ALHAMISI WIKI YA 30 YA MWAKA-C
Somo:
Efe 6:10-20
Zab/Kit: 144:1, 2, 9-10
Injili: Lk 13:31-35
Nukuu:
“Vaeni silaha zote za
Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani,” Efe 6:11
“Kwa maana kushindana
kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya
wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho,”
Efe 6:12
“Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha
walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode
anataka kukuua,” Lk 13:31
“Akawaambia,
Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya
wagonjwa, siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32
“Pamoja
na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa
haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu,” Lk 13:33
TAFAKARI:
Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Mwana falsafa Spinoza aliwahi kusema “kifo hakiwezi kuepukika. Ni
lazima tutakukufa. Kinachotusumbua ni hofu kuhusu kifo. Hivyo yatupasa
kuishinda hofu. Na hivyo ni vizuri kufikiri kuhusu uhai.” Mpendwa, je wamwamini
Kristo Yesu? Kama unamwamini Kristo Yesu hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu
kifo. Kristo Yesu kwa maisha yake, mateso, kifo, na ufufuko wake ni jibu kuhusu
aina zote za uovu na kifo. Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu kama wafuasi wake.
Kristo Yesu ametupatia mfano na jibu kwamba hakuna uovu wowote unaoweza kudumu
katika umilele wake. Yesu haogopi vitisho wala kifo.
Yesu
anapoambiwa aondoke kwa kuwa Herode anataka kumuua aliwajibu, “Nendeni,
mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa,
siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32. Mnyama huyu Mbweha alitafsiriwa kama mtu
asiye na msimamo, kigeugeu na mwongo. Kristo
hawezi kutishiwa na mtu wa hali hii na kuacha kutoa huduma kwa watu ikiwa ndiyo
sababu na mpango kazi wake kwa watu wote. Ni kwa kupitia Kristo “vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye
ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa
habari njema,” Mt 11:5. Kristo pia anaufunua Utukufu wake mara baada ya
kuushinda uovu anaposema, ‘siku ya tatu nakamilika.’
Mateso
tunayoyapata leo au tuliyokwisha yapata kupia wazazi wetu, siyo kwamba historia
hiyo ya uovu Mungu haioni. Wakati utimiapo vyote vitafanywa upya. Yesu
anapoutazama mji wa Yerusalemu anayakumbuka na kuyaona mateso na uovu wa
manabii wake waliyofanyiwa na kusema, “Ee
Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako,
mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo
vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka,” Lk 13:34. Huu kwetu ni wito wa kuongoka na kuacha njia zetu
mbaya na kujisalimisha kwa Kristo. Tusisubiri hadi siku ya Mwisho kwani
hatutakuwa na muda tena wa kujisalimisha kwake. Utakuwa muda wa kupokea ukumu
yetu kila mmoja kadiri ya matendo yake na livyotenda. Yesu anasema, “Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami
nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina
la Bwana,” Lk 13:35. Je, kuna sababu ya kusubiri hadi siku ya mwisho? Ndugu
yangu natuanze kuishi maisha ya ufufuko kabla ya kuja kwake Bwana wetu Yesu
Kristo.
Maisha
baada ya ufufuko ni maisha yaliyokamili. Tunayaishi maisha haya ya ufufuko kwa
kuhesabiwa haki na kwa kuzaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu. Hivyo “si kwa sababu ya
matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa
kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia
ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili
tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele,
kama lilivyo tumaini letu,” Tit 3:5-7. Je, una sababu yoyote ya kuwa na hofu
juu ya maisha yako ukiwa na Kristo?
Ndugu yangu tunaye
safiri sote katika tafakari hii, ni vyema ukafahamu kweli hii kwamba kwa wewe
kuwa mfuasi wa Kristo ni uchaguzi uliyofanya dhidi ya giza, yaani, vita dhidi
ya uovu. Ushuhuda ya maisha ya imani yako leo na sasa na hadi siku yako ya
mwisho hapa duniani ni kuifia kweli na haki dhidi ya uovu na dhuluma. Hivyo
katika vita hii mimi na wewe tulio Wakristo hai kwa kuishi kwa uaminifu ahadi
zetu za ubatizo, yatupasa kuvaa “silaha zote za Mungu, tupate kuweza kuzipinga
hila za Shetani,” Efe 6:11. Vita hii si lelemama. Yatupasa kusimama imara
daima. Na tushindapo vita hii siyo kwamba shetani kaghairi, bali utuacha kwa
muda tu, Lk 4:13
Ukweli ni kwamba, vita
hii “si juu ya damu na nyama; bali ni
juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya
katika ulimwengu wa roho,” Efe 6:12. Ni vita ya kiroho, nayo yatupasa kujiandaa
kupambana kiroho. Kuishinda vita hii yakupasa kuwa na haya yafuatayo; Amani ya
ndani na yenye kuneemeshwa na Injili, Imani thabiti, na Nguvu ya Roho
Mtakatifu. “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya
haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya
yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye
moto ya yule mwovu,” Efe 6:14-16.
Vita hii inahitaji
ujari, tena wa kujitoa bila kujibakiza. Na wokovu ikiwa ndiyo kushinda kwake ni
kuvumilia hadi mwisho. Yawezekana twapambana kila siku na kwa bidii zote lakini
matokeo yake ni kwamba afadhali ya jana kuliko leo na huko tuendapo. Katika
hali na mazingira haya Yesu anatuambia hivi;
“Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini
mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22. Ndugu yangu, penye
mateso makali ndipo penye ukaribu wa furaha ile tuitumainiyo, yaani, utukufu.
Nguvu na faraja yetu na
Roho yule wa Bwana, yaani, Roho Mtakatifu. Huyu ndiye atutiaye nguvu na
kutufariji hasa pale tunapokumbana na sintofahamu zilizozidi ufahamu wetu. Naye
Yesu katika hali na mazingira haya ya sintofahamu zilizozidi ufahamu wetu
anatukumusha jambo hili la msingi juu ya Roho Mtakatifu kwamba, “Lakini hapo
watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile
mtakayosema,” Mt 10:19. Tusipoteze muda mwingi kujitetea kwa yale yasiyo na
kweli ndani yake na kuacha kusimama katika kweli na haki.
Kama jumuiya ya wenye
hofu ya Mungu, yaani, familia, jumuiya ndogo ndogo ya Kikristo, au Kanisa
mahalia, Mtume Paulo anatuambia, tupokee “chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho
ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika
Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote,” Efe
6:17-18. Kudumu katika sala ndiko tuchotapo nguvu ya kupambamba na vita hivi
vya kiroho, yaani, aina zote za uovu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nendeni, mkamwambie
yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu
nakamilika,” Lk 13:32
Tusali:-Ee Yesu,
uliyeshinda vita dhidi ya uovu, tujali nguvu na imani thabiti kupigana bila
kuchoka dhidi ya uovu katika jamii yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario