viernes, 21 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 29 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 29 YA MWAKA-C

Somo: Efe 4:7-16

Zab/Kit: 122:1-2, 3-4a, 4b-5

Injili: Lk 13:1-9

Nukuu:

“Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo,” Efe 4:7

“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu,” Efe 4:11

 “Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Lk 13:2

“Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:3

TAFAKARI: “Msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”

Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo inatuasa kutumia vyema fursa hii ya upendo na huruma ya Mungu kwa kuishi matendo ya roho na kuachana na matendo ya mwili. Tusipoteze Muda mwingi kuzitazama dhambi za watu wengine na hata maafa ya watu wengine tukafikiri kwamba wao ni waovu kupita sisi.

Yesu analiona hilo kwa wayahudi wanapomsimulia tukio lile la Pilato kuchanganya damu za Wagalilaya na dhabibu zao. Yesu akawaambia, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Lk 13:2. Je, nasi tunatofauti na hao Wayahudi kwa fikra na matendo yetu? Ndugu yangu, mimi na wewe tunaambiwa hivyo hivyo na Yesu.

Miongoni mwetu  wapo baadhi yetu ambao ni hodari sana wa kuyasema maovu ya watu wengine na wakati mwingine wayasemayo na kuyashuhudia hayana ukweli wowote juu ya kile wakisemacho au kukishuhudia. Uzushi katika jamii yetu leo umekuwa ndiyo wimbo tuupendao na uujazao vinywa vyetu. Je, tumepata nafasi ya kuyachunguza maisha yetu kwa undani? Kama hatufanyi jambo hili hatuwezi kuepuka kuwa wanafiki.

Yesu anatukaripia kwa nguvu zote kuhusu unafiki wa mtindo huu na kusema, “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako,” Mt 7:5. Hakuna njia ya kuepukana na unafiki huu kama hatutafanya tafiti moyo na kufanya toba ya kweli. Nawaambia,  lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:3. Kilichowapata wengine kwa mtindo ule ule kitatupata nasi tusipotubu na kumrudia Mungu.

Mungu wetu ambaye ni Upendo na Huruma humjalia kila mmoja wetu nafasi na muda wa kutosha kujirekebisha. Mungu huyu asingekuwa hivyo, tusingeendelea kuishi hata kwa sekunde moja tungali na dhambi zetu. Ukimya wa Mungu juu ya dhambi zako siyo kwamba haoni kinachoendelea ndani yako, bali anakupa  muda wa kutosha kufanya tafiti moyo na toba ya kweli.

Mungu wetu ni huruma kama mtunza bustani alivyomjibu mmiliki wa mtini kwa kutokuzaa matunda yake kwa miaka mitatu mfululizo. “Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate,” Lk 13:8-9. Mungu wetu ni Mvumilivu sana kwa sababu anatupenda sana. Ni kwa sababu ya Upendo wake Mungu alichagua kutuumba kama tulivyo kwa sifa na utukufu wake.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii yatupasa kutumia vyema nafsi na muda tulionao kuyatenda matendo ya roho. Huu siyo wakati wa kupoteza muda kwa kuyatazama makandokando ya wengine. Ni vyema ukatambua uzito na vilema vyako ili upata kumtukuza Mungu kwa yale aliyokujalia ya pekee. Ukweli ni kwamba, “kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo,” Efe 4:7. Basi ni vyema kutumia muda katika kuvitambua vipawa hivi na kuvitumia kwa sifa na utukufu wake Mungu.

Mungu wetu aliye Upendo, amemkirimia kila mmoja wetu vipawa na karama kadiri ya hitaji lake yeyé aliyemwuumba, yaani, Mungu. Hakuna sababu yoyote ya kuwa kivuli kwa kutamani vipawa vya wengine. Ni katika maana hii kwamba, Mungu kadiri alivyoona inafaa “alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu,” Efe 4:11. Mpangilio huu una kusudi lake.

Utofauti huu siyo ile hali ya kuzidiana na kujiona nani zaidi, bali katika utofauti huu tuweze kufaidiana. Na kufaidiana huku ndiko tunapokamilishana katika kuujenga mwili wa Kristo, yaani, Kanisa lake-wote waliobatizwa. Na hili ndilo lengo la Mungu, yaani, “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe,” Efe 4:12. Na hatma ya ukamilisho huu ni “kuufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo,” Efe 4:13. Na cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo ni Utakatifu ule ambao mimi na wewe yatupasa kuuchuchumilia usiku na mchana. Bila UTAKATIFU huwezi kuuona uso wa Mungu.

Ukomavu wa Kiroho ni hatua ya kuufikia ukamilisho, yaani, utakatifu wako. Lengo la makuzi haya ya kuufikia ukomavu huo “ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu,” Efe 4:14. Na dalili ya kutokuwa na ukomavu wa kiroho ni pale unapoona Mkristo akiyumbishwa hapa na pale kwa kukosa imani thabiti. Leo utamsikia kaokoka, na kesho kutwa kasilimu. Ukomavu wa kiroho ni kuishika kweli ndani na katika Kristo Yesu. Hivyo, “tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeyé aliye kichwa, Kristo,” Efe 4:15. Kristo ndiye Njia, kweli, na Uzima, Yoh 14:6. Amina!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo,” Efe 4:15

Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ili tuzame ndani zaidi mioyoni mwetu ili tuvijue vipawa ulivyotujali, na tuvitumie kwa sifa na utukufu wako.

No hay comentarios:

Publicar un comentario