lunes, 31 de octubre de 2016

TAFAKARI: WAAMINI WOTE MAREHEMU


WAAMINI WOTE MAREHEMU

Somo I: Hek 3:1-9

Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6

Somo II: Rum 5:5-11

Injili: Yoh 6:37-42

Nukuu:

“Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1

“Na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek 3:2b-3

 Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6 

Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8

 Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,” Yoh 6:37 

Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39 

Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:40

TAFAKARI: “Roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa pote duani anaadhimisha Misa Takatifu kwa heshima ya Waamini Marehemu Wote waliotutangulia katika haki. Kanisa la wana wa Mungu limegawanyika katika makundi makuu matatu. Katika mgawanyiko huo lipo Kanisa la hija, yaani, Kanisa linalosafiri hapa duniani ikiwa ndiyo mahali pa kujindaa kwa ajili ya uzima wa milele. Lipo Kanisa la toharani, ambalo tunaamini ni Kanisa linaloteseka, na kwa kiasi kikubwa linategemea maombezi ya Kanisa la hija na la Watakatifu Wote Mbinguni. Mgawanyiko wa mwisho ni Kanisa la Watakatifu wa Mungu, ambalo ndilo mwombezi wa Kanisa la hija na linaloteseka, yaani, Toharani. Kanisa hili ndilo lililodhihirika la wateule wa Mungu, na wote waishio humo wanafana na Kristo na kufurahia Utukufu wake na kumwona Mungu kama alivyo.  Lakini wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo,” 1Yoh 3:2.

Wapendwa wana wa Mungu, tungali hapa duniani yatupasa kuishi katika matumaini hayo niliyoyasema pasipo shaka yoyote tukijua wazi kwamba maisha ya umelele yakilinganishwa na haya ya duniani, tu hapa kwa muda mfupi sana. Hivyo, “kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3. Kanisa hili la hija linatoa sadaka hii ya Misa Takatifu kwa matumaini makubwa likijua kabisa kwa sadaka ile ya Bwana wetu Yesu Kristo pale msalaba ni kielelezo cha utakaso wa Kanisa hili linaloteseka huko toharani lipate Utakakatifu. “Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,” Hek 3:9. Kanisa la hija linawajibu huu kama Sakaramenti ya wokovu kwa watu wote. Mungu pekee ambaye ni Huruma, Upendo, na Msamaha na Haki ndiye mwenye kuwahesabia haki wote waliotutangulia na hasa Kanisa hili la toharani.

Haki hiyo ya Mungu tutahesabiwa kutokana na  sadaka ya damu ya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo pale Msalabani. Hivyo, “Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,” Rum 5:9. Yapo maswali mawili ya msingi kwako na kwangu tutakayo ulizwa siku ya Mwisho. La kwanza; Je, umefanya nini na upendo wa wangu [Mungu] kupitia mwanangu Yesu Kristo kwa sadaka yake pale msalabani?  La pili; Je, umefanya nini na vipaji nilivyokupa? Ili uweze kujibu vizuri siku ya mwisho yakupasa kujiandaa vyema kuyajibu maswali haya sasa kupitia ushuhuda wa maisha yako leo. Hatuwezi kuwa na kesho yenye matumaini ya kweli kama hatuishi leo yenye matumaini ya kweli.

 Wapendwa katika Kristo, maisha ya ushuhuda wa kweli yanagharama zake. Kama yalivyo majira ya mwaka, yaani, kipindi cha baridi, joto, vuli, na kipupwe, ndivyo yalivyo maisha ya binadamu. Yatupasa kuwa wastahimilivu katika vipindi vyote vya shida, taabu, mateso na furaha, na hata kufa kwa ajili ya haki na kweli. Pamoja na maumivu tutakayoyapata katika safari hii ya kuelekea uzima wa milele, roho zetu zenye haki zitakuwa mikononi mwa Mungu. “Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1. Imani na matumaini ndiyo dira ya kushinda na kufikia hatua hii muhimu.

Maisha ya ulimwengu wa leo ni maisha yenye kusukumwa na falsafa ya umimi na ujimbilikiziaji wa mali. Katika hali hii ni vigumu sana jamii inayokuzunguka kusadifu majitoleo yako kwa wahitaji. Tupo kwenye ulimwengu wa kila mtu na yake na wakati wake. Hata katika hali na changamoto hizi tusimuonee aibu Kristo Yesu hasa tunapojali na kuithaminisha damu yake iliyomwagika pale msalabani. Kufa katika hali hii hakuna hasara yoyote. “Na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek 3:2b-3. Tunayo amani na matumaini kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili ya waovu, na hasa pale tulipokuwa hatuna nguvu za kuushinda uovu. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6.

Licha ya udhaifu wetu kama binadamu, upendo wa Mungu unajidhihirisha kwetu kwa kumtoa mwanaye afe kwa ajili yetu tungali tuna dhambi. Huu ni upendo Mkubwa sana kwetu. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka hii ya Yesu pale Msalabani ni upatanisho wetu na Mungu, na kurudishiwa hadhi ya kuwa wana wake Mungu, waridhi wa ufalme wake, na maisha ya uzima wa milele. Hivyo, Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake,” Rum 5:10. Je, tufanye nini sasa?

Wapendwa wana wa Mungu, wenzetu wesha tutangulia katika haki ni jukumu langu mimi na wewe tuishi kama tunayo siku hii ya leo na muda huu wa sasa. Hakuna kati yetu anayejua litakalotokea kwake sekunde moja ijayo. Kristo Yesu yupo daima kutusubiri na anayemwendea hawezi akampoteza. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,” Yoh 6:37. Kumwendea Kristo ni kuwa karibu naye kila wakati. Ni kuishi maisha yasiyo na hatia. Ni kuupigania ukamilifu ingawa udhaifu upo. Ni kuishi maisha ya kisakramenti na kuchota huko neema na baraka za Mungu kila wakati na kwa kila nafasi tuipatayo kushiriki masakramenti hayo. Ni kuwa waaminifu katika sheria na amri za Bwana kwa kuzishika na kuziishi. Ni kuwa tayari kupokea neema na huruma ya Mungu, na kuwa vyombo vya amani na upendo katika kusambaza neema na huruma hiyo ya Mungu kwa watu wengine.

Kwa kuyashika na kuyaishi haya kamwe Kristo Yesu awezi kutuacha leo, siku ya kufa kwetu, na mwisho siku ya ufufuo wetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa kwenye mpango wa wokovu wa Bwana wetu Yesu Kristo, naye atayatimiza mapenzi ya Mungu kwetu. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39.  Kumtazama Mwana na kumwamini kuna maanisha kujazwa uzima wa milele.

Ndugu yangu unaye safiri nami katika tafakari hii, tunamtazama Mwana na kumwamini tunapowajali wahitaji hasa wagonjwa, wafungwa, wenye njaa, wenye kiu hasa ya haki, wageni, na walio uchi, Mt 25:36-40. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:40. Je, hujakutana na Kristo Yesu bado kwa kumtazama na kumwamini? Usiende mbali bali anza hapo hapo ulipo utakutana naye.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21

Tusali:-Ee Yesu, nijalie kifo chema. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario