martes, 8 de noviembre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 32 YA MWAKA-C


ALHAMISI WIKI YA 32 YA MWAKA-C

Somo: Flm 7-20

Zab/kit: 146:7, 8-9a, 9bc-10

Injili: Lk 17:20-25

Nukuu:

lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia,” Flm 9

Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili,” Flm 10, 13

“Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” Lk 17:20b-21

Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki,” Lk 17:25

TAFAKARI: Kwa upendo sadaka, Mwana wa Adamu hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha yako na makusudi ya kuumbwa kwako na Mungu ni kuishi milele. Ufalme wa Mungu upo ndani yetu tangu kuumbwa kwetu. Mungu kwa kutuumba kwa sura na mfano wake alianzisha rasmi ufalme wake ndani yetu. Kwa hiyo ni jukumu lako na langu kuupokea kwa uhuru ufalme huu na kuwa sehemu ya maisha mapya na Mungu au kuukataa. Hivyo pamoja na kwamba ufalme huu wa Mungu umo ndani yako unayo hiari ya kuukataa pia kwa sababu Mungu haingilii uhuru wako.

Ni kwa mantiki hii hatuwezi kusema ufalme wa Mungu waja kutoka upande gani wa maisha yetu, bali yatupasa kujibiidisha kila siku kuuelewa na kuuishi. Yesu leo anatuambia, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” Lk 17:20b-21. Hii ni sehemu ya kwanza kuhusu ufalme wa Mungu, yaani ni kufanya juu chini kuutambua na kuuishi kila siku. Sehemu ya pili kuhusu ufalme wa Mungu ni yale Kristo aliyojitolea kwa ajili yako, yaani mateso na kifo cha msalaba. Hapa ndipo tulipohesabiwa haki na Mungu kwa kumtoa mwanaye Mpendwa afe kwa ajili ya dhambi zetu nasi tuwe huru na warithi wa ufalme wake. Je, unayo sadaka ya kutoa?

Wapendwa wana wa Mungu, kama wewe ni mfuasi kweli wa Kristo elewa jambo hili: ‘hakuna utukufu pasipo msalaba, na hakuna pasaka pasipo ijumaa kuu.’ Kristo alijitoa kwa ajili yetu sisi na kukubali kuiendea njia ile ya mateso kwa ajili ya kweli na haki. Naye Yesu anatuambia hayo yote yatatokea, Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki,” Lk 17:25. Nasi kama wafuasi wake Kristo tutaifuata njia itupelekayo kwenye utukufu na ufufuko tunaposimama katika kweli na haki na hapo tutaonja mauti yake.

Pale tunapoonja mateso yake pasipo shuruti ila kwa hiari yetu ndipo tutoapo sadaka upendo kwa kile tukidhamiriacho katika kweli na haki. Hali hii ya kujitoa bila kujibakiza kwa wengine na katika maana halisi ya upendo ndiko kunakotuelekeza katika upendo sadaka. Ndgu yangu, kuufahamu ukweli huu wahitaji hekima ya Mungu kuyachambua yote kwa busara, na kutenda katika kweli na haki. “Maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima,” Hek 7:28.

Ndugu yangu tunaye safiri sote pamoja katika tafakari hii, tunahitaji sana hekima ya Mungu ili tuyaone mahangiko yetu na mateso yetu kama sehemu muhimu ya wokovu wetu ambao tayari tunao ndani mwetu. “Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata pembe hii ya dunia, na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya ufaa,” Hek 8: Tuikubali hekima ili hekima hiyo itufunulie siri za Mungu.

Ni kwa ajili ya upendo sadaka Mtume Paulo haoni shaka kumtoa Onesimo kwa Filemoni kwa ajili ya vifungo vya Injili. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili,” Flm 10, 13. Naye anamwambia Filemoni, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia,” Flm 9.

Kadiri ya mapokeo, Paulo anaandika Waraka kwa Filemoni akiwa Rumi kunako mwaka 61-63 Baada ya Kristo (BK). Mtume Paulo anampasha habari Filemoni kwamba mtumwa wake Onesimo aliyemtoroka atarudi. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe,” Flm 17.

Waraka huu unafunua moyo wa Paulo na mafundisho yake juu ya utumwa, Rum 6:15. Mtume Paulo hakatazi utumwa kama ulivyokuwa zamani, bali anakazia sana kwamba Mkristo lazima amjali mtumwa/mfanyakazi wake kama ndugu katika Kristo, Kol 3.22-4.1. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari,” Flm 14. Ndani na katika Kristo Yesu sisi sote ni ndugu licha ya historia zetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” Lk 17:20b-21

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie neema na upendo wako ili tuchukuliane na kutaabikiana katika undugu wa kweli. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario