JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO YA MWAKA-A
Somo: Isa 4:2-6
Zab: 122: 1-2, 3-4b, 4cd-5, 6-7, 8-9
Injili: Mt 8:5-11
Nukuu:
“Na
mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani
kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika
mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika
Yerusalemu,” Isa 4:3
“Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende
katika nuru ya Bwana,” Isa 4:5
“Yesu
akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7
“Yesu
aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni,
Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10
TAFAKARI: “Twende katika nuru ya Bwana.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Mwokozi tunayemtazamia kwa hamu ni Bwana wa Amani
atakayetufundisha njia zake na kuenenda katika NURU yake. Sheria yake kuu ni
UPENDO. Ni wakati wa kuyajenga upya mahusiano yetu na Bwana huyu wa Amani. Ni
Bwana wa Amani wa wataifa yote, na ulimwengu mzima. Ni Bwana aliye katika
kilele cha vilele vyote ambacho uthibitisha ukuu wake. Nabii Isaya anasema
habari za Mkombozi huyu: “Na itakuwa katika siku
za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao
utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi,” Isa 4:2
Haki ndicho kipimo na
uwepo wa Amani ya Mkombozi huyu tunayemtazamia. Hivyo ajapo lazima ipite hukumu
ya haki, na ndipo atakapousimika utawala wake wa Amani, Haki, na Upendo. Ili
mambo haya yatendeke katika utawala wake yatupasa kubadili namna yetu ya
kufikiri na kutenda. Na ndipo “mataifa
mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa
Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito
yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,”
Isa 4:3
Ulimwengu wa leo vita
na hasa ugaidi vinashamiri kwa nguvu kubwa sana na uhai wa mwanadamu ikiwa ni
pamoja na amani vipo reheni. Nabii Isaya anasema, “Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu
wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu;
taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena
kamwe,” Isa 4:4
Tunahitaji sana kwa sasa utawala wa Mkombozi
huyu. Lengo la Mungu kuumba ulimwengu pamoja na mambo mengine, aliuumba ili
pawe sehemu salama kwa ajili ya uhai wa viumbe vyote alivyoviumba na kwa namna
ya pekee Mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.
Kujenga mahusiano mapya
na Mungu ni pamoja na kuwa na imani thabiti naye. Uthabiti wa imani ya kweli
hujengwa kwa kuyaacha mambo yako ya giza na kuikumbatia nuru. Wana wa Israeli
waliiacha nuru na kulikumbatia giza. Mungu aliwaacha. “Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa
sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na
wanapana mikono na wana wa wageni,” Isa 4:6
Leo katika Injili Yesu anakutana na mtu
mmoja, Akida, aliyekuwa anauguliwa na mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Akida
huyu anamwomba Yesu aende kumponya mgonjwa wake. Yesu anamjibu, “Nitakuja,
nimponye,” Mt 8:7. Akida huyu akitambua uwezo wake na nafasi aliyokuwa nayo, na
ule uwezo wa Yesu, bado anatambua kuwa umbali na uwepo wa Yesu aviwezi kumzuia
kumponya mtumishi wake. Akida anamtaka Yesu aseme neno tu na mgonjwa wake
atapona.
Hii ndiyo imani thabiti
na isiyokuwa na shaka. “Yesu aliposikia
hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona
imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, waamini kuwa Yesu aweza kutenda maajabu ndani
yako? Jenga uhusiano mpya naye kuanzia sasa! Yesu ni Rafiki wa kweli.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kama mngekuwa
na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe
baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6
Tusali: Ee Yesu Mwema,
jenga tena uhusiano wangu nawe. Nijalie neema na nguvu nisikusaliti. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario