JUMATANO WIKI YA 29 YA MWAKA-C
Somo:
Efe 3:2-12
Zab/Kit:
Isa 12:2-3, 4ab, 5-6
Injili:
Lk 12:39-48
Nukuu:
“ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya
Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri
hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache,” Efe 3:2-3.
“Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua
ufahamu wangu katika siri yake Kristo,” Efe 3:4.
“Nanyi jiwekeni
tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40
“Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake
ajapo atamkuta anafanya hivyo,” Lk 12:43
“Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa
vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk
12:48b
TAFAKARI:
“Tu Mawakili wa Kristo, na uwakili wetu ni uwajibikaji unaojidhihirisha katika
kweli na haki.”
Wapendwa wana wa Mungu,
uwakili ni uwajibikaji katika maana ya dhamana mtu aliyopewa, na dhamana hii
ujidhihirisha katika kweli na haki. Ni maisha ya kujali na kuwajibika mara na
nyakati zote unapopima thamani ya kile ulichokabidhiwa. Kitu hicho kimulike
‘fikiri yako, amua yako, tenda yako, na ishi yako.’ Dhamana hii, na siri hii,
ndiyo Injili anayoizungumzia Mtume Paulo. Naye anawakumbusha Waefeso kwamba,
“ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu;
ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika
kwa maneno machache,” Efe 3:2-3.
Na siri hiyo ni Injili,
yaani, habari Njema ya Wokovu. Mtume Paulo anajua wazi haya yote anayoyafanya
si kwa nguvu na ujuzi wake kama mwanadamu, bali ni kwa neema ya Mungu. “Kwa
hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo,” Efe
3:4. Ni katika upendeleo huo wa Mungu kwa wanyonge wake, na kadiri
ilivyompendeza, Mtume Paulo anayatafakari hayo katika maisha yake na kusema,
“Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa
mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni
warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja
nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6.
Hakika mawazo na njia ya Mungu si njia na mawazo yetu wanadamu.
Ni kwa neema ya Mungu
Mtume Paulo anatumika kama atumikavyo kuifahamu na kuihubiri siri hiyo, yaani,
Habari Njema wa wokovu-Injili. “Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa
kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza
wake,” Efe 3:7. Ufahamu huu unaopelekea ‘kuona na kutenda kwake Mtume Paulo,
unaufunua unyenyekevu wake kama Mtume wa watu wa Mataifa, yaani, hata wale
ambao sio Wayahudi. Katika kweli hii Mtume Paulo anasema, “Mimi, niliye mdogo
kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri
Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za
madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu
aliyeviumba vitu vyote,” Efe 3:8-9.
Na siri hiyo, yaani,
Habari Njema-Injili, “kwa njia ya Kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi
ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho,” Efe 3:10. Kanisa ndiyo
chombo na alama wazi ya mwili wa Kristo, na bubujiko la Neema kama Sakramenti
ya Wokovu. Mwonekano huu wa Kanisa kama Mwili wa Kristo-wabatizwa wote, na
bubujiko la Neema kama Sakramenti ya Wokovu,
hili ndilo “kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana
wetu,” Efe 3:11. Hivyo ndani na Katika Kristo Yesu, “tunao ujasiri na uwezo wa
kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini,” Efe 3:12.
Wapendwa
wana wa Mungu, Somo letu la Injili linakazia sana kuwa tayari muda wote kwa
sababu hatujui siku ya kutoka kwenye ulimwengu huu. Hivyo kuwa katika mikono
salama ni kukesha katika utumishi wa kweli na haki katika kutenda mapenzi ya
Mungu. “Nanyi
jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40.
Jambo la msingi kupita yote katika kesha letu ni kuishi katika hali ya neema,
yaani, kutokuwa na hatia juu ya dhambi.
Pamoja na kutokuishi
katika hatia, yaani, kuishi katika neema ya utakaso, Injili ya leo inakazia
kweli hii ya kuwa watumwa katika utumishi wa utii uletao haki. Yesu anasema
heri ya mtumwa huyu anayekesha kwa utumishi wa utii na kufanya mapenzi ya
Mungu. “Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo,” Lk
12:43. Kwa kuiongoza nafsi katika kweli na neema tuipatayo kwa Sakramenti ya
Upatanisho, ndipo tunapoiokoa na kuhesabiwa haki kadiri ya mapenzi yake Mungu.
Kwa kutokufanya mapenzi
ya Mungu huku ukijua ukweli huo, itakupasa kipigo kutoka kwa Mungu. “Na mtumwa
yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi
yake, atapigwa sana,” Lk 12:47. Ni kwa
namna hiyo hiyo kwamba, “Na yule
asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo,” Lk 12:48a.
Hivyo maisha yetu hapa
duniani na fursa tulizojaliwa na Mungu vinatualika kuwa mawakili wazuri na
waaminifu. Mwisho wa siku itakupasa kutoa hesabu yake kwa namna ulivyotumia
fursa hizo. “Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye
waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48b. Ni wakati wa kila mmoja wetu kujitazama vyema ili
usije anguka katika mtego huu wa kutokukesha katika utumishi wa haki uliotukuka
katika kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa
vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk
12:48b
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nijalie neema yako ili niweze kukumbuka daima uwakili wangu kadiri
ya nafasi na wito wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario