viernes, 11 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 33 YA MWAKA-C



 

Somo I: Mal 4:1-2a

Zab/Kit: 98:5-6, 7, 8-9

Somo II: 2The 3:7-12

Injili: Lk 21:5-19

Nukuu:

“Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi,” Mal 4:1

“Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake,” Mal 4:2a

Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa,” Lk 21:6 

Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8 

 Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17 

Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18

wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote,” 2The 3:8 

“Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine,” 2The 3:11

TAFAKARI:Fahari na mamlaka za kibinadamu zitapita, utawala wa Mungu utadumu hadi mwisho wa nyakati. Subirá yako itaiponya nafsi yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 33 ya mwaka “C” wa Kanisa. Masomo yetu yote matatu yanatutafakarisha mwisho wa nyakati; yaani,  yatakayo jiri, mapaswa yake, na nini cha kufanya leo na sasa. Njia iliyo salama kwa yeyote yule mwenye hofu ya Mungu ni KUJISALIMISHA. Je, wenye hofu ya Mungu wana nafasi gani kwa kujisalimisha kwao?

Hakika Mungu hataacha kamwe kuwanyeshea mvua ya neema na baraka wenye hofu Naye. Wenye hofu ya Mungu kwa kuishi kwao kuliko kwa kweli na haki, watasitawi katika haki na kweli ya Mungu. Mungu humwelekea mwenye hofu naye kwa sababu ndani yake kuna unyofu wa moyo.  Huku ndiko kusitawi mbele za Mungu kuliko haki. Hivyo, “mwenye haki atasitawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanoni,” Zab 92:12. Mungu hawezi kukaa kimya kwa wonyofu wa moyo.

Hakuna alichaye jina la Mungu, naye Mungu akaziba masikio kwa kilio chake. Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake,” Mal 4:2. Yatupasa kudumu katika sala na maombi yetu tukiwa na matumaini kwamba tumekwisha pata kile tuombacho. Na kinyume chake ni dhahiri, yaani, “siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi,” Mal 4:1. Kwa maana nyingine, wewe na mimi tusiotaka kujisalimisha kwa Mungu katika kweli na haki, tujiandae kuuvuna upepo, majanga yasiyo koma.

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya kweli kwamba maisha yetu sisi wanadamu katika ulimwengu huu ni ya muda mfupi, maisha hayo kama yalivyo ni fumbo. Mzaburi anasema, Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10. Nafikiri leo Mzaburi huyu angekuwa anaandika haya angesema vingine, miaka 40, na mwenye nguvu miaka 50. Umri wa kuishi hasa nchi za ulimwengu wa tatu ikiwemo na nchi yetu-Tanzania umeshuka sana.

Hata hivyo maisha ni fumbo kwa sababu kifo kwa kila mmoja wetu kimefichwa licha ya kwamba ipo siku na kwa wakati wake kila mmoja atafikia kikomo chake hapa duniani. Ndiyo kusema kwamba, “Fahari na mamlaka za kibinadamu zitapita, utawala wa Mungu utadumu hadi mwisho wa nyakati.” Hivyo ni vyema kila mmoja wetu akajishughulisha na mambo yale yatakayojenga uhusiano mzuri na Muumba wake, jirani yake, na mazingira yake. Uzuri wa ulimwengu huu na fahari yake vyote vitapita na kusahaulika.

Licha ya kwamba maisha ya mwanadamu hapa duniani kuwa na kikomo chake, mwanadamu huyu hawezi sahaulika na Muumba wake kwa sababu kaumbwa kwa sura na mfano wa Muumba wake, Mwa 1:26. Mungu hawezi kujisahau mwenyewe. Ni kwa maana hiyo na sababu hii, ipo siku kila mmoja ataitajika kutoa hesabu yake mbele za Mungu. Kwa chapa hii ya Mungu ndani yako, kamwe uwezi sahaulika. Jiandae kwa kutoa hesabu kwa yale uliyo kasimiwa bure, ikiwa ni pamoja na vipaji na karama ulizo nazo.

Ndugu yangu, wakati wa Yesu na hata kabla yake, wapo walio vutwa sana na ulimwengu huu na fahari yake kama ilivyo leo. Wapo waliolitazama Hekalu la Yerusalemu na kupambwa kwake wakaishia hapo tu wasione zaidi ya Hekalu hilo. Yesu anatutaka tutazame zaidi ya kile tunachokiona, yaani, tuzame zaidi ya fumbo lenyewe katika ufahamu na umaana wake. Naye Yesu aliwaambia watu wa nyakati zake, na sisi pia kwamba, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa,” Lk 21:6. Tunachotakiwa kukitazama ni uwepo wa ufalme wa kweli wa Mungu na siyo fahari na mamlaka za kibinadamu tu.  Nabii Danieli anatoa tafsiri kwa mfalme kuhusu kubomoka kwa sanamu ile iliyojengwa kwa mikono ya wanadamu licha ya uzuri iliyokuwa nayo.

Hii ni kutofautisha falme na mamlaka za wanadamu na ufalme ule wa kweli wa Mungu, ufalme ambao wadumu milele na milele. Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele,” Dan 2:44. Kile kibebacho ufahari wa kibinadamu na kisichotoka kwa Mungu hakina umilele.

Kutokana na ukweli huo nilio usema, kuna hatari ya watu kuja na tafsiri zao kuhusu mwisho wa nyakati kwa lengo hasa la kuwaogopesha watu kwa manufaa yao binafsi. Yesu Kristo anatoa angalizo na kusema, “Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8. Hawa ndio wale wajulikanao kama manabii wa uongo kadiri ya Maandiko Matakatifu. “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule,” Mt 24:24. Je, leo si jambo la kawaida mtu kujiita nabii, askofu, mtume, n.k?

Mambo haya, mfano uaskofu, ukasisi, mchungaji, mtumishi, nk, hakuna anayejitwalia, bali hutwaliwa na Mungu peke yake, ikiwa ni hitaji la Kanisa mahalia kama Mwili wa Kristo inapoonekana inafaa na mhusika anastahili kadiri ya mamlaka iliyopewa Kanisa (Mwili wa Kristo) na Kristo mwenyewe (Kichwa cha Kanisa). “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1. Hata Kristo hakujitwalia mwenyewe kuwa kuhani Mkuu. “Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa,” Ebr 5:5. Tujihadhari sana na manabii hawa wa uongo. Kila kona wapo na wanajiinua kila kukichwa!

Mwisho wa nyakati hauji upesi kama tusemavyo au kufikirivyo licha ya mwamba kabla ya mwisho huo kutatokea matokeo ya kutisha. Yesu leo anatuambia ukweli wa jambo hili, “Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9. Tunapoona mtu anapanga hadi tarehe ya matukio haya ya mwisho wa nyakati yeye kaupata wapi ukweli huo zaidi ya hiki anachotuambia Kristo? Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii usisahau maneno haya ya wahenga wetu: “Wajinga ndio waliwao.” Kristo kesho uweka sawa ukweli huu alipowajibu wanafunzi wake, Mdo 1:6, kabla ya kupaa mbinguni, kwamba, “si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyeyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kilichopo mbele yetu leo na sasa ni kuihubiri habari njema hadi mwisho huo wa nyakati, Mdo 1:8. Na katika kweli hii, tusichoke wala kukata tamaa katika kutenda mema, 2The 3:13

Leo Yesu anawaambia wafuasi wake nasi pia maneno haya mazito, ‘subirá yako itaiponya nafsi yako.’ Mwenye subira ufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Mwenye subira huyatazama yote katika jana yake, leo yake, kesho yake, na umilele wake. Kuwa mfuasi hai wa Kristo kuna mapaswa yake. Yesu anatuambia leo mapaswa ya kuwa mfuasi wake hai. Mapaswa yake ni kusalitiwa. “Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17.

Badala yake, na katika hali hii ya kusalitiwa, Yesu anatuambia tuwe na furaha. “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Yatupasa kufurahi kwa sababu katika mateso na ugumu huu wa kusimama katika kweli na haki, “hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18. Hakuna aliye wa bahati mbaya katika ulimwengu huu “kwa maana kama tunaishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8

Mpendwa katika Kristo, elewa kwa hakika kabisa kama kweli wewe ni mfuasi hai wa Kristo, ipo siku ufuasi wako utapimwa. Na hilo kama litatokea jiachie-jisalimishe kwake Kristo Yesu. “Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga,” Lk 21:14-15. Kumbe kwa kujiachia-kujisalimisha kwake Kristo ni kwa namna hiyo hiyo tayari tunaye mtetezi.

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli pasipo shaka kwamba, ‘palipo na utaratibu kuna akili.’  Ipo mifano mingi yenye kuthibitisha ukweli huu wa uhusiano kati ya utaratibu na akili. Mfano halisi ni uumbaji wa ulimwengu huu tunaoishi. Hata kama wengi wetu kwa sababu zao hawaamini uwepo wa Mungu aliye hai, hatuwezi kupinga kwamba mpangilio mzima wa ulimwengu huu tunaoishi haukuhusisha akili. Hivyo palipo na utaratibu kuna akili. Ikiwa wewe na mimi tupo kwenye mpango huo na utaratibu huo, maisha yetu yanatutaka tuenende katika utaratibu. Kila mmoja wetu yupo hapa ulimwenguni kwa lengo. Huu ndio wito wa Mtume Paulo kwetu leo, kwamba tuenende kwa utaratibu. Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu,” 2The 3:6. Pasipo utaratibu ni fujo. Na hukumu ya mwisho yategemea ishi yako na yangu leo katika utaratibu.

Wanapoishi watu zaidi ya mmoja, lazima kuwe na utaratibu, na utaratibu huu kuheshimiwa baina ya hao walioweka huo utaratibu, kwa mafaa yao, na sifa kwa Muumba wao. Ni jambo la kusikitisha sana tunapoona kwa wazi kabisa waliopewa dhamana ya kuulinda na kuutetea utaratibu, Katiba, ndiyo vinara wa kuivunja Katibu hiyo kwa wao kujihalalishia jeuri na ubatili wao. Huku ni kuusaliti umma wa watu, ambayo ni sauti ya Mungu, na mwisho kuwa kikwazo kikubwa kwa UMMA na MUNGU MWENYEWE. Mtume Paulo anashinda kishawishi hiki na kusema pasipo shaka kwamba,  Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu,” 2The 3:7.

Mtume Paulo hakuishia hapo tu, yaani, kutokuvunja utaratibu, bali alikuwa mstari wa mbele yeye na wenzake katika kutimiza wajibu wao. Na hivi ndivyo anavyotoa ushuhuda wa maisha yake na wenzake ya kila siku, na kusema, wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote,” 2The 3:8. Huu ni mfano mzuri sana wa kuigwa na kupongezwa kwa kiongozi yeyote yule mwenye dhamana, na aliyepewa dhamana hiyo na Mungu kupitia sauti ya watu. Maisha katika ujumla wake ni DHAMANA. Je, ugonjwa wetu kama Taifa ni upi?

Wapendwa wana wa Mungu, saratani angamizi ya Taifa hili letu la Tanzania ni UNAFIKI na UBABAISHAJI katika kufikiri, kuamua, na kutenda. Tusitegemee maajabu hata kama tukimpata Rais Malaika, kama hatutabadili mfumo huu wa maisha-Unafiki na Ubabaishaji. Tatizo ni kwamba palipo na unafiki na ubabaishaji ni vigumu kutofautisha aliye soma na aliye elimika. Palipo na unafiki na ubabaishaji, uhalisia wa jambo hauwi kama ulivyo, bali kama tulivyo. Katika jambo hili, Mtume Paulo anatupa angalizo na kusema, “twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine,” 2The 3:11. Huu ni utumiaji mbaya wa rasilimali muda, na malighafi tuliyo kirimiwa bure na Mungu.

Badala yake, tunatumia muda mwingi kutetea na kuufunika uovu. Wahenga katika hili wanasema, “mficha uchi hazai, na mficha kidonda ndugu harufu umuumbua.” Kukiri udhaifu siyo kushindwa bali ni mwisho wa mwanzo mpya wa kule utakako kufika. Ukweli wa jambo uwezwa kufunikwa kwa wakati tu, bali kadiri ya muda uendavyo kweli hiyo ujifunua yenyewe. Kweli ni asili ya Mungu, nayo  ni milele katika maana yake kama alivyo Mungu. Kwa misuli yetu na ubinadamu wetu hatutoweza kamwe kuifunika kweli katika umilele wake. Badala yake, na kama tutafanya hivyo, basi tujiandae kuanikwa na kuumbuliwa wakati utakapo fika. Mtume Paulo analo jambo kwetu leo kama asemavyo, “Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe,” 2The 3:12. Kuwa kile ulicho, na fanya yote katika ukamilifu wake kadiri ya; wito wako, uwezo wako, hali yako, na nafasi yako katika jamii.

Ndugu yangu, bila shaka wamfahamu vizuri Nyani. Pamoja na weledi wake nyani katika harakati zake za kila siku, na kukweya kila aina ya miti kwa kujifurahisha na hata kujihifadhi, kamwe hafanyi kosa katika jambo hili; “usiku awapo juu ya mti ujisaidia kwenye kiganja chake na kupaka kinyesi chake kwenye mti.”

Nyani hufanya hivi siyo kwa kupenda, bali kwa usalama wake mwenyewe. Mmoja ya wanyama hatarishi kwa nyani ni chui. Hivyo nyani kukiacha kinyesi chake kudondoka chini ni kumpa taarifa chui kwamba juu ya mti tena usiku kuna kitoweo, yaani, nyani. Na nyakati za usiku nyani hana werevu wa kubembea kwenye matawi ya mti kwa jeuri na majivuno. Kinyume chake, usiku kwa chui ndiyo muda muafaka kwa mawindo.

Ndugu yangu, ujumbe wa simulizi hili  ni kwamba, fanya yote kadiri ya uwezo na maarifa yako, ila usisahau ukomo wako. Mungu kwa kukuumba wewe na mimi kwa sura na mfano wake, na ndiyo tulivyo wanadamu, alijua na anajua wazi kabisa kwamba kwa kuishi kama wanadamu ndipo ulipo ushindi wetu, yaani, utakatifu wetu.

Kumbuka: Malaika walipo muasi Mungu walibadilika kuwa mashetani. Nasi tunapoukataa ubinadamu wetu katika ukomo wake, na kutaka kuwa sawa na Mungu, tunabadilika na kuwa wabaya kuliko masheni kwa sababu tamanio hili hata malaika walilita na mwisho wakawa mashetani.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine,” 2The 3:11

Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ya kuishi katika utaratibu ili uonekane kwa kila mmoja wetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario