miércoles, 16 de noviembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 33 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 33 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 10:8-11

Zab/kit: 119:14, 24, 72, 103, 111, 131

Injili: Lk 19:45-48

Nukuu:

“Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi,” Ufu 10:8

“Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali,” Ufu 10:9b

 “Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi,” Ufu 10:11

 “Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:46

“Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza,” Lk 19:47-48

TAFAKARI: “Kwa Ubatizo wako nawe umetengwa kwa kazi maalum. Naam, umewekwa wakfu.”

Wapendwa wana wa Mungu, umuhimu wa kile kilichowekwa wakfu na kwa ajili ya matumizi rasmi ndicho kisemacho katika Injili yetu ya leo. Yesu anaingia hekaluni na kukuta yawiyoendana na hadhi ya Hekalu. Hekalu limegeuka kuwa kituo cha uchuuzi, biashara. Naye anawaambia, “Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:46. Nyumba ya Mungu pamoja na kutolea sadaka na shukrani zetu ni nyumba ya sala.

Yote yale yasiyokuwa na uhusiano wa sala, shukrani, sadaka, na mengine kama hayo, hayapaswi kufanyika mahali hapa. Kabla ya kuteswa, kufa, na kufufuka kwake Bwana Yetu Kristo alijiweka wakfu kwa ajili yetu na kutufanya kuwa viungo vyake akiwa yeye ndiye Mwili, yaani Kanisa. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh 17:19.

Kanisa kama mwili wa Kristo, ni kwa namna hiyo ya kutakaswa kupitia Sakramenti ya ubatizo nasi tunakuwa viungo vya Kristo, na miili iliyowekwa wakfu kwa kushiriki ukuhani wa kawaida wa Kristo. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake,” 1Kor 12:12, 27. Kwa maana hii, miili yetu imewekwa wakfu ndani na katika Kristo.

Hivyo matendo yote machafu katika mwili ni kwenda kinyume na kutengwa huko kuliko wekwa wakfu kwa ajili ya Kristo. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!” 1Kor 6:15.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na miili yetu kuwa ni viungo vya Kristo na kuwekwa wakfu kwa ajili ya Kristo, mwili wa mtu ni Hekalu la Roho Mtakatifu. “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu,” 1Kor 6:19-20. Ndugu yangu, na kilichowekwa wakfu na kibaki kwa ajili hiyo daima.

Yohana kwa maono yale juu ya Mbingu na Hukumu ya mwisho, kama chombo, anaandaliwa na kuwekwa wakfu, yaani, kutengwa kwa kazi maalumu. “Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi,” Ufu 10:8. Hili ndilo neno la uzima, na ndani yake twajifunza kweli juu ya Mungu.

Hata hivyo ili kutoa ushuhuda wa kweli juu ya neno hili la uzima, yakupasa kupitia hatua nne muhumu. Nazo ni kama ifuatavyo, moja, KULISIKIA neno, mbili, KULIPOKEA neno, tatu, KULITAFAKARI neno, na nne, KULISHIRIKISHA neno. Kwa mantiki hii, ni vigumu kutoa ushuhuda wa neno kwa wengine kama huwezi kushirikisha NENO. Hutoweza kulishirikisha NENO kama hujalitafakari. Huwezi kulitafakari NENO kama ukulipokea. Na hutoweza kulipokea NENO kama hukulisikia.

Hivyo Malaika wa Mungu anamwambia Yohana, “Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali,” Ufu 10:9b. Maana yake nini? “Kukitwa kitabu” ni kulisikia Neno na kulipokea. “Kukila kitabu,” ni kulitafakari Neno. Na “kutiwa uchungu,” ni kulishirikisha Neno. Na utamu wa “kitabu,” yaani, ujumbe wa Neno, ni kutoa ushuhuda pasipo woga. Ni kuishuhudia Imani bila woga. Ni kuishi Imani kwa sababu Neno sasa linakupa Uzima. Na habari yenyewe ndiyo hii, kama asemavyo Yohana, “Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu,” Ufu 10:10.

Na utoaji wa unabii, ndiyo ushuhuda wa kile kikutiacho uzima na nguvu. Furaha ni kama kikohozi huwezi kukizuia. Uzima huo siyo kwa ajili yako tu, bali yakupasa kuupasisha kwa wengine pia. Na ndiyo maana ilimpasa Yohana  “kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi,” Ufu 10:11. Ujumbe huu siyo kwa yale tu wayapendayo watu kuyasikia, bali hata yale wasiyoyapenda ila yanawapa uzima wa kweli. Hata baadhi ya dawa huwa chungu, ila tokeo lake ni uponyaji. Na lengo msingi hapa ni kufinyangwa na kuwa na umbo la kimungu; yaani, upendo wake, haki yake, kweli yake, huruma yake, na msamaha wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:46

Tusali: Ee Yesu Mwema, nijalie kuishi ahadi za ubatizo wangu kwa uaminifu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario