Somo
I: YbS 35:12-14, 16-19
Zab/Kit: 34:2-3, 17-18, 19, 22
Somo II: 2Tim 4:6-8, 16-18
Injili: Lk 18:9-14
Nukuu:
“Kwa kuwa Bwana ndiye
mhukumu wala hakijali cheo cha mtu,” YbS 35:12
“Hatakubali yeyote juu
ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa,” YbS 35:13
“Nimevipiga vita
vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa
taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi
tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake,” 2Tim 4:7-8
“Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia
nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie
Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba,” 2Tim 4:17
“Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni
mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi,
wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa
juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote,” Lk 18:11-12
“Lakini yule mtoza
ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali
alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk
18:13
“Nawaambia, huyu
alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila
ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:14
TAFAKARI:
ANGALIZO: “Waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 30 ya mwaka “C” wa Kanisa. Tafakari ya
Dominika hii imezama katika ‘angalizo,’ hasa kwa wale ambao twajikinai ya kuwa
tu wenye haki, na kuwadharau wengine. Ndugu yangu unayesafiri nami katika
tafakari hii, uwe kile ulicho ikiwa na fahari zake zote, lakini elewa jambo
hili muhimu katika maisha yako kwamba, “Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo
cha mtu,” YbS 35:12. Falme, nguvu, fahari, na madaraka mara nyingi humtia mtu
upofu. Wahenga wanasema, ‘mpe mtu madaraka, nawe utaijua tabia yake.’
Kwa falme unayomiliki,
nguvu ulizo nazo kutokana na cheo chako, fahali unayojitapia, madaraka
unayoyatumia kama fimbo kuwachapa wengine, kwayo hayo kama yalivyo hayata
kuhesabia haki mbele za ngumu, na mbaya zaidi unapoyatumia ndivyo sivyo.
Binadamu katika fahari yake ufikia hatua ya kumtunishia misuli mwenzake na
kumwambia, ‘nauwezo wa kukuadhibu kwa fedha, na kukulipa fedha.’ Fikra na
taswira kama hizi huakisi jamii tunayoishi. Mwenye fedha na utajiri kwenye
jamii hii iliyoporomoka kimaadili hawezi kufungwa hata kama imethibitika kuwa
anakosa na anastahili adhabu. Mara nyingi katika kesi za watu kama hawa
“Mabwanyenye na akina Pedezee,” mahakama uishia kusema, ‘mtuhumiwa alifanya
kosa hilo kwa kutokukusudia.’ Na hapa ndipo huwa mwisho wa kilio cha mnyonge.
Ila umweli ni kwamba,
kilio cha maskini na mnyonge hakipotei bure kama machozi ya samaki kwenye maji.
Mungu kamwe “hatakubali yeyote juu ya
maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa,” YbS 35:13. Leo kati yetu
wapo wanao vikuna vitambi vyao kila kukuchwa kwa furaha ya kuwadhulumu wanyonge
na wajane. Leo wapo pia watu kati yetu wanao wadhulumu wajane fedha za mirathi
za waume zao kwa kuchukua asilimia themanini na kumpatia mjane asilimia
ishirini tu. Ni Mungu gani aliye kiziwi na kipofu asiye sikia na kuyaona malalamiko haya ya yatima na wajane? Mungu
wetu aliye hai “hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane
amwelezapo habari zake,” YbS 35:14. Ndugu yangu, ukunapo kitambi hicho cha
dhuluma, kumbumbu ‘ukimya hai’ huu wa Mungu juu ya yatima na wajane unao
wadhulumu.
Mayatima na wajane
katika sintofahamu zao, na hasa pale wanapokosa watetezi wao katika kweli na
haki, Mungu husadifu unyenyekevu wao, hasa pale wanapoyakabidhi yote mbele yake
bila kujibakiza. Na hii ndiyo sala yake mnyenyekevu ambayo, “hupenya mawingu, wala haitatulia hata
itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa
adili, akatekeleza hukumu,” YbS 35:17-18. Ndugu yangu, ingawa vyote ni chakula,
siyo kwamba vyote vyalika kwa nyakati zote. Hivyo tumwogope Mungu tunapo
wadhulumu yatima na wajane. Na kama ushadumbukia katika mtego huu, tafakari hii
ikuamshe uielekee huruma ya Mungu kwa kufanya toba ya kweli na majuto.
Injili yetu ya leo
yatufundisha namna ya kufanya toba ya kweli na mkao wetu mbele ya Mungu kwenye
kiti cha Huruma na Msamaha. Ndugu yangu, tuwapo mbele ya Kiti cha huruma na
msamaha wa Mungu, Yeye haitaji historia ya mema yetu tufanyayo kwa sababu wema
na uzuri ni hali na mali ya Mungu. Haitaji kusikia ubaya wa wengine, ila makosa
yako. Mfarisayo anatoa historia ya mazuri yake na namna afanyavyo mfunga wake.
“Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi,
wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa
juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote,” Lk 18:11-12.
Ndugu yangu, mbele za
Mungu hatujihesabii haki, bali tunapewa haki baada ya kufanya yampendezayo
Mungu. Tunachohitaji mbele ya Mungu ni huruma na msamaha wake. Tukiwa mbele ya kiti hiki cha huruma ya
Mungu, hatufanyi malinganisho ya dhambi wala uhalalishaji wa dhambi, ila makosa
yetu tuliyoyafanya kwa kujua au kutokujua. Labda nitoe mfano: Huwezi kwenda
kuungama na kusema hivi; “nimechukua pesa ya mume wangu na kulipa zaka kwa
sababu yeye hapendi kulipa zaka.” Kosa la wizi lipo pale pale, licha ya kwamba
nia yako ilikuwa nzuri, yaani, kulipa zaka kwa niaba ya mume wako. Njia mbovu
na ovu, haziwezi kamwe kuhalalisha tendo lolote lile hata kama malengo yake ni
mazuri.
Mfano wa kuigwa ni wa
Mtoza ushuru. Mtoza ushuru anajiachia kwenye kiti hiki cha huruma na msamaha wa
Mungu kama alivyo na kama alivyoyatenda makosa yake. “Ee Mungu, uniwie radhi
mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa maneno haya yanatosha kupewa thawabu na
kuinuliwa katika hali yake ya unyonge iliyotokana na dhambi zake. Mtoza ushuru
alikuwa amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho
yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani mwake. Hii ndiyo toba ya kweli na
aibu juu ya dhambi. Tunachoitaji ni uponyaji wa mwili na roho. Mponyaji wetu ni
Mungu anayejua makandokando yetu yote. Kamwe tusione aibu kuziungama dhambi
zetu, na tena kwa uwazi kabisa.
Ndugu yangu, mara nyingine
twaona baadhi ya dhambi zetu ni kubwa sana, na mbele ya kiti hiki cha huruma na
msamaha, tunaishia kusema na “nyingine nilizosahau,” ili hali tunajua
hatujazisahau. Huku ni kuchezea kiti hiki cha huruma ya Mungu na msamaha, na
zaidi, kumkufuru Roho Mtakatifu. “Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa
Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10.
Hakuna dhambi kubwa ambayo mbele ya Mungu ambayo atashindwa kukusamehe, na
hakuna dhambi ndogo mbele ya Mungu ambayo hata ichukulia maanani. Ikiwa dhambi
ni ukosefu wa kutenda mema na kwenda kinyume cha upendo wa Mungu, basi hakuna
uzito wa dhambi kubwa wala ndogo mbele ya Mungu kwa kusamehe. Tuziungame zote
bila aibu.
Kwa kuziungama dhambi
hizo kama alivyofanya Mtoza ushuru, tunahesabiwa haki, na kukwezwa mbele za
Mungu. “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko
yule (Mfarisayo); kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye
atakwezwa,” Lk 18:14.
Ndugu yangu, mali yako
halali mbele ya Mungu ni dhambi zako. Vingine vyote ni mali na uzuri wa Mungu.
Kuviishi kwa amani na uhuru alivyokupa Mungu kama sehemu ya uzuri wake,
yatupasa kusalimisha mali yetu halali kwake, yaani dhambi zetu. Twende muda na
wakati wo wote kupatanishwa naye kwenye kiti chake hiki cha Huruma, Msamaha na
Upendo.
Ndugu yangu, chuma kinapoitwa “Iron Still,” kimepita
katika moto mkali sana. Uimara wa chuma hiki
ni tokeo la chuma hicho kuvumilia joto hilo kali bila kupoteza uhasilia wake.
Mitume, na hasa Petro na Paulo ambao leo Mama Kanisa anawasherekea, walitaabika
vya kutosha kuhusu jina la Yesu. Somo la Pili linaeleza kwa undani mahangaiko
na taabu alizozipata Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema kama ni vita ameishinda
na mwendo ameumaliza. “Nimevipiga
vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim 4:7. Faida
kubwa aliyoipata katika utume wake huo wa pekee ni kuilinda Imani ambayo si kwa
faida yake mwenyewe, bali kwa Kanisa zima. Msingi wa maisha ya Mtume Paulo ni
kauli mbiu yake hii: “kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni
faida.” Flp 1:21. Hii ni hatua ya juu kabisa kwa mfuasi wa Kristo. Hapa ni
kuishi kile unachokiamini na kukubali kuyapata yote kutokana na imani hiyo.
Wapendwa wana wa Mungu,
hatua aliyoifikia mtume Paulo ni hatua ya kutokutishika na jambo lolote. Ni
hatua ya kuishinda hofu na kuukumbatia uzima wa milele ingawa tunajua wote
lazima tutakufa. Ni kujiachia katika mikoni ya Kristo, na kuacha yeye atende
kadiri apendavyo. Ni kutokuwa na shaka yoyote juu ya: sababu ya kuja kwake Yesu
Kristo kwetu, kuteseka kwake, kusulubiwa kwake, kifo chake na ufufuko wake.
Mtume Paulo analiweka fumbo hili kwa maneno haya: “Bwana ataniokoa
na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu
una Yeye milele na milele. Amina,” 2Tim 4:18. Je, ninaweza kuyatamka maneno
haya bila hofu yoyote ninapokabiliwa na changamoto za maisha yangu ya kila
siku? Ndugu yangu Utume si lelemama, bali kuvumilia hadi ushindi, yaani,
kuyafikia maisha yale ya milele.
Jumanne Ngawira
alifanikiwa sana katika shughuli zake za biashara kutokana na ujanja ujanja
wake wa kupiga madili na hata kuwadhulumu wengine. Na kwa vile pesa alikuwa
nayo, aliweza kuwahonga wale wote ambao aliona kwake ni kizuizi cha kuyafikia
malengo yake.
Kwa vile Mungu siyo Edgar
wala Abdalah, siku zilipofika ‘Bilionea’ huyu alifarika na kuzima kwa fahari
sana. Jeneza lake lilipambwa kwa vito vya gharama, huku likiwekewa kiyoyozi, na
ndani yake walimwenge simu ya kiwango, ikiwa na chaji na vocha ya kutosha. Je,
huko mbinguni ukweli wa mambo uko vipi?
Mara Jumanne Ngawira
alizinduka na kujikuta yupo mbele ya mavazi ya aina mbili, yaani, kanzu nyeupe
na nyingine kuukuu hivi ya kahawiya. Na mara akasikia sauti ikiita, “Maria
chukua kanzu hiyo nyeupe uvae na uelekee mkono wako wa kulia kwenye lango lile
jembamba.”
Kutokana na uzoefu wake
Jumanne Ngawira wa madili na ujanja ujanja, na alipoona Maria hatokezei, mara
akaichukua ile kanzu nyeupe na kuivaa, na kuelekea kwenye lango lile jembamba,
kwani hadithi hizi alizisikia sana angali duniani, na leo imekuwa kweli.
Akajisemea moyo, “kutesa hadi mbinguni! Kufika kwenye lango lile jembamba
alikutana na malaika, naye alimruhusu kuingia mbinguni.
Mara tu baada ya
kuingia alijisikia baridi sana, na kuanza kushindwa kupumua kwani hewa haikumtosha
ingawa watu wengi waliokuwa wakiimba na kucheza, walionekana kuifurahia hali
ile bila tatizo lolote wakiwa na mavazi yao meupe.
Ili kuyanusuru maisha
yake aliutafuta mlango ule alioingilia ili atoka mara. Akiwa katika hali ya
sintofahamu, alikutana na malaika mlinzi wa lango lile na kumwongoza hadi nje.
Akiwa nje huku akifurahia hali ya hewa nzuri na joto la kutosha, alimwona Binti
mmoja mzuri na mara alisikia sauti, “Jumanne Ngawira, livue vazi hilo na umpe
Binti huyo Maria, nawe uvae vazi lako lililopo mkono wako wa kushoto.”
Baada ya kulivaa vazi
lile, alisikia tena sauti ikimwambia, “sasa ifuate njia hiyo pana upande wa
kushoto kuelekea lango lile kubwa mbele yako. Huko ndiko kwenye kilio na kusaga
meno, na hayo ndiyo makazi yako ya milele uliyoyaanda kwa miaka yote niliyokupa
ungali duniani.”
Ndugu yangu, madili
yako unayoyafanya, na ujanja ujanja wako ni hapa duniani tu. Hata hivyo Mungu
wetu aliye huruma na upendo bado anakupa nafasi ya kubadili mwenendo mzima wa
maisha yako leo na sasa ungali hai huku ukiipumua pumzi yake. Tafakari na
chukua hatua. Wakati ndiyo sasa!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala
hakijali cheo cha mtu,” YbS 35:12
Tusali:-Ee
Yesu, niongoze katika njia ya kweli na haki siku zote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario