miércoles, 9 de noviembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 32 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 32 YA MWAKA-C

Somo: 2Yoh 4-9

Zab/kit: 119:1, 2, 10, 11, 17, 18

Injili: Lk 17:26-37

Nukuu:

“Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo,” 2Yoh 6

 “Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu,” 2Yoh 8

“Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2Yoh 9

 Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma,” Lk 17:31 

Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya,” Lk 17:33 

 Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai,” Lk 17:37b

TAFAKARI:Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.”

Wapendwa wana wa Mungu, kifo wakati mwingine uonekana kipo mbali sana hasa pale tunapozama katika anasa na malimwengu. Wakati wa Nuhu na hata Lutu habari za Mungu na uwepo wake hazikuonekana kama kitu cha pekee kwa wengi hasa wale walioishi katika mfumo wa “ponda mali.” Ila hata kama hatuna hisia na Mungu, Yeye hupo hai na anayaona yote tuyafanyayo. Siku ya kuzungumza na kila mmoja wetu kwa wakati wake inakuja. Hivyo, Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu,” Lk 17:26. Itakapofika siku hiyo tutapigwa na mshangao kwa vile hatutakuwa tumejiandaa vyakutosha kwa sababu tu ya kupuuzia kama walivyompuuzia Nuhu kuitengeneza Safina ilhali hapakuwa na dalili yoyote ya mvua, mto, ziwa wala baharí, ila Mungu aliinyeeshea duania kutoka chini.

Mshango mwingine ni kwamba tukio hili la kifo litamkuta kila mtu pale alipo kwa mshangao. Ni mara ngapi tunaondokewa na wapendwa wetu ilhali hatukuwa kumeagana vizuri au kuongea nao kwa urefu? Mara nyingi tunabakiwa na ‘ninge…’ zisizo na idadi. “Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma,” Lk 17:31. Hapa ni pale tunaposema, “lo! Nilikuwa naye leo asubuhi na sana hatunaye tena!” Hata tukio kama hilo halisemi chochote kuhusu maandalizi yako?

Yesu anatupatia jibu la mkwamo huu, na kutuweka mkono salama tusijepigwa na mshangao. Naye anasema, “Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya,” Lk 17:33. Kuiponya nafsi katika kuingamiza ni kuiridhia nafsi kwa yale inayoyataka. Ni pale nafsi inapoegemea katika mwili na kufanya matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,  ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Huku ni kuiponya nafsi katika kuiangamiza.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kuiangamiza nafsi katika kuiponya ni pale nafsi yako inapoegemea roho, na kutenda matendo ya roho yenye tunda la roho. “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23. Huku ni kuiangamiza nafsi yako katika kuiponya. Je, mzoga wako utakuwa wapi?

Baada ya mafundisho haya mazito ya Injili ya leo, watu walitaka kujua hayo yatatendeka wapi? Yesu anatujibu hivi, “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai,” Lk 17:37b. Kwa maana nyingine mwisho wako utategemea ishi yako. Hivyo kama nafsi yako katika ishi yako itaegemea mwili, ndivyo hivyo mwisho wako utakuwa katika matendo ya mwili. Tuna ambiwa watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Vile vile kama nafsi yako itaegemea roho yako, basi mwisho wako utakuwa tunda la roho. Tunaambiwa juu ya mambo kama hayo hakuna sheria, kwani kwa kuishi hivyo ndiyo sheria yenyewe aipendayo Mungu. Ni maisha ya kweli na haki.

Palipo na upendo wa kweli, tokeo lake ni tunda la roho. Na twaudhihirisha upendo kwa kuzishika amri za Mungu, “Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo,” 2Yoh 6. Uwepo wako na wangi leo ni tokea la upendo wangu aliyeona na kumpendeza kutuumba kwa sura na mfano wake. Nasi ni furaha na utukufu wake Mungu. Mungu kalifanya tendo hili la upendo siyo kwa sababu ya hitaji, bali kwa uhuru wake na kupenda kwake.

Ni kwa upendo wake huu Mungu,  “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, 5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Hivyo  ndugu yangu, baada ya Mungu kukuumba kwa sura na mfano wake hakukuacha ujiendee mwenyewe kama saa ya mshale. Lengo na furaha yake Mungu ni mimi na wewe tuishi milele. Na hili ndilo kusudi la NENO wa Mungu, yaani, Yesu Kristo, kufanyika mwili-kumwilishwa, na kukaa kwetu. Ndugu yangu, kuwa macho kwa sababu, pamoja na ukweli huu, wapo “wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo,” 2Yoh 7. Hata kati yetu na hapo ulipo wampinga Kristo wapo. Kuwa macho!

Pamoja na mpango huu mzuri wa Mungu kwa kila mmoja wetu, ‘Mungu huyu aliyekuumba wewe pasipo wewe hatoweza kukusaidia/kukuokoa wewe pasipo wewe,’ kama asemavyo Mtakatifu Augustino wa Hippo. Hivyo Mtume Yohana anatuambi sote kwamba, “Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu,” 2Yoh 8. Lengo la maisha yetu hapa duniani mwisho wa siku tuwe wakamilifu kama Baba yetu wa Mbingu alivyo makamilifu, Mt 4:48. Bila ukamilifu/Utakatifu hatutaweza kumwona wala kukutana na Mungu aliye Mkamilifu na Mtakatifu.

 Hivyo ndugu yangu, uwapo hapa duniani licha ya mbwembwe zako zote, majivuno yangu, kiburi, na jeuri ya hela na madaraka uliyo nayo, ukomo wake ni mfupi sana. Ukweli ni kwamba, “Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2Yoh 9. Je, bila Kristo nawe wajiita Mkristo, utatoboa, yaani, kuufikia ufalme huo wa Mbinguni?

Tumsifu Yesu Kristo!

Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya,” Lk 17:33

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, tukumbushe mara zote ufupi wa maisha yetu hapa duniani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario