lunes, 14 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 33 YA MWAKA-C


JUMANNE WIKI YA 33 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 3:1-6, 14-22

Zab/kit: 15:2-3ab, 3bc-4ab, 5

Injili: Lk 19:1-10

Nukuu:

“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa,” Ufu 3:1ac

“Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako,” Ufu 3:3

 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; 15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto,” Ufu 3:14a,15

“Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu,” Ufu 3:16

 Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” Lk 19:5

 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9 

Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea,” Lk 19:10

TAFAKARI: Tazama, nasimama mlangoni, nabisha hodi.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo tunaona upendo mkubwa na wa ajabu wa Mungu  katika kutano lile kati ya Yesu na Zakayo. Zakayo hamwoneyi Yesu aibu pamoja na watu kuyajua madhaifu yake ikiwa ni pamoja na ufupi aliokuwa nao. Bado anaona salama yake ipo kwa Kristo tu na siyo mitazama ya wale walikuwa wanamzunguka. Ili amwone Yesu, Zakayo alipanda juu ya mkuyu. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” Lk 19:5.

Ni wazi kwamba huwezi kuwa mrefu zaidi ya wewe mwenyewe. Na kwa kuwa huu ni ukweli wa lazima, kumbe kuvijua na kuviona vile vilivyo nje ya uwezo na kimo chako yakupasa kufanya juhudi ili kuujua ukweli ule ulio nje vya vimo vyako. Hivyo Zakayo anatufundisha kwamba hata kama ulimwengu ushatuhukumu, na hali na mazingira yetu yanatukwamisha, bado tunaweza kukutana na upendo na huruma ya Mungu tufanyapo bidii. Mtakatifu Agustino wa Hippo katika kweli hii anasema, “aliyekuumba wewe pasipo wewe, hataweza kukusaidia wewe pasipo wewe.” Hizo Zakayo kwa juhudi zake, na mpango mahususi wa Mungu, anafanikisha ndoto yake, na Yesu anakuwa mgeni wake.

Tendo hili la Yesu linawashangaza wengi na wengine wananung’unika. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi,” Lk 19:7. Hapa tunakumbushwa pia moja ya kazi ya Yesu Kristo katika safari na historia hii ya wokovu kama asemavyo yeye mwenyewe kwamba, “sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu,” Lk 5:32.

Kwa utayari wa Yesu kwenda nyumbani kwa Zakayo, kwa furaha aliyokuwa nayo Zakayo hakuweza kuificha. Hivyo Zakayo anayaweka yote wazi mbele ya Yesu.  Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne,” Lk 19:8. Hii ni toba ya kweli na maungamo ya wazi mbele ya Yesu aliye sasa njia, kweli na uzima.

Maungamo haya ya kweli toka moyoni mwa Zakayo yanaifunua furaha na upendo wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo na kuonyesha kile hasa Yesu alichokijia ulimwenguni. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9. Wokovu ni kwa kila mmoja na hasa pale tunapouridhia wokovu huo kwa utashi wetu wenyewe na kwa dhamiri iliyo hai na safi. 

Mungu anatazama utayari wako katika upya wa kuyaanza yote nawe na siyo historia ya maisha yako mabaya yaliyopita. Tu wapya mbele ya Mungu siku na muda wowote. Ni wewe na mimi tu kujisalimisha mbele ya uso wake wau pendo, huruma, na Mtakatifu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea,” Lk 19:10. Ndugu yangu, afadhali kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa unajisi.

Wakati ndiyo sasa kusimama katika kweli na haki, na kuchukia uovu wa aina yoyote ile kwenye maisha yako na jamii inayotuzunguka. Hivyo kwako na kwangu ni mwito tunaopatiwa leo kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake pale alipo. Kwa yeyote aliyepewa dhamana na umma kwake vitahitajika vingi pia. Naye Yesu anasema, “Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48b

Somo letu la kwanza limebeba ujumbe huo huo wa kubadilika na kuanza maisha mapya na Mungu. Ni wazi kuwa Makanisa yale saba anayoyazungumzia Yohana yalighubikwa na dhuluma na taabu nyingi kwa wampingao Kristo. Hata hivyo, kwa upande wa wanakanisa, nao iliwapasa kuenenda katika uchaji na hofu ya Mungu. Na salama yao ipo katika toba ya kweli na majuto. Na huu ndio ujumbe wa Yohana kwa Kanisa la Sardi,  “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa,” Ufu 3:1ac. Ni kweli kabisa kama waonekanavyo kuwa hai kumbe ni wafu, nasi tunapo dondoka katika hali ya dhambi twaikumbatia mauti na mwisho wa siku tunakosa uzima ndani yetu.

Wito kwa kila mmoja wetu ni kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi. Ni kuyashika kwa uaminifu mafundisha ya Kristo Yesu na kuyaishi. “Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako,” Ufu 3:3. Kwa vile hakuna ajuaye kwa uhakika siku yake ya mwisho, kumbe ni vyema kuwa tayari kila siku katika hali ya neema. Na kuwa katika hali ya neema ni kujitahidi kila siku kutokuwa katika hatia ya mwili, nafsi, na roho yako. Sakramenti ya kitubia/upatanisho utusafisha na kuturejesha katika hali ya neema.

Kwa kuwatia moyo, Yohana anatambua vile vile wale wachache walioweza kuishi bila hatia katika hali ya uchaji na kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa Kanisa hili la Sardi. “Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili,” Ufu 3:4. Hawa ndio watakatifu wa Mungu. Hawa ndio mfano wa kuigwa. Utakatifu wawezekana kwa kila mmoja wetu. Ni utayari wako tu wa kuiacha njia ile mbaya na kumfuata Kristo kwa uaminifu.

Ndugu yangu, maisha ni jaribu na kila siku iendayo kwa Mungu twapaswa kulishinda jaribu hilo. Majaribu mengine kwa nguvu zetu hatuweza kushinda kwa wepesi. Katika hali na mazingira hayo twahitaji nguvu na msaada wa Mungu. Na watakatifu ni wale waliokuwa na uhusiano wa karibu na Mungu, na hawakuwa na mashaka na uweza wake Mungu. Hivyo, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake,” Ufu 3:5. Mungu awezaye yote, huifanya njia pasipo njia, kwa sababu majaribu hayo hayawezi kupita uwezo wa Mungu, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu, IKor 10:13.

Tatizo kubwa la wanakanisa wa Laodika ni kwamba hawakuwa imara katika Imani, na mwisho wa siku walikosa msimamo kabisa kwa kile walichokiamini. Yohana anawapa karipio na wasio huu; “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto,” Ufu 3:14a, 15. Kuwa vuguvugu katika imani ni hatari sana. Heri kuwa baridi au moto katika imani.

Mungu atakutapika, yaani, kutoshughulika nawe kwa sababu umekosa msimamo katika imani ya kweli. “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu,” Ufu 3:16. Leo kati yetu, tu vinara wa kuhama hama kutoka nyumba moja ya sala na kwenda nyingine. Tunachotafuta usiku na mchana ni ishara na miujiza. Hivi sivyo vielelezo vya ukomavu wa imani, bali huwasaidia wale tu walio na imani changa.

Usalama wa wanakanisa hawa wa Laodika ni kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi zao. Na huu ndio ushauri wa Yohana; “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona,” Ufu 3:18. Kuinunua dhahabu ni ule utayari wa kumrudia Mungu ulio wa thamani,  toba ya kweli na majuto. Mungu aliye Upendo na Huruma, yu tayari kumsamehe yeyote mwenye kutubu na kuiacha njia yake mbaya na kumfuata. Naye anasema, “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu,” Ufu 3:19.

Ndugu yangu, subira ya Mungu kwako na kwangu ni kubwa sana. Mungu wetu ni mvumilivu sana na mwenye kutungoja tumrudie kwa uhuru wetu. Mungu kamwe hatumii shuruti kutulazimisha jambo. Mungu anathamini sana uhuru wako. Naye anasema, “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami,” Ufu 3:20. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu na wa ajabu.

Upendo huu wa Mungu ulio wa ajabu, kwetu ni jaribu kubwa sana katika matumizi sahihi ya uhuru aliotupatia Mungu kwa upendo wake. Tunapomrudia Mungu yeye anatuhaidia jambo hili; “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi,” Ufu 3:21. Ni furaha kubwa iliyoje kuketi pamoja na Mungu katika kiti chake cha enzi! Kila mmoja wetu anayo nafasi hiyo. Ni utayari wako tu kuiacha njia yako mbaya na kumfuata katika kweli, haki, na uaminifu.

Tusifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea,” Lk 19:10

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nipo hapa usinipite Bwana. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario