domingo, 6 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 32 YA MWAKA-C


JUMANNE WIKI YA 32 YA MWAKA-C

Somo: Tit 2:1-8, 11-14

Zab/kit: 37:3-4, 18, 23, 27, 29

Injili: Lk 17:7-10

Nukuu:

“Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi,” Tit 2:1-2

 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa,” Tit 2:11-12

“Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula?” Lk 17:7

 “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10

TAFAKARI:Mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.”

Wapendwa wana wa Mungu, lazima nielewe kwamba tendo lolote nilifanyalo lapaswa kuongozwa na unyenyekevu wangu. Nielewe nayafanya haya kwa sababu yanipasa kuyafanya tena kwa umakini mkubwa nikitimiza nafasi yangu kama initakavyo kufanya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Ni katika kweli hii Yesu anatuambia, Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Tutajisikia hali hii pale tu tunaposhinda kujifananisha na kujilinganisha na  yale tuyafanyayo. 

Hivyo katika kweli na haki simama katika dhamiri yako safi bila woga. Hupaswi kuwa na hofu kulisema lile libebalo uzima ndani yako na kwa wengine. Hekima aliyonayo mtu mara nyingine siyo tunda la umri wa mtu, bali ni uwezo ule alio nao mtu wa kuliona jambo kama lilivyo na siyo kama alivyo. Hapa ndipo hekima ya mtu kutoshahabiana na umri wake. Na hili likiwa ndani yako,  “nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi,” Tit 2:1-2.

Ni kweli isiyo shaka kwamba kuishi miaka mingi ni kuona mengi na kung’amua mengi katika maisha. Na katika hali na mazingira kama haya, ndipo tunaposema kwamba mang’amuzi ni mwalimu mzuri. Hapa ndipo kigezo cha umri huusishwa na hekima aliyokuwa nayo mtu. Hivyo katika jamii yoyote ile wale walio kula chumvi nyingi, yaani, wenye umri mkubwa zaidi ya wengine yawapasa kuwa mfano na darasa la maadili mema, ili jamii iijue kweli, haki, usawa, na kuishi katika upendo kama ndugu. Kwa mantiki hiyo, “vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe,” Tit 2:3-5

Hata hivyo kumjua mfugaji aliye hai na endelevu ni uwepo wa idadi ya ndama alio nao kwenye zizi. Ikiwa kuna ndama wengi na wenye afya, basi hiyo ni dalili ya mfugaji mwenye maono, malengo, na mwendelevu. Hivyo hivyo katika jamii yoyote ile uwepo wa vijana wenye maadili mema  ni uhai wa jamii hiyo na taifa hilo. Ila kuwapata vijana wenye maadili mema leo hutegemea sana shule yetu ya awali, yaani, familia. Familia zilizo hovyo ni tokeo la jamii hovyo, kuanzia viongozi hadi waongozwa. Vijana ndiyo injini-“nguvu sukuma” ya jamii husika na taifa pia. “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu,” Tit 2:6-8

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, ‘neema na baraka hufanya kazi katika uhalisia wa kitu kama asemavyo Mt Thomasi wa Aquina.’ Kumbe palipo andaliwa vyema, yaani, katika ufahamu na umaana wake, neema na baraka hiyo ya Mungu ujifunua na kufanya kazi sawasawa. “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa,” Tit 2:11-12.

Hata hivyo, kuwa na uhakika na kule tuendapo tusipopajua twahitaji kielelezo cha kutufikisha huko. Leo wewe na mimi ndani na katika Kristo Yesu, tunacho zaidi ya kielelezo cha kule tusipokujua bado ingawa kupo. Hivyo “tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema,” Tit 2:13.14. Kristo ndiyo Njia, Kweli, na Uzima, Yoh 14.6. Bila Kristo kwa Mkristo, hatuwezi kuufikia uzima huo wa milele ingawa wasiomfahamu Kristo na wasio Wakristo wataufikia uzima huo wa milele kwa dhamiri zao njema.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia,” Tit 2:11

Tusali:-Ee Yesu tujalie neema ya kutumika kwa ajili ya wengine kwa sifa na Utukufu wako, na siyo kutumikiwa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario