domingo, 23 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 30 YA MWAKA-C





JUMANNE WIKI YA 30 YA MWAKA-C

Somo: Efe 5:21-33

Zab/Kit: 128:1-2, 3

Injili: Lk 13:18-21

Nukuu:

“Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24

“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27

 “Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa,” Efe 5:29

 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe,” Efe 5:33

“Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini?” Lk 13:18

“Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19

“Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia,” Lk 13:21

TAFAKARI: “Upendo wa Kristo na Kanisa lake.”

Wapendwa wana wa Mungu, upendo wa Kristo na Kanisa lake ndicho kiini cha pendo zote. Upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi Yesu Kristo, Mungu hujidhihirisha kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani.

Upendo wa Mungu na mshikamano na mwanaye tunauona katika Masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa ukaribu Sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume Paulo anasema, Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao vyuma chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?

Kwa upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndipo penye utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya pekee sana zaidi ya nyie kuyasadifu yale wayatendayo wake zenu kila siku katika familia. Tabia ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.

Utii wa kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa kupitia Sakramenti hiyo. Hivyo, kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele, Yoh 1:3. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31.

Tendo hili la ajabu katika Sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha Sakramenti hiyo ya ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufa katika uhalisia wa mambo na ukweli wa Kimungu. Kilicho baki ni maigizo tu, na wote mmekuwa wasanii katika Sakramenti hii Takatifu.

Hata hivyo, hayo yote tuishiyo kila mmoja kadiri ya wito yake ulenga katika imani ya kweli itupelekayo katika uzima wa milele. Swali ni hili; Je, imani hiyo itupelekeayo kwenye Ufalme wa Mungu ina mfanano gani?

Jibu la swali hili limetolewa katika Injili ya leo. Yesu anauliza aufananishe na nini na ufalme wa mbingu? Kwanza Yesu anasema ufalme huu, Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19. Maana yake nini? Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, imani ni kuamini na kusadiki pasipo shaka yale mambo madogo madogo yanayoonekana na yasiyooneka na yenye kuufunua utukufu wa Mungu.

Punje ya haradali ni ndogo sana. Lakini katika udogo huu mwisho wake huwa mti mkubwa na ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Imani si jambo la siku moja, bali imani ukua hatua kwa hatua kadiri tunavyoishi na kuona vitu na mazingira yake kwa mwono wa Kimungu, (Kila kitu kuwa na sababu yake).

Pili, Yesu anasema ufalme wa Mungu umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia,” Lk 13:21. Imani ya kweli na thabiti ni nguvu ya ndani ya ajabu kwa mtu ambayo hubadili kabisa mwonekano wa vitu kwa mtu, utendaji, na hata namna ya kuyachukulia mambo. Chachu katika uchache wake hubadili kabisa mwono na umbo wa kile kilichochachushwa. Imani hii ndiyo inayotupa nguvu na dira mpya ya kuyaona maisha kwa namna ya pekee licha ya ufupi wake na sababu ya kuishi kwetu hapa duniani, katika maana ya makazi ya muda mfupi. Makazi haya ni sehemu ya maandalizi ya maisha ya umilele ambayo ndiyo Ufalme wenyewe wa Mungu.

Hivyo ndugu yangu, tunapoishi hapa duniani mambo haya yafuatayo yatupasa kuyazingatia. Moja,  msingi wa maisha yetu lazima ujengwe katika haki. Kwani, yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kumb 16:20. Pili, tusienende katika tamaa za wanadamu. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani,” 1Pet 4:2. Na tatu na mwisho, kuishi kwetu kuwe ndani na katika Kristo. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida!” Flp 1:21. Kristo ndiye mtetezi wetu na mwokozi wetu. Amina

Tumsifu Yesu Kristo!

“Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa,” Efe 5:29

Tusali:-Ee Yesu, nijalie furaha ya kweli katika wito wangu. Amina
 
 

No hay comentarios:

Publicar un comentario