domingo, 30 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 31 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 31 YA MWAKA-C

Somo: Flp 2:1-4

Zab/Kit: 131:1, 2, 3

Injili: Lk 14:12-14

Nukuu:

“Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja,” Flp 2:1-2

 “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo,” Lk 14:12

“Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki,” Lk 14:13-14

TAFAKARI: “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tunaishi katika ulimwengu wa ushindani mkubwa sana,  na mbaya zaidi ushindani unaojali nafsi na ubinafsi. Hakuna anayetaka kwenda kwa hasara ingawa ndilo lengo la ye yote yule aliye katika ushindani hasa ushindani wa kibiashara. Ni hulka ya binadamu kutafuta mafaa katika faida. Hivyo kwa mazingira ya leo na mtazamo wake, ukihimidi hali hii basi utaupata ulimwengu wote.

Hata hivyo, Yesu anatupa angalizo hasa kwa wale wenye kusombwa na hulka hii kiasi kwamba kusahau sehemu ile ya pili ambayo ni muhimu sana, yaani, NAFSI na ROHO. Binadamu ni mwili, nafsi na roho, na vyote na vyote vitatu ndivyo vimfanyavyo binadamu aliye hai. Mwili ni nyumba ya Nafsi na Roho, ingawa nafsi ipo kati ya mwili na roho. Nafsi ikiegemea mwili utaishia katika matendo ya mwili ambayo kwayo hakuna uzima wa milele, Gal 5:19-21. Na nafsi ikiegemea Roho matokeo yake ni tunda la roho, ambalo kwalo kuna uzima wa milele, Gal 5:22-23.

Ni katika mazingira haya Yesu anazihoji dhamiri zetu na kwa kutoa angalizo, na kusema, “kwa kuwa itamfaidia mtu nin kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala  ya nafsi yake?” Mk 8:36-37. Basi nikiwa nafanya ushindani wowote ule ni ufanye nikilenga faida ya wote. Hivyo “Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja,” Flp 2:1.2. Huu ni upendo na mwono wa kujali kama wafuasi wake Kristo tukijifunza unyenyekevu wake na utii kwa Mungu Baba.

Mwito kwetu leo sote kama wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake, yatupasa kueneka katika hofu ya Mungu. Na hofu hii ya Mungu utusuma kutenda bila majivuno bali kwa unyenyekevu na kuwajali wengine. Na hili ndilo analosisitiza Mtume Paulo kwetu, kwamba, tusitende, “neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake,” Flp 2:3. Na kama ni faida basi iwe kwa ajili ya wengi. Hivyo,  “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine,” Flp 2:4. Mtindo huu katika kufikiri, kuamua na kutenda, unasema zaidi kuhusu tabia ya Yesu Kristo na kuthibitisha pendo lake kwetu. Naye Yesu katika kweli hii anasema, “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13.

Na tabia ya Yesu inasema zaidi kuhusu mtindo wake wa maisha ulivyokuwa. Yesu licha ya kwamba hakuwa hata na mahali pa kulaza kichwa chake, Lk 9:58, marafiki zake wakubwa walikuwa masikini, vilema, viwete, vipofu, wadhambi, wakoma, wazinzi, watoto, akina mama, waliotengwa na wale wote walikata tamaa. Ukaribu na urafiki wa Yesu katika makundi haya ya watu haukulenga kudumisha mtindo wa maisha yao, bali kuwatoa katika hali zao za unyonge, na kufurahia nuru na neema ya Mungu. Mimi na wewe tunahitaji nuru na neema hiyo ya Mungu.

Tabia hii ya Yesu inajidhihirisha katika Injili yetu ya leo hasa katika matendo yale ya upendo na huruma. Namna yetu ya kufikiri, kuamua, na kutenda kuwe na mwelekeo wau pendo na huruma hasa pale tunapoigusa jamii inayotuzunguka. Na katika kweli hii Yesu anasema, “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo,” Lk 14:12. Kufanya hivyo ni kuukubali upendo faida-nipe nikupe. Huu ni upendo linganishi na shindanishi. Ni upendo usio tayari kupoteza kwa faida na mafaa ya wengi. Huu ni upendo tasa na wenye kubaki katika hali ile ile ya mwenendo sawa bila mabadiliko ya kupoteza.

Bali kinyume chake Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki,” Lk 14:13-14. Huu ni upendo ule ulio tayari kutoa bila tegemeo la kupokea. Ni upendo wa kujitoa bila faida. Ni upendo unaotazama mafaa ya kitu kama kilivyo kwani cha stahili. Ni upendo wenye kuwajibisha kwa sababu huwezi kupenda ukaacha kutoa. Ni upendo uliokomaa na ulio tayari kuzaa. Na kimo cha upendo huu ndicho hiki asemacho Kristo Yesu, kwa namna nyingine, kwamba, “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24.

Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, hakuna haja ya kwenda mitaani, na mijini kuwatafuta hawa marafiki na wapendwa wa Kristo Yesu. Marafiki hawa wa Yesu na wapendwa wake unao hapo ulipo. Embu anza kutazama vizuri hapo nyumbani kwako (Mke, watoto, ndugu, na wafanyakazi wote). Je, hawapo? Embu tazama vizuri pia katika Jumuiya yako ndogo ya Kikristo (familia zake, wanajumuiya wote, na mahitaji yao na Kanisa Mahalia). Je, hawapo? Bila shaka baada ya zoezi hili utakutana na marafiki na wapendwa hawa wa Kristo Yesu. Fanya kitu kwa ajili yao. Amina!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki,” Lk 14:13-14

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nipe macho ya kuona marafiki na wapendwa wako, na nijalie moyo wa kuwapenda kama ulivyo wapenda na kuwajali. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario