JUMATATU WIKI YA 28 YA MWAKA-C
Somo:
Gal 4:22-24, 26-27, 31-5:1
Zab/Kit: 113:1-2, 3-4, 5a, 6-7
Injili: Lk 11:29-32
Nukuu:
“Lakini yule wa mjakazi
alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi,” Gal 4:23
“Bali Yerusalemu wa juu
ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi,” Gal 4:26
“Katika ungwana huo Kristo alituandika huru;
kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa,” Gal 5:1
“Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu
pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu
kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona,” Lk 11:32
TAFAKARI:
“Katika
ungwana huo Kristo alituandika huru; simameni, wala msinaswe tena chini ya
kongwa la utumwa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
yapo mambo mawili mazito ya kutafakari kutoka katika somo letu la Injili.
Pamoja na Yesu kukemea uhitaji wao wa ishara, Yesu anajitabanaisha kuwa yeye
ndiye Ishara halisi ya Toba na msamaha wa dhambi. Yeye ni Mungu aliyemwilishwa.
Yeye ndiye njia, ukweli na uzima, (Yoh 14:6). Hivyo leo Yesu anawakaripia wale
wasioamini uwepo wake na kubakia tu katika Ishara. Ujumbe anaotupa Yesu leo ni
kwamba Yeye ni zaidi ya Ishara zile tuzionazo.
Ishara utusaidia tu
kuelewa na kuamini mambo yale yaliyopita ufahamu wetu. Ila kwa ishara hizo kama
zilivyo haziwezi kulingana na Kristo kwa sababu wala pasipo yeye hakikufanyika
cho chote kilichofanyika, Yoh 1:3. Hivyo msingi wa imani yetu haupo kwenye
Ishara. Yesu anawaambia makusanyiko ya watu na sisi pia katika ulimwengu wetu
leo kwamba, “Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa
ishara, ila ishara ya Yona,” Lk 11:29. Ishara ya Yona ilikuwa kwamba baada ya
kukaidi kwenda Ninawi alimezwa na samaki na kukaa ndani ya tumbo la samaki kwa
siku tatu. Kwa Ishara hii, Yesu
aliwafunulia kusanyiko lile Ishara ya ufufuko wake uliotokea siku ya tatu baada
ya mateso, kusulubiwa msalabani na kufa. Hii ndiyo Ishara kubwa kupita zote na
kielelezo cha uzima wa milele.
Wapendwa
wana wa Mungu, tusipoyaona maisha yetu katika mtazamo huu wa umilele, maisha na
fahari yake yote hapa duniani hayana maana yoyote. Ninawi walikengeuka na
kumwasi Mungu, ila walitubu na kupata msamaha wa Mungu kupitia Nabii Yona. Hawa
walioamini na kumsadiki Mungu pasipo shaka ndio watakao kuwa mahakimu wetu siku
ya kiama. “Watu wa Ninawi watasimama siku
ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao
walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona,” Lk 11:32.
Miongoni mwetu hata leo wapo watu ambao kwa maisha yao na unyofu wao Mungu
anasema nasi kupitia wao. Hawa pia siku ya mwisho watakuwa mahakimu wetu. Mara
nyingi tumekuwa vinara wa kuwanyanyapaa kwa mabadiliko yao ya kiroho kwa kuzidi
kuwafananisha na maisha yao ya zamani. Hili ni kosa kubwa sana kiimani. Hakuna
mwenye hati miliki ya maisha ya umilele. Sote tunaitaji upendo na huruma ya
Mungu katika kuhesabiwa haki na kuwa warithi wa maisha hayo ya umilele.
Ndugu yangu, wewe na
mimi kama wafuasi wa Kristo, na ndivyo tulivyo Wakristo, ni ndoto na ni jambo
lisilowezekana kwenda mbinguni bila kupitia kwa Yesu Kristo. Je, tunataka
ishara gani tena zaidi ya Yesu? Katika hili Yesu anachukua nafasi mbili kwa
wakati mmoja. Kwanza ni ishara kama kielelezo cha uhai kamili na umilele. Pili, Yesu ni mfanya ishara ambazo kwayo
zaonyesha Umungu wake. Kwa nini basi ndugu yangu ukiwa na maangaiko kidogo tu
unakimbilia kwa waganga wa kienyeji kupata ishara? Kwa nini huchoki kuhama
“nyumba moja ya sala” kwenda nyingine ukitafuta ishara? Na ziita hizi ni
‘nyumba za sala,” nikitambua kuwa Kanisa ni moja tu, yaani, Mwili wa Kristo,
nasi kwa Sakramenti ya Ubatizo tu viungo vya mwili huo wa Kristo. Naposema
naenda “Kanisa la Edgar” si sahihi. Inaweza kuwa tu ‘nyumba ya sala”
inayomilikiwa na Edgar.
Wapendwa wana wa Mungu,
Kristo ndiye kilele cha historia nzima ya mwokovu wetu. Na “hata ulipowadia
utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili
sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Hili ndilo agano la
Yerusalemu ikimaanisha kwamba, Utukufu wa Mungu ulijidhihisha hapa baada ya
sadaka ile ya Yesu pale msalabani; mateso, kusulubiwa, kufa, na siku ya tatu
kufufuka. Agano hili ndilo lenye ushindi na wokovu. Agano la sinai ni agano la
utumwa na la mjakazi aliyezaliwa kwa mwili, Gal 4:24. Agano la Yerusalemu ni la
mwungwana ambalo linajidhihirisha kwa ahadi, Gal 4:23 “Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye
mama yetu sisi,” Gal 4:26. Huyu ndiye Kristo Yesu.
Kuzipenda ishara bila
kujua maana na lengo la ishara, na huyu azifanyazo hizo ishara, ni kupotea
katika imani. Katika kweli hii Mtume Paulo anaturudisha katika mstari sahihi na
kusema, “sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana,”
Gal 4:31. Na “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni,
wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa,” Gal 5:1. Kristo Yesu ndiye
ufunuo wa wazi wa Mungu, na hakuna ufunuo mwingine zaidi ya huu. Ndugu yangu
acha kupwaya pwaya katika IMANI!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Watu wa Ninawi watasimama siku ya
hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia,” Lk 11:32a
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, yafumbue macho na mioyo yetu ili tudumu katika imani ya kweli.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario