ALHAMISI WIKI YA 28 YA MWAKA-C
Somo:
Efe 1:1-10
Zab/Kit: 98:1, 2-3ab, 3cd-4, 5-6
Injili: Lk 11:47-54
Nukuu:
“Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa
Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo,” Efe 1:2
“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao
ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake,” Efe 1:7
“tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria,
aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa
kizazi hiki,” Lk 11:51
“Ole wenu, enyi
wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale
waliokuwa wakiingia mmewazuia,” Lk 11:52
TAFAKARI:
“Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu
Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Mafarisayo na Wana-sheria waliishi kweli ya Mungu waliyoipindisha kwa manufaa
yao wenyewe. Waliukataa ukweli na maarifa ya kumjua Mungu katika kweli na haki.
Tendo hili ni sawa na kukataa ufunguo wa kweli na uzima. Mpendwa unayesafiri
nami katika tafakari hii, njia ya kweli leo katika maisha yako ya kiroho ni
Kristo Yesu Mwenyewe. Kristo Yesu ni kweli tuipasayo kuichuchumilia kwa gharama
zote. Na mwisho, uzima wa kweli upo kwa
Kristo Yesu Mwenyewe.
Kwa mankiti hii Yesu haoni haya
kuwakaripia Mafarisayo na Wana-sheria kuhusu ukweli huu. Naye anasema, “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa
maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia,” Lk 11:52.
Ufunguo wa maarifa na kweli kuhusu siri ya Mbinguni upo kwa Kristo Yesu peke
yake. Hivyo kuijua siri hii yatupasa kuishi ndani na katika Kristo. Hakuna
ufunuo wa Mungu ulio wa wazi zaidi ya Kristo Yesu.
Na
kama tunautaka ukweli juu ya uzima wa milele yatupasa kwenda kwake Yesu. Kama
wataka kuijua njia ya uzima wa milele yakupasa kwenda kwa Kristo Yesu. Na kama
wautaka uzima ndani yako nenda kwa Kristo Yesu. Mambo haya yote matatu Yesu
Kristo mwenyewe kesha tuhakikishia. Naye anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli,
na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi,
mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona,” Yoh 14:6-7.
Ndugu
yangu, bila Kristo Yesu hutoweza kufanya lolote lile, lile kubwa au dogo. Kwa
jambo hili, Yesu anakuambia wewe na mimi
kwamba, “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake,
huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh
15:5. Kumbe salama yako na yangu ni kuwa ndani na katika Kristo Yesu.
Ujumbe
wa Mtume Paulo kwetu leo unasisitiza nafasi hiyo ya Kristo Yesu ndani ya maisha
yetu. Na katika hili anasema, “Neema na iwe kwenu na amani
zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo,” Efe 1:2. Kumbe neema na
amani asili yake ni Mfalme huyu wa Amani, yaani, Yesu Kristo. Nasi kama wafuasi
wake Kristo ni wajumbe na vyombo vya amani hiyo ya Kristo kama pia asemavyo
Mtakatifu Fransisco wa Assis katika sala yake ile, “Ee, Bwana unifanye chombo
cha amani yako...” Hivyo ndugu yangu, ni “katika yeye huyo (Kristo Yesu), kwa
damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema
yake,” Efe 1:7.
Wapendwa katika Kristo,
zaidi ya kuwa vyombo vya amani yake Kristo pale tulipo, mimi na wewe ni vyema
tukatambua kwamba tumekombolewa kwa damu yenye thamani kubwa sana kama asemavyo
Mtume Petro, “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa
fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba
zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na
waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hivyo kama mimi ni Mbatizwa yanipasa
kuthamini ubatizo wangu, kuulinda, na kuishi kwa uaminifu ahadi zangu za
Ubatizo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Katika yeye huyo, kwa damu yake,
tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake,” Efe
1:7
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tufanye vyombo vya amani yako pale tulipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario