sábado, 19 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 34 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 34 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 14:1-3,4b-5

Zab/kit: 24:1-2, 3-4ab, 5-6

Injili: Lk 21:1-4

Nukuu:

“Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao,” Ufu 14:1

 “Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa,” Ufu 14:4

“Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,” Lk 21:3-4

TAFAKARI: Je, najitoa vya kutosha?

Wapendwa wana wa Mungu, kusimama katika kweli na kujitoa bila kujibakiza ndiyo mfumo aupendao Kristo hasa pale tunapoishi katika mazingira ya kubaguana kutoka na hali na historia zetu. Katika utoaji wa sadaka, mwanamke mjane anahesabiwa haki kwa tendo la kujitoa bila kujibakiza. Yesu Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,” Lk 21:3-4.

Je ndugu yangu umejitoa vilivyo? Ni katika kutoa bila kujibakiza kunakuwa kwako silaha za haki. Hivyo, “wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki,” Rum 6:13. Kama wafuasi wa Kristo nielewe kwamba pale nilipo ninamwakilisha Kristo katika kweli na haki.

Na tokeo la kujitoa kama ulivyo na bila kujibakiza ni kuhesabiwa haki pia baada ya maisha yako hapa duniani. Naye Yohana anasimulia maono yake kuhusu yale aliyoyaona huko mbinguni, “nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao,” Ufu 14:1. Ujumbe ni kwamba, hapa duniani waweza kufanya ujanja wa kila aina, ila hata ukifanikiwa kuingia mbinguni kwa ujanja ujanja hutofurahia hali hiyo kamwe, na kama kutakuwa na nafasi ya kuchoropoka, basi utakimbia haraka.

Sababu hasa ya kuchoropoka haraka huko mbinguni ni kutokana na kutoendana na hali hiyo ya Mbinguni. Elewa uwapo hapa duniani ndivyo unavyoiandaa hali hiyo. Maandalizi yetu ya maisha ya uzima wa milele yanaanza hapa hapa duniani. Na kwa sababu hiyo, Yohana katika maono yake anatuambia hivi, pamoja na watakatifu hao kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, “wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi,” Ufu 14:3. Hivyo ikiwa kwa ujanja wako utafanikiwa kuingia mbinguni utajiondokea mwenyewe kwa sababu utaonekana wazi kuwa ni mzamiaji.

Hivyo wataeule wa Mungu katika mastahili yao hawatakuwa na shaka yoyote kwa sababu uwepo wao umekidhi kiwango na mastahili yake. Ndugu yangu, wateule “Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa,” Ufu 14:4. Mimi na wewe leo tunaoivuta pumzi hii ya uhai tuelewe kwamba maandalizi ni leo na sasa kwa sababu hakuna ajuaye nukta ijayo ya maisha yake hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo,” Ufu 14:4a

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nijalie nife kifo chema. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario