viernes, 14 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 28 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 28 YA MWAKA-C

Somo: Efe 1:15-23

Zab/Kit: 8:2-3a, 4-5, 6-7

Injili: Lk 12:8-12

Nukuu:

“Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu,” Efe 1:15-16

“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeyé,” Efe 1:17

 “Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu,” Lk 12:8-9

 “Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema,” Lk 12:11-12

TAFAKARI: “Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.”

Wapendwa wana wa Mungu, hatuna kitu chochote cha kumficha Mungu wetu. Mungu kesha tupatia namna ya kumfikia kwa kupitia uwepo wa Mwanaye Yesu Kristo. Yesu ananiambia mimi na wewe leo na sasa kwamba, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Je, ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii wasadiki maneno hayo ya Yesu Kristo? Kusadiki maneno haya ya Kristo Yesu ni kukiri kwamba katika maisha ninayoishi leo na sasa Yesu Kristo yupo hai ndani yangu, na kwa wale wote wanaonizunguka.

Nisipolifanya jambo hili nisijeshangaa siku ya mwisho napishana na Kristo Yesu katika maana ya kutokunitambua mbele ya Baba yake wa Mbinguni. Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu,” Lk 12:8. Ukiri wangu katika maisha na ushuhuda mbele za watu, ndiyo salama yangu mbele ya Mungu.

Kinyume chake ni kwamba, na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu,” Lk 12:9. Inasikitisha kwamba wapo miongoni mwetu ambao watakanwa milele kwa vile tu walishindwa kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao na kuuishi ukweli huo kwa Imani iliyo hai. Wakati mwingine matatizo yako yanaweza kuwa sababu ya kutokuona uwepo wa Mungu na hali hiyo ikakufanya ukate tamaa kabisa. Je, kunasababu ya kukata tamaa tukifikiri kuwa Mungu ametuacha?

Ukimya wa Mungu juu ya matatizo yako siyo kwamba haoni wala hajali. Mungu anajua ni wakati gani unaofaa kukupa kile anachoona kitakufaa katika maisha yako ya umilele. Hivyo Mungu hawezi kukusahau kabisa kwasababu alikuumba kwa sura na mfano wake, na anampango madhubuti na maisha yako. Yesu anatuamba, “lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote,”Mt 10:30. USIOGOPE hasa pale mambo yanapoanza kwenda ndivyo sivyo. Huo nao ni mtihani wa imani yako. Mungu anajua utashinda tu ukimtumainia.

Mungu utuwazia mema kila wakati. Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11. Ndugu yangu huna sababu ya kukata tamaa. Kukata tamaa katika maisha ni kosa kubwa sana kulifanya kama unaishi kwa malengo. Kosa hili au dhambi hii ni kumkufuru Roho Mtakatifu.

Kwa tendo hili, yaani, kukata tamaa hatuwezi kupata msamaha wake. Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10. Je, ni mara ngapi nimemkufuru Roho Mtakatifu kwa kukata tamaa? Roho Mtakatifu utuondolea mifadhahiko yote hasa pale tunaposhindwa kujitetea kutokana na mazingira yetu, hali zetu, na ubinadamu wetu.

Tunapokuwa na Roho Mtakatifu, huyatakatifuza yote na kuyafanya mapya na yenye nguvu. HivyoYesu anatuambia, “msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema,” Lk 12:11b-12. Je, naitaji silaha gani zaidi ya kiroho kumshinda Roho Mtakatifu?

Kusimama imara katika imani kunakupa furaha ya ndani ambayo hakuna mtu wa kukuondolea, Yoh 16:22. Nasi kama wafuasi wake Kristo Yesu tunayofuraha kwa sababu Kristo ni mshindi na ushindi huo umekwisha jidhihirisha katika tendo lile la ufufuko. Hivyo ufuasi wetu kwake siyo wa kubabaisha au kujaribu jaribu. “Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu,” Efe 1:15-16. Mtume Paulo haoni haya kuisema furaha ile iliyoko ndani ya moyo wake ndani na katika Kristo Yesu.

Hatuna tena shaka yoyote ile ya kumfikia Baba Yetu aliye mbinguni kwa sababu Kristo Yesu kesha tuonyesha njia hiyo ambayo ndiyo Yeye Mwenyewe. Kesha tuonyesha kweli ikiwa Yeye Mwenyewe ndiyo Kweli hiyo, yaani, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1. Naye ndiye uzima wetu tunaposhiriki Sakramenti Takatifu katika stahili yake. Ekaristi Takatifu ndiyo kelelezo cha uzima huo tunaposhiriki pasipo hatia. “Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele,” Yoh 6:55-56, 58.

Ndani na katika Kristo Yesu tunapata roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Mungu Baba aliyejifua wazi kwa njia ya Neno wake kufanyika mwili na kukaa kwetu (Yoh 1:14, Ebr 11:1, Gal 4:4-5), yaani, Yesu Kristo. Hivyo, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeyé,” Efe 1:17. Na katika Kristo Yesu twatiwa nuru na tumaini la kweli. “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo,” Efe 1:18. Kumbe ndani ya ulinzi wa Bwana wetu Yesu Kristo hakuna tunachopoteza, zaidi ya kuhakikishiwa uzima ule wa milele.

Kwa hiyo kama mfuasi wake Kristo, yanipasa kuamini pasipo shaka ndani na katika Kristo Yesu. Ni kwa maana hivyo kwamba, “ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake,” Efe 1:19. Hivyo matendo yangu yaakisi ukweli ule wa Yesu ndani yangu. Mateso, kifo, na ufufuko wake Kristo ni uthibitisho dhahiri kuwa vita dhidi ya uovu haina nguvu tena.

Kwa ushindi wake Kristo, Mungu Baba kesha “vitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:22-23. Kanisa Takatifu leo ndio chombo wazi na Sakramenti hai ya wokovu wetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema,” Lk 12:12a

Tusali:-Ee Yesu, tujalie uthabiti katika imani, na kusimama katika kweli na haki. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario