JUMATANO WIKI YA 33 YA MWAKA-C
Somo:
Ufu 4:1-11
Zab/kit: 151:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Lk 19:11-28
Nukuu:
“Na
mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja
ameketi juu ya kile kiti,” Ufu 4:3
“Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile
kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi,
wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu,” Ufu
4:4
“Na huyo mwenye uhai wa
kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama;
na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa
nne alikuwa mfano wa tai arukaye,” Ufu 4:7
“Akamwambia,
Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe
na mamlaka juu ya miji kumi,” Lk 19:17
“Nawaambia,
Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho
nacho,” Lk 19:26
TAFAKARI:
“Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye
na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kila mmoja wetu kapewa uwezo wa kupambana na
mazingira yoyote yale atakayokutana nayo. Uwezo huu siyo wa kuufungia sehemu
fulani na kutokufanya chochote. Na kadiri tutumiavyo uwezo na maarifa hayo
ndivyo Mungu anavyozidi kutukirimia kadiri ya hitaji letu na wenzetu. Na ikiwa
maisha yetu hapa duniani ni jukumu la muda mfupi, safari yetu kuelekea uzima wa
milele ni pamoja na kutumia vyema karama na vipaji aliyotujalia Mungu kama
sehemu ya maandalizi hayo.
Injili
ya leo inafafanua jambo hili kwa mifano ya watu waliopewa fedha za biashara na
mtu mmoja Kabaila. Aliyepewa kumi alizalisha nyingine kumi, aliyepewa tano
alizalisha nyingine tano, na aliyepewa moja hakufanya chochote zaidi ya
kulalamika. Naye alipotakiwa kutoa hesabu yake alijibu kwa jeuri, “Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa
usichoweka, wavuna usichopanda,” Lk
19:21. Mara nyingi huwa tunajihukumu wenyewe kwa kutokuviendeleza vipaji
alivyotupa Mungu na kubaki kutamani vipaji vya wengine. Wapo pia wengine kati
yetu ambao muda wao wote katika maisha ni kuyatafuta yale ambayo yapo nje ya
uwezo wao, na mwisho wa siku wanabaki kuwa vivuli vya wengine na kukosa furaha
ya kweli ndani yao.
Kumbe leo Kristo anatuambia tuthamini aliyotupatia
Mungu, na tuyaendeleze kwa sababu, “Kila aliye na kitu atapewa, bali
yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26.
Usipo kithamini ulicho nacho na kukiendeleza kitachukuliwa na kupewa mwingine.
Kwa maneno mengine, wewe mwenyewe wakati mwingine ni sababu tosha ya kuyadumaza
yale aliyokujalia Mungu kwa kutojishughulisha. Hatua ya kwanza ya kuthamini
kile ulichonacho huanza kwa wewe mwenyewe kuwa mwaminifu kwa yale madogo madogo
ya kila siku na hasa kwa yale tunayopewa dhamana. Watumwa wale waliofanya
vizuri walipewa hakikisho la utendaji wao. “Akamwambia, Vema, mtumwa mwema;
kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya
miji kumi,” Lk 19:17. Je, wajua vipaji vyako na uwezo wako?
Tunzo ya kuvitumia vipaji na karama
zetu vyema, kwa ajili yetu na wengine, ni ezekano lile la kuhesabiwa haki na
kuurithi ufalme wa mbinguni. Hivyo somo letu
la kwanza leo linaelezea manndari hiyo ya Mbinguni. Kwanza huko mbinguni uishi
Mungu aliye Mtakatifu na ndiyo makazi yake ya milele. Yohana katika maono yake
anatuambia kile alichokiona: “Na mara nalikuwa katika Roho; na
tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti,”
Ufu 4:3. Kiti hiki cha Mungu ni ishara wazi ya ukamilifu wake. Na ishara hii ya
ukamilifu imejifunua kwa uwepo wa taa saba za moto zikiwaka. “Na katika kile
kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto
zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu,” Ufu 4:5.
Mungu wetu ni hai, tena ni mwanzo na mwisho-ALFA NA OMEGA.
Kundi la pili ni
wateule wake Mungu, yaani, watakatifu. Nao hawa wanawakilishwa kwa viti vile
ishirini na vinne. Idadi hii ya vitu yamaanisha idadi ya kutosha, na iliyo
kamili. Hawa wateule wa
Mungu ukizunguka kiti kile cha enzi cha Mungu. “Na viti ishirini na vinne
vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na
wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji
za dhahabu,” Ufu 4:4. Mavazi yao maupe ni alama uthibitisho tosha wa utakaso na
Utakatifu wao.
Wateule
hawa wa Mungu wanayo kazi moja tu huko mbinguni. Kazi hiyo ni kumsujudu yule
aliye hai hata milele na milele. Na “ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka
mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye
hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi,
wakisema,” Ufu 4:10. Kusujudu huku ndiko kujisalimisha pasipo kujibakiza, na
ndiyo maana halisi ya kuabudu. Ni kuunganishwa na furaha ile ya Mungu na
utukufu wake milele yote. “Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti
cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na
milele,” Ufu 4:9
Kundi lingine la tatu
huko mbingini ni kundi la Malaika wa Mungu. Hawa ndio wale walindao malango
yale pande zote nne za Utukufu huo huko mbinguni. Malaika hawa hujulikana kwa
kazi na muono wao kama anavyosimulia Yohana. “Na huyo mwenye uhai wa kwanza
alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na
mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne
alikuwa mfano wa tai arukaye,” Ufu 4:7.
Nao hawa Malaika kazi yao kubwa licha ya ulizi,
humzunguka Mungu na kuimba ‘Mtakatifu’ pasipo ukomo. “Na hawa wenye uhai wanne,
kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala
hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana
Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja,” Ufu 4:8. Je,
kuna kwaya gani na yenye uwezo hapa duniani kama hii ya kundi hili la malaika?
Leo tuolio na vipaji vya kuimba wakati mwingine twa jaa kiburi kwa vile bado
hatujajua ni nani tunayemwimbia.
Hakika, sifa na
shukrani ni kwa Mungu tu. Na zoezi hilo la kumpa Mungu sifa na shukrani
linaanza hapa hapa duniani kwa kutoa kile ulicho nacho kwa moyo mkunyufu na
usio jibakiza. Hivi ndivyo vile vipaji ulivyo jaliwa na Mungu kwa ajili yako na
wengine. Hizi ndizo karama zile Mungu alizokujalia bila mastahili yako. Na huu
ndio ule utajiri aliokuazimisha Mungu kwa wakati tu ungali hapa duniani. Na
unafanya yote hayo kwa sifa na Ufalme wake Mungu ukijua wazi anayestahili hayo
yote ni Mungu peke yake kwa kuwajali jirani zetu, na wale wote wenye uhitaji.
Hakika, “umestahili
wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa
wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako,
navyo vikaumbwa,” Ufu 4:11. Ni Mungu peke yake apaswa kuabudiwa na kutukuzwa
milele. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na hao wenye uhai wanapompa yeye
aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai
hata milele na milele,” Ufu 4:9
Tusali:-Ee
Mungu, tujalie neema na nguvu tukusifu milele yote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario