lunes, 10 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 28 YA MWAKA-C


JUMATANO WIKI YA 28 YA MWAKA-C

Somo: Gal 5:18-25

Zab/Kit: 2:1-2, 3, 4, 6

Injili: Lk 11:42-46

Nukuu:

 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21

“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23

 “Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo,” Lk 11:44

TAFAKARI: “Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.”

Wapendwa wana wa Mungu, mtu kamili anakuwa katika sehemu kuu tatu:- Nafsi, Roho, na Mwili. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi Nafsi zenu na Roho zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23. Katika hili Roho na Nafsi huwa pamoja na ndizo wewe mwenyewe. Mwili ni nyumba ya roho na nafsi. Katika uumbaji Mungu aliumba mwili kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani ambayo ni roho yake ndipo mtu huyo akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7. Miili tuliyonayo ni nyumba ya Nafsi na Roho.

 Kwa hali hii sisi binadamu ni wawili. Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi na Roho, na mtu wa nje ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi kuwatenganisha wala kumwona kwa macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo. Huyu mtu wa nje hukua, kuzeeka na kufa Mtu wa ndani hakui, hazeeki, wala hafi Mtu wa ndani hubadilika kwa kuchakaa kunakotokana na kujeruhiwa na kuumizwa kunakosababishwa na dhambi na matukio mbalimbali yanayomsibu binadamu.

Mtu wa ndani alianza tangu pale kutungwa mimba siku ya kwanza wakati yai na mbegu na pumzi ya Mungu alipoweka roho yake Mtu huyu wa ndani hakui wala haongezeki ila hufanywa upya. “Kwa hiyo hatulegei, bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16.

Nafsi ikiegemea rohoni huleta matunda mzuri. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Gal. 5:22-23.

Ila nafsi inapoingia katika Mwili mambo huwa mabaya kwani ufanya matendo ya mwili kama tusomavyo katika maandiko matakatifu, “basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal.5:19-21. Ni vizuri kujua nafsi yako imeegemea wapi. Ikiegemea rohoni utaenda Mbinguni, ikiegemea mwilini utaenda motoni.

Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo Yesu anawakemea Mafarisayo na wana sheria kwa kutokuishi katika kweli na haki. Yesu anawafananisha Mafarisayo na wataka sifa bila kuwa na siha, wajikwezao bila thaminisho la kweli, na mwisho wajipambao kwa uzuri na wema ingali wameoza kabisa ndani yao. Haya ndiyo makaburi yanayovutia machoni mwa watu ili hali ndani yake ni majanga na fedheha.  Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo,” Lk 11:44. Ndugu yangu, katika maisha yako jaribu mara zote kuwa kile ulicho.

Hatua ya kwanza ni kuwa binadamu na kuikubali hali hiyo ya kibinadamu. Mungu hawezi kukupandisha ngazi nyingine kama haupo tayari kukubali ubinadamu wako aliyo kuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Yesu alipowapa Mafarisayo ukweli juu ya maisha yao, wanasheria walimjia juu na kutaka kujua kama wao nao wapo salama. Yesu akawajibu, akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu,” Lk 11:46. Wana-sheria yawapasa kusimama katika kweli na haki siku zote.

Leo katika jamii yetu, watu hawa (wana sheria) wanadhamana kubwa sana katika mizania ya kweli na haki. Rushwa na ufisadi vimekuwa mitengo hatarishi sana katika sekta zote za utumishi serikalini. Haki ya mtu haiwezi nunuliwa kwa gharama yoyote ile. Uwepo wa mtu na haki yake ambayo inayochezewa, hali hiyo imewekwa na Mungu mwenyewe kwa chapa ya uumbaji wake wa peke wa mtu huyo. Hivyo ni Mungu mwenyewe anayestahili kulipwa haki hiyo.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria,” Gal 5:18

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tuongoze katika kweli yako daima. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario