jueves, 20 de octubre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 29 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 29 YA MWAKA-C

Somo: Efe 4:1-6

Zab/Kit: 24:1-2, 3-4ab, 5-6

Injili: Lk 12:54-59

Nukuu:

“Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa,” Efe 4:1

“kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo,” Efe 4:2

 “Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” Lk 12:56

 “Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani,” Lk 12:58

TAFAKARI: “Mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna yeyote kati yetu kwa kile alicho leo kwake ni bahati mbaya. Iwe leo mimi ni mlei, mtawa, mtawa na mkleri, au mkleri, yote ni kwa mpango na kusudi la Mungu kuishi kusudi lile la kuumbwa kwangu; yaani, nimjue muumba wangu, nimpende, nimtumikie, na mwisho nirudi kwake mbinguni. Na hatma ya maisha yako na yangu ni umilele. Hivyo wajibu msingi kwa kila mmoja hapa duniani ni kuenenda kama ilivyostahili wito wake alioitiwa. Na huu ndio ujumbe wa Mtume Paulo kwangu na kwako, kwamba, “nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa,” Efe 4:1.

Paulo ni mfungwa wa Kristo katika maana ya kuyasalimisha maisha yake yote ndani na katika Kristo Yesu. Kama ni tunu ya thamani katika maisha yake Paulo Mtume ni ‘Kristo katika yote.’ Hivyo kujisalimisha kwangu kwa Kristo kusiwe kwa asimila kadhaa tu. Asilimia 95 hazitoshi! Leo katika maisha ya ufufuko, mimi na wewe lisiwe lengo la kuisha kwa kukubaliana kwa kutokubaliana. Ni kuishi yote katika yote, yaani, “kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo,” Efe 4:2. Tunapochukiliana katika hali na mazingira haya, Roho Mtakatifu huyaongoza na kuyaratibisha yote hata pale tunapokosa majibu katika hali ya sintofahamu.

Na hili ndilo alilomaanisha Yesu kwamba, “lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:19-20. Hivyo ni jukumu langu na lako “kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani,” Efe 4:3. Na kuishi katika kweli hii kunamaanisha kuishi katika  “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,” Efe 4:4-5. Na Mungu huyu tunayemwamini, mwabudu, na kumpa shukrani zetu “ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote,” Efe 4:6. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba, ndani na katika Kristo Yesu upo salama. Unachoitajika kukifanya ni kimoja tu, yaani, jisalimishe kwake bila kujibakiza. Na hii ndiyo kweli na siri ya maisha yale ya umilele.

Lakini siri hii ya maisha ya umilele ujifunua hatua kwa hatua tunapoishi na kuenenda kwa uaminifu kila mmoja kama ilivyostahili wito wake alioitiwa. Je, niende wapi kumtafuta Kristo? Ndugu yangu, tukio lile la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo limeweka wazi ni wapi yanipasa kumtafuta na kukutana na Kristo Yesu. Katika hali ya kufadhaika kwa wale waliokwenda  kaburini na kulikuta lipo wazi, watu wawili waliosimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta, waliwaamba, “kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?” Lk 24:5. Watu wale waliwaambia wakumbuke aliyoyasema Yesu alipokuwapo nao Galilaya. Kuanzia siku ile Kristo Yesu hakuwa anapatikana makaburini, yaani, kusiko kuwa na tumaini, bali kwenye tumaini jipya yaani, Galilaya. “Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7. Ndugu yangu, Galilaya yako leo ni kile ulichoitiwa kadiri ya wito wako. Hapo utakutana na Kristo Yesu endapo utaishi kwa uaminifu na hofu yake Mungu. Na hapo ndipo penye utakatifu wako.

Hata hivyo ukweli ni kwamba, sheria ya Mungu katika utu wa ndani, ni UHURU aliyopewa mwanadamu umsaidia katika mambo mazuri kumwelekea Yeye na ufalme wake. Kufurahia uhuru huu katika ubaya ndilo anguko la mwanadamu. Sheria ya utu huu wa ndani, yaani uhuru ulionao unapoifanya nafsi yako kuegemea mwili, ndipo mtu anapodondoka kwenye dhambi iliyo katika viungo vyake. Hii ni sawa na nafsi kupigwa mwereka na uhuru huu ambao ndiyo sheria ya ndani ya utu wako. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu,” Rum 7:22-23. Kujinasua katika mtego huu ni kutambua na kuyafanya matendo ya Roho ambayo ndani kwayo yamejaa uhai na uzima, Gal 5:22-23.

Unapotambua hali hiyo na usifanye chochote ndicho anachosema leo Yesu katika Injili. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” Lk 12:56. Ni kuujua ukweli kama ulivyo  nawe ukabaki katika ubishi na ung’ang’anizi usio na uzima ndani yake. Watesi wa Yesu nyakati zake, hasa Waandishi, Mafarisayo na Wanasheria, waliujua ukweli lakini waliupindisha kwa makusudi kukidhi haja zao na maslahi yao.

Yesu anawashauri na kutushauri sisi leo kwamba, kama tunaufahamu ukweli basi tuufuate na kuufanya tungali hai kwani hakimu wetu Mungu yupo anasafiri nasi kuelekea kwenye kiti cha hukumu. Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani,” Lk 12:58. Kumbe kabla ya kutupwa gerezani, yaani kwenye mateso yasiyo na mwisho, Mama Kanisa anatushirikisha huruma ya Mungu kwa kupitia Sakramenti ya upatanisho. Sote tunahitaji toba na kupatanishwa na Mungu kila tunapodondoka katika dhambi.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?” Lk 12:56

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nifunulie hatua kwa hatua siri ile ya uzima wa milele kadiri ya zawadi ya wito ulionijalia. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario