lunes, 3 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 27 YA MWAKA-C


JUMATANO WIKI YA 27 YA MWAKA-C

Somo: Gal 2:1-2, 7-14

Zab/Kit: 117:1, 2

Injili: Lk 11:1-4

Nukuu:

“Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja name,” Gal 2:1

“Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure,” Gal 2:2

 “Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake,” Lk 11:1b

 “Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]” Lk 11:4

TAFAKARI: “Kuishi na kusimama katika kweli na haki. Michanganyo Bwana Yesu amekataa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuongoka kwa Mtume Paulo kulimaanisha mwisho wa maisha yake ya zamani, na kuzaliwa upya ndani na katika Kristo Yesu. Kuongaka huku kuliko maanisha kuzaliwa upya ndani na katika Kristo Yesu, kunampa wajibu mpya Paulo mbele ya Kristo Yesu, yaani, kuihubiri Habari Njema ya Wokovu. Mtume Paulo anaanza mwelekeo mpya wa maisha yake ya kiimani ndani na katika Kristo Yesu.

Jukumu hili zito hakulifanya mwenyewe, bali kwa kushirikiana na jumuiya ile ya kwanza ya Kikristo, na chini ya mamlaka iliyokuwepo- Petro aliyejulikana kama Kefa. Naye Paulo anasema, “Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja name,” Gal 2:1. Umoja huu katika uinjilishaji, yaani, Paulo, Barnaba na Tito unatoka nje ya mipaka ile ya Yerusalemu na kwenda kwa watu wa Mataifa, yaani, wale wasiokuwa Wayahudi.

Tendo hili la kipekee si tokeo la kukurupuka, bali limefunuliwa kwake Paulo kama asemavyo kwamba, “Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure,” Gal 2:2. Hali na mazingira ya nyakati zile hayakuwa rafiki sana kwa kazi hii ya uinjilishaji. Licha ya miundo mbinu kuwa mibovu, Paulo alipata upinzani mkubwa sana kutoka kwa Wayahudi wenzake.

Hata pamoja na upinzani huo mkubwa, Paulo alisimama imara katika imani, kweli na haki na wala hakuyumbishwa kwa kile alichokiamini. Hii yote ni neema ile ya Mungu iliyokuwa ikifanya kazi ndani yake kama asemavyo, “kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi  Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu,” 2Kor 12:8-9. Kwa neema hii ndani yake, Paulo hakuwa na shaka lolote kwa kile alichokuwa anaishi na kukihubiri.

Kwa msisitizo Paulo anasema, na “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara,” Gal 2:9. Watu wa tohara hapa ilimaanisha wale wafuatao mila na desturi za kiyahudi na hasa swala zima la kutahiriwa. Na kwa kiasi kikubwa swala hili la kutahiriwa lilitumika kama kigezo cha kuwa Mkristo. Mtaguso wa Yerusalema, Mdo 15, ulizungumzima jambo hili pamoja na mambo mengine yaliyohusu kuhubiri Habari Njema ya Wokovu.

Hivyo jukumu analopewa Mtume Paulo kama lilivyo funuliwa kwake, na  kadiri ya jumuiya ile ya Wakristo wa Yerusalime ni kuihubiri Habari Njema kwa Mataifa. Na katika kuhubiri huko Mtume Paulo anasema, “neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya,” Gal 2:10. Maagizo haya Mtume Paulo aliyafanya kwa nguvu zake zote na bila kupindisha kweli ile.

Kinyume chake, Petro ambaye alijukana kama Kefa, alipofika Antiokia alikuja na mtindo wake wa ‘mchanganyo,’ ambao ulimsikitisha sana Paulo. Naye Paulo anasema, “Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu,” Gal 2:11. Michanganyo hii ambayo Bwana wetu Yesu Kristo haitaki iliwa hivi; “kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, (Kefa) alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao (Wayahudi), akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa,” Gal 2:12. Huu ni unafiki mkubwa aliokuwa akiufanya Kefa-Petro. Hii ndiyo michanganyo tunayoiona katika imani hata leo.

Hali hiyo haikuwa tu kwa Kefa, bali hata kwa wale waliokuwa kwenye njia, yaani, Imani, ndani na katika Kristo Yesu. Hivyo, “Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao,” Gal 2:13. Barnaba ambaye alikuwa kundi moja na Paulo naye anaingia katika unafiki huu. Tendo hili linamkwaza sana Paulo. Kwa kusimama katika kweli na mafundisho ya kweli, Paulo anasema, “Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?” Gal 2:14. Huu ndio uliokuwa unafiki wa Kefa na michanganyo katika imani.

Hata hivyo, pamoja na hatia alizokuwa nazo mtu, Mungu hubaki kuwa HURUMA, MSAMAHA, UPENDO NA AMANI yetu. Huruma hii na upendo huu wa Mungu, tunaiona katika sala ya Baba yetu ambayo leo mmoja wa wanafunzi wa Yesu anamwomba Yesu awafundishe namna ya kusali. Katika sala hii inatufundisha na kuweka wazi ni nani aliyekimbilio letu la pekee, na mapaswa yetu tungali hapa duniani. Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]” Lk 11:2.

Jambo lingine la msingi ni huruma ya Mungu kwa msamaha wa makosa yetu inayotokana na kiwango kile kile cha sisi kuwasamehe wale waliotukosea. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu],” Lk 11:4. Wapendwa wana wa Mungu, kama kipimo cha kupenda ni kupenda bila kipimo kama asemavyo Mt. Agustino, basi ni hivyo hivyo masharti ya kusamehe ni kusamehe bila masharti.

Ndugu yangu, sintofahamu kati ya Paulo na Kefa haikuwa sababu ya kukwamisha wajibu ule wa kuihubiri Habari Njema. Mara zote tujifunze kutoka makosa yetu, na mara tuanze upya na kwa nguvu mpya.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake,” Lk 11:1b

Tusali:-Ee Yesu Kristo, tujalie neema zako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario