miércoles, 5 de octubre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 27 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 27 YA MWAKA-C

Somo: Gal 3:7-14

Zab/Kit: 111:1-2, 3-4, 5-6

Injili: Lk 11:15-26

Nukuu:

 “Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa,” Gal 3:8

“Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani,” Gal 3:9

“Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka,” Lk 11:17

“Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wakemutasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli,” Lk 11:18

 “Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23

TAFAKARI: “Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika somo letu la Injili ikiwa ni mwendelezo ule ule wa kumkomboa mwanadamu, Yesu anapata shutuma za kutoa pepo kwa kutumia nguvu za Pepo Mkuu- Beelzebuli. Je, mawazo hayo ya kishirikina yanatoka wapi kwa wana hawa wa Israeli? Kama kweli walikuwa wanamwabudu Mungu mmoja, iweje wawe na mawazo kama hayo? Wapendwa wana wa Mungu, tusipoachana na yaliyo yetu na ubinadamu wetu hatutaweza kuondokana na hisia za kishirikina. Ni wazi kwamba licha ya kuwa walimwamini Mungu moja, watu hawa hawakuachana na yaliyo yao na ubinadamu wao. Hisia hizo mbaya juu ya uwezo wa Yesu wa kutoa pepo kwa nguvu wasiyoijua, zinakuja kwa sababu miongoni mwao walikuwa na mazoea ya kufanya hivyo. Mara nyingi mtu humwekea hisia mbaya mtu mwingine kwa kile ambacho yeye huwa anakifikiri na kukitenda.

Kutokana na tuhuma hizo za Wayahudi juu ya uwezo wake Yesu wa kutoa pepo, ilhali Yesu akiyajua mawazo yao, anawafikirisha kidogo na kusema, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka,” Lk 11:17. Hoja hapa ni kwamba, kama Yeye, yaani, Kristo, anayafanya hayo yote na watu wanapona kwa kuutoa utawala wa pepo, kuna sababu gani ya kufanya hivyo kwa maana ya kwenda kinyume cha yule aliyempa nguvu hizo yaani Beelzebuli? Kwa kufanya hivyo kama hoja yao inamshiko ni kujichanganya kwa utawala huo wenyewe. Ila Yesu anawaambia kwama hayo yote anayafanya kwa uwezo wa Mungu mwenyewe. Na kwa mantiki hiyo Ufalme wa Mungu huu kati yao tayari. Hawana sababu ya kuwa na hofu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk 11:20. Ni mara ngapi tunapata nguvu na uponyaji kwa njia ya sala na maombi na mara tupatapo tena shida kama hiyo tunakosa imani na kwenda kwa waganga wa kienyeji? Kwa nini basi unatapatapa katika Imani?

Wapendwa wana wa Mungu, kujitenga kwetu na Mungu kwa kufuata mambo yetu na ubinadamu wetu ndiko kunakotunyima neema na baraka zake. Tunajifungia milango wenyewe na tunapokosa neema na baraka hizo tuna mtafuta mchawi aliyeturoga. Ni sawa na mlevi aliyepoteza ufunguo kwenye Kilabu cha pombe akawa usiku kucha anatafuta ufungua barazani mwa jirani yake eti kwa sababu tu pale kuna mwanga. Je, ataupata ufunguo huo? Ndiyo maana Yesu leo anatuambia maneno haya mazito, Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23. Ndugu yangu, hakuna namna nyingine tuwezayo kupata neema na baraka kama hatutajisalimisha moja kwa moja kwa Kristo.

Imani yetu ndani na katika Kristo Yesu Mwokozi wetu ndiyo ponya yetu kwa sababu, Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:11-12. Na kwa kutokuamini kwao Wayahudi, Mtume Paulo anawarudisha nyumba kwa Ibrahimu ambaye Mungu alimhesabia haki na kuwa mfano wa mtu aliyekuwa na Imani thabiti. “Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa,” Gal 3:8. Na kwa kuhesabiwa haki huku kwa Ibrahamu kama Baba wa Imani haikuwa kwa sababu ya matendo ya sheria.

Akiwa ndio mfano na muhimili wa Imani katika agano lile la kale, waliokuwa na Imani kabla ya ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo walibarikiwa pamoja  Ibrahimu. Kwa mantiki hiyo,  “hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani,” Gal 3:9. Matendo ya sheria ambayo yalikuwa ni ukweli wa Mungu ulipotoshwa kwa kukidhi matakwa ya kibinadamu hayakuwa na Umungu ndani yake, na hivyo kuhesabika kama laana. Na Yeremia Nabii anasema, Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Na, amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:5,7. Yaliyo ya kibinadamu na yenye lengo la kunyanyua binadamu katika ubinafsi wake hayana thawabu mbele ya Mungu.

Ni vyema kuelewa kuwa Mtume Paulo haipingi torati kama ilivyoachwa na Musa, bali anapinga tafasiri ile ya torati-Talmud, ambayo ilipewa kipaumbele zaidi ya torati yenyewe. Hata Yesu mwenyewe haipingi torati zaidi ya kuikamilisha kama asemavyo, Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Hivyo ni makosa kufikiri kwamba Mtume Paulo anaipinga torati kama ilivyo.

Ni katika mazingira haya ya tafasiri ya torati, Mtume Paulo anayasema haya kwamba, “wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye,” Gal 3:10. “Yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ayafanye,” ni yale yaliyofafsiriwa na walimu wa sheria kutoka torati yenyewe, na yaliyobeba ubinadamu zaidi kuliko Umungu. Kwa kuyafuata hayo kuna laana ndani yake. Yamebeba utukufu wa mwanadamu ambao kwayo hauwezi kumkomboa. Ni mbwembwe tu.

Ni kwa mantiki hiyo kwamba, “ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani,” Gal 3:11. Kwenye haki ataishi milele kwa sababu tunda la haki ni amani, na penye amani upendo ujidhihirisha. Na penye haki, amani, na upendo Mungu hujidhihirisha, na imani ukolezwa zaidi na zaidi. Kwa mtazamo huu, “torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo,” Gal 3:12. Torati ambayo ni sheria ya Mungu katika upana wake, utusaidia kuibainisha dhambi, na kuishi kadiri ya mapenzi yake Mungu. Ni Kristo Yesu pekee aliye muhimuli kati ya hiyo torati-sheria, na upendo huo wa Mungu Baba usio na kipimo.

Kristo Yesu ndiye anayeweza kututoa katika anguko hili la laana. “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani,” Gal 3:13-14. Kwa kifo chake cha Msalaba na kwa ufufuko wake, Mungu “akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:20-23. Huyu ndiye twapaswa kushikamana naye kwa sababu ndani na katika yeye ipo njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie neema tudumu katika imani ndani na katika Wewe. Amina.

No hay comentarios:

Publicar un comentario