Somo
I: 2 Mak 7:1-2, 9-14
Zab/Kit: 17:1, 5-6, 8b, 15
Somo II: 2The 2:16-3:5
Injili:
Lk 20:27-38
Nukuu:
“Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya
sasa, lakini Mungu wa ulimwengu attufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri
zake, hata tupate uzima wa milele,” 2Mak 7:9
“Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na
kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe
hakuna ufufuo,” 2Mak 7:14
“Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa
na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na
kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi,” Lk 20:34-35
“wala hawawezi kufa
tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile
walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:36
“Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa
kuwa wote huishi kwake,” Lk 20:38
“Na Bwana wetu Yesu
Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na
tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika
kila neno na tendo jema,” 2The 2:16-17
“Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la
Mungu, na saburi ya Kristo,” 2The 3:5
TAFAKARI:
“Mungu wetu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 32 ya mwaka “C” wa Kanisa. Wazo Kuu la
leo ni ‘uwepo wa Mungu wetu ambaye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa
kuwa wote huishi kwake.’ Hivyo hatuna kitu chochote cha kupoteza hata kama
katika hali ya mateso na dhiki nyingi uhai wetu utaondolewa kwa hila za
mwanadamu. Mwanadamu kwa ulevi wa madaraka, nguvu, sifa, ufahari, na utajiri
haweza kuibatilisha dhima ile aliyopewa na umma wa watu, na kuifanya shubiri
kwao. Hapa ndipo mwanadamu anapojichukulia maumbile na ukuu wa Mungu.
Katika hali na
mazingira kama haya, Yesu anatutaka tusimame katika kweli na haki, na wala
hakuna cha kuogopa hata kama twafikwa na mauti. Naye anasema, “Msiwaogope
wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye
kuangamiza mwili na roho pia katika jehenum,” Mt 10;28; Lk 12:5. Pale
kunapokuwa na utawala kandamizi juu ya watu, na kujiinua kwa tawala hiyo
mithili ya malaika walio hasi na mfano wa miungu, jamii husika hujawa na hofu,
na hata wakati mwingine huweza kumwasi Mungu kwa kuzitii mamlaka hizi za giza.
Jambo hili linapotokea ni chukizo kubwa sana mbele ya Mungu.
Somo letu la kwanza
linatufundisha kuwa na hofu ya Mungu, na kusimama katika kweli na haki pasipo
maasi. Ndugu wale watatu wa familia mmoja wanalazimishwa kuonja nyama ya nguruwe ingawa kwetu leo
lingetokea zoezi hilo lingekuwa heri kwa sababu kwa walio wengi ni kitoweo
kipendwacho sana. Ila kinacholengwa katika somo hili la kwanza ni shuruti ile
ya kulazimishwa kwenda kinyume cha dhamiri iliyo njema na safi kwa kumridhisha
mwanadamu ambaye kwake yeye kama alivyo hana uzima huo wa milele ndani yake.
Ndugu hawa wapo tayari kufa kuliko kwenda kinyume cha dhamiri zao. “Sisi tu
tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu,” 2Mak 7:2b. Tupo kama tulivyo,
yaani, jamii husika kutokana na mazingira, mila, na desturi tulizokulia. Na kwa
asilimia kubwa mila na desturi hizi zimebeba uhai wa watu na ndiyo maana jamii
husiku uendelea kuishi na kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
Jambo la kushangaza ni
pale mmoja wa jamii husika kwa kulewa kilevi cha madaraka anajaribu kuvunja
utaratibu ulio mzuri kwa kujiimairisha na kujitukuza kusiko kwa mafaa wala afya
kwa jamii husika. Kuiokoa ama kuikomboa jamii husika kila mwenye hofu ya Mungu
yampasa kusima katika kweli na haki kukemea uovu huu wa wazi na ulio moja kwa
moja katika kuleta maumivu kwa watu pasipo sababu yoyote zaidi ya kujiinua kwa
tawala dhalimu. Mmoja ya ndugu hawa watatu anatoa ujumbe sawiya kwa tawala hii
dhalimu na kusema, “Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini
Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata
tupate uzima wa milele,” 2Mak 7:9. Ndugu yangu tunaye safiri sote katika
tafakari hii, ni vyema ukajua wa kuogopwa na Mungu peke yake. Huyu ndiye mwenye
mambo yote, yaani, “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu,
tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena
huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka
jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;
Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” 1Sam
2:6-8
Historia ni mwalimu
mzuri sana katika maisha. Hakuna tawala yoyote ile iwe ya kiustarabu au ya
kiimla iyodumu katika umilele wake. Huu ni ujumbe kwetu kwamba mtawala katika
umilele wake ni Mungu peke yake kwa sababu wote huishi kwake, Lk 20:38b. Ni
kweli kunakupoteza ili kupata hata kama haki hiyo itacheleweshwa, ila ahadi ya
Mungu kwa watu wake itasimama kama ilivyo mbele ya macho yake na kamwe haiwezi
kupotezwa. Na huu ndio msimamo wa mmoja wa ndugu wale waliolazimishwa kuionja
nyama ya nguruwe; “Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu
navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena,” 2Mak 7:11.
Leo pamoja na binadamu
kuwa na ufahamu mkubwa juu ya mazingira yake, na uwepo wa binadamu mwenzake
ambaye naye ana haki sawa na huyu anayoisimamia haki hiyo, lakini jambo la
ajabu ni kwamba binadamu huyu amekuwa mwepesi kuikandamiza haki hiyo na
kuwafanya mwenzake waishi kama panya na watumwa katika mazingira yao. Je,
tuyafanyapo haya kwa wenzetu twakiona kifo mbele yetu? Na kama hatukioni kifo
mbele yetu, Je, waifikiria kesho yetu? Ubatili hauwezi kudumu katika umilele
wake kwa sababu hauna mfanano na Mungu wala ukuu wake. Hivyo “Ni vema kufa kwa
mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa
naye. Lakini kwako wewe (Mdhalimu) hakuna ufufuo,” 2Mak 7:14. Na ngoma ikiwamba
sana ni ujumbe pia inakaribia kupasuka.
Yesu katika Injili ya leo anawatoa wasiwasi wale waliomuuliza
juu ya nani hasa atakaye kuwa mume baada ya maisha haya ya duniani ikiwa
mwanamke huyo aliolewa na kurithiwa na ndugu saba wa familia moja. Yesu
anawajibu na kuwaambia, “Wana wa
ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini,
wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika
wafu, hawaoi wala hawaolewi,” Lk 20:34-35. Tukiwa hapa duniani ni wakati wa
kuyafanya yote katika wema na haki. Hivyo, kesho yetu ni matokeo ya leo yetu.
Mahitaji yetu tuwapo hapa duniani/ulimwenguni ni tofauti na
mahitaji yetu tukiwa mbinguni kwenye uzima wa milele. Hivyo walioko huko kwenye
uzima wa milele, “wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika,
nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:36. Kwa sababu
hiyo mahitaji ya kimwili hayana nafasi tena kwani tutakuwa na miili iliyotukuka
na tukufuzwa. Miili ya ufufuko. Ukweli huu unathibitisha kwamba Mungu wetu, “si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa
wote huishi kwake,” Lk 20:38. Ndugu yangu, kesho yako katika mikono salama ya
Mungu inategemea leo yako katika mikono ya Mungu iliyo salama (katika kweli na
haki). Hivyo mtafute Bwana ungali hai kwani anapatikana. Ni kuishi katika hofu
ya Mungu.
Na tumaini letu katika nyakati hizi za
sintofahamu ndilo hili; “Bwana
wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya
milele na tumaini jema, katika neema, awafariji
mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema,” 2The 2:16-17.
Hakuna lisilowezekana kwa Mungu.
Tangu sasa ndani na katika Kristo Yesu, neema na baraka
zimefunguliwa kwa watu wote. Mlango huu umefunguliwa hata kwa wale walioonekana
ni wapagani kwa njia ya maono ya Petro alipokuwa akisali na mbingu zikafunguka,
na chombo kikashuka kama nguo kubwa, wakiwemo aina zote za wanyama wenye miguu
minne, watambaao, na ndege wa angani, Mdo 10:11-12. Kadiri ya maono haya Petro
alisita kupokea maagizo ya Mungu kwa sababu ndani yake walikuwepo wanyama wale
waliokatazwa kuliwa nao ni najisi, Mdo 10:14. “Pamoja
na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio
na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na wibari, kwa sababu yeye hucheua
lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na
sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo
kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga
yao; hao ni najisi kwenu,” Law 11:4-8. Na hiki ndicho kisa tulichokiona katika
somo letu la kwanza leo. Ndugu wale hawakuwa tayari kwenye kinyume cha dhamiri
zao juu ya mapokeo na mafundisho ya wazee wao.
Kipindi
cha Yesu na baada ya kufa na kufufuka kwake, Wapagani hawakuchangamana na
Wayahudi, na mbaya kazaidi Wayahudi wale ambao kwa namna ya pekee ndio walikuwa
Kanisa la Mwanzo. Hizi ni changamoto ambazo zilipelekea kuwepo kwa
Mkutano/Mtaguso huko Yerusalemu, Mdo 15:1-41. Kuchangamana kwao ni najisi kama
ilivyokuwa kula nyama za wanyama hawa au kugusa mizoga yake. Badala yake “sauti
ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Sauti
ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe
najisi,” Mdo 10: 13, 15. Neno “Ondoka uchinje ule,”
linatupa uthibitisho wa kufunguliwa neema na baraka kwa watu wote wenye hofu ya
Mungu.
Tendo hili
linathibitishwa na Petro mwenyewe huko Kaisaria kwa ujumbe uliotumwa kwake na Kornelio akida, mtu mwenye haki,
mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, Mdo 10:22.
Mtume Petro kwa kuona tendo hili kubwa likitokea hata kwa wapagani kushukiwa na
Roho Mtakatifu, anatoa hitimisho la Imani na kusema, “Hakika natambua ya kuwa
Mungu hana upendeleo; bali katika
kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35. Hivyo
kumcha Mungu na kutenda haki ndicho kibali chakukubaliwa na Mungu.
Kibali hiki ndicho kielelezo cha utakatifu wetu. Na
utakatifu huu ndio cheo chetu mbele ya Mungu licha ya utofauti rangi zetu,
familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu. Haya yote yaliyo ya
kibinadamu bila utakatifu wa Mungu katika kumcha na kutenda haki hayana fadhila
yoyote mbele za Muumba wetu.
Ndugu yangu, hakuna asiyependa mwanga kunako giza nene.
Kuyafanya mazingira yetu ya giza kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi, yatupasa
kujifunza kutoka Mshumaa. Kwa kuwaka mshumaa tunapata mwanga na giza linatoweka.
Hata hivyo, kwa tendo hilo la pekee haliuachi mshumaa katika hali yake. Kadiri
uwakavyo mshumaa ndiyo hivyo hivyo kutoweka, kujififisha, na kupungua kwa
mshumaa huo. Bila kuwa na tabia ya mshumaa jamii yetu haitaweza kupiga hatua
kutoka kwenye uovu na kwenda kwenye wema na uzuri.
Mimi na wewe, na kila mmoja wetu kadiri ya wito wake, na
nafasi yake aliyonayo katika jamii, yampasa kuwa mshumaa pale alipo. Kutumia
nguvu nyingine bila kubadilika sisi wenyewe kimtazamo na tabia, hakuna heri
mbele zaidi ya majanga.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ni vema kufa kwa mikono ya
wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye.
Lakini kwako wewe hakuna ufufuo,” 2Mak 7:14
Tusali:-Ee
Yesu Mwema na Mkombozi wetu, tujalie hofu yako ndani yetu, ili kuyatenda yote
katika upendo, kweli, na haki. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario