuongozwa na mamlaka ya Mungu katika mfumo wa Upendo.
Tunakaa katika upendo wa Mungu kwa kuyatimiza mapenzi yake pale tu
tunapolipokea neno lake, tunapolisoma neno lake, tunapolifanyia tafiti neno
lake, tunapolikumbuka neno lake, na tunapolitafakari neno lake.
Haya mambo matano ni
muhimu sana kama tunataka kweli kukaa naye na kuyafanya mapenzi yake. “Basi
kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye
akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Hakuna awezaye
kutung’oa kwenye mwamba huu wa imani hata kikija kimbunga cha tsunami.
Tusipo lishika neno la Mungu vizuri tutakuwa
tayari kuongozwa na mamlaka hizi; mila zetu (kwa kufanya yale yanayotutia hofu
bila kuhoji sababu yake), desturi zetu (kwa kufanya kadiri ya mapokea ya wazee
wetu katika hali ya upofu), hisia zetu (kwa kufanya kadiri ya miyeuko yetu na
siyo utashi wetu). “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye,
atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo
zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt
7:26-27. Hakika kwa hali hii tunabaki kuwa kama bendera fuata upepo. Na kwa
sababu hiyo, kila ajitokezaye na kutushawishi hatutakuwa na nguvu ya kuimili
vishindo vya imani kwani tu wepesi kama pamba.
Hivyo ndugu zangu
katika kipindi hiki cha majilio tunapomsubiri Masiha wetu tukae katika neno la
uzima. Ni katika hali hii kwamba Mungu “atamlinda
yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa
anakutumaini,” Isa 26:3. Mungu wetu
ndiye mwamba wetu wa milele. Tumia muda wako vizuri kulitafakari neno lake la
uzima. Kama unaweza kutumia masaa mawili au matatu kwenye runinga, tenga basi
hata robo saa kulisoma neno la Mungu na ubaki nalo kwani ndilo lenye uzima. “Mtumainini
Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele, kwa
kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi,
auleta hata mavumbini,” Isa 26:4-5. Yote yanayotupa matumaini leo na sasa bila
Mungu hufifia kama mkaa wa mabua ya mahindi.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kila
akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala
hakumtambua,” 1Yoh 3:6
Tusali:-Asante
Ee Yesu na Mwokozi wangu, kwa sababu kwako kuna uzima wa milele. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario