JUMAMOSI WIKI YA 32 YA MWAKA-C
Somo:
3Yoh 5-8
Zab/kit: 112:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Lk 18:1-8
Nukuu:
“Kwa
maana, kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa,” 3Yoh 7
“Basi imetupasa sisi
kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli,” 3Yoh 8
“Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane,
aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu,” Lk 18:3
“Naye
kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali
watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije
akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4-5
“Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Lk 18:8
TAFAKARI:
“Kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa. Hivyo yatupasa kumwomba Mungu sikuzote, wala tusikate tamaa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Kadhi kama tulivyosoma na kusikia Injili ya leo anampa mama mjane haki yake si
kwa kupenda bali kwa kulazimika kutokana na usumbufu. Naye anasema, “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi,
nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4b-5. Hivyo
unaweza kutoa bila kupenda.
Tunapokuwa
na mahusiano mazuri na Mungu kamwe hawezi kutuacha katika mahangaiko yetu. Bwana
wetu Yesu Kristo anatupatia uhakikisho huyo. “Na
Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni
mvumilivu kwao?” Lk 18:7. Uvumilivu wa Mungu
kwetu ni Imani ile tuliyo nayo juu yake. Kwa imani dhabiti tunauhakika kwa
kuyapata yale tumwombayo Mungu wetu aliye huruma na upendo.
Yesu anatupa pia
uhakika wa jambo hili, ila imani ni moja ya kielelezo kikuu kwa kile tuombacho.
Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja
Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
Lk 18:8. Je, unayoimani kwa hayo uyaombayo?
Kwa upande mwingine huwezi kupenda bila kutoa.
Yesu anasema, “Mimi ndimi mchungaji
mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:11. Yesu
kwa kutupenda yupo tayari kutoa uhai wake kwa anjili yetu. Upendo ndiyo amri
yenyewe. Kristo ndiye kielelezo chetu juu ya upendo na kupenda. Hili ndilo lile
neno lililofanyika mwili nalo likakaa kwetu, Yoh 1:14. Kwa kupitia Kristo tunalo
hakikisho la wokovu, na kwa jina lake kila tuombalo kwa imani tutapewa kwa
wakati wake. Ni kwa matiki hiyo kwamba, “hakuna wokovu katika mwingine awaye
yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu
litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Kristo ndiye JIBU.
Hivyo ndugu yangu
tunaye safiri sote katika tafakari hii, wewe kama ni Mbatizwa na unaishi ahadi
zako za ubatizo kwa uaminifu, una wajibu mkubwa sana wa kufanya katika Kanisa
la Kristo. Na kubwa kuliko yote ni kufanana na Kristo katika kufikiri, kuamua,
na kutenda. Haya yote matatu yalidhihirisha upendo kamili wa Kristo ambaye
ndiye maana halisi ya ufunuo na upendo wa Mungu kwetu. Kama Wakristo na wenye
hofu ya Mungu, sote tu vyombo vya amani, upendo, haki, na huruma ya Mungu pale
tulipo. Na lengo ni kuwasafirisha wote-wana wa Mungu, kwake Yeye aliye waumba
kwa sura na mfano wake.
Hivyo “Mpenzi, kazi ile
ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, waliokushuhudia upendo
wako mbele ya Kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu,”
3Yoh 5-6. Kupotezana njiani tena kwa agenda binafsi ni chukizo kubwa sana kwa
Mungu ilhali twajiita Wakristo, Walei, Watawa, na Makreli. “Kwa maana, kwa
ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa,” 3Yoh 7. Mimi na wewe
ni watimiza wajibu wetu kwa uaminifu, ila awaitaye kwake ni Yule aliye waumba
kwa sura na mfano wake. Mimi na wewe tusaidiane kuifikia taji na mede ile
tuliyoandaliwa. Hali na mazingira hayo ya kusaidiana yanahitaji roho ile ya
kutaabikiana. Twahiji fadhila ya unyenyekevu na burasa ili kufikia lengo lile
la kufanana kama Kristo. Tusichoke kuomba neema ya Mungu, na fadhila hizo.
Mkristo na mwenye hofu
ya Mungu siye mfunga mlango na mzuiya neema na baraka za Mungu kwa wateule
wake. Kinyume chake Mkristo ni mtumika wa Mungu katika kweli na haki, na mwisho
wa siku ni mtumishi asiye na faida, na aliye utimiza wajibu wake katika upendo,
kweli, na haki ya Mungu, Lk 17:10. “Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama
hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli,” 3Yoh 8. Na palipo na upendo Mungu
hujidhihirisha katika maisha ya watu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nawaambia,
atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani
duniani?” Lk 18:8
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
ustahimilivu katika sala. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario