domingo, 9 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 28 YA MWAKA-C


JUMANNE WIKI YA 28 YA MWAKA-C

Somo: Gal 4:31b-5:6

Zab/Kit: 119:41, 44, 45, 47, 48

Injili: Lk 11:37-41

Nukuu:

“Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno,” Gal 5:2

 “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo,” Gal 5:6

 “Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu,” Lk 11:39

 “Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” Lk 11:41

TAFAKARI: “Toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, maneno haya ya Yesu, “toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” yanatutaka tujue ni kipi hasa kimtiacho mtu unajisi. Mara nyingi tunapoteza muda wetu mwingi kwa kutazama mambo ya nje na kusahau yale ya ndani ambayo kwayo hubeba kile ulicho. Katika kweli hii, Yesu anakuambia wewe na mimi, “Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi,” Mk 7:18. Ukweli ni kwamba mambo ya nje hayamtii mtu unajisi kwayo kama yalivyo. Na mantiki ya hicho asemacho Yesu kipo hapa, kwamba, vyote alivyoviumba Mungu aliona vinafaa, na vyote vina malengo yake, Mdo 11:9. “Kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote,” Mk 7:19.

Kwa maana nyingine, “Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi,” Mk 7:20. Ndani ya mtu ndipo lilipo sanduku la hazina yake. Na ndani ya moyo wa mtu ndipo penye kiwanda cha kuzalisha mema au maovu. “Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu,” Mk 7:21-22. Haya ndiyo yanayomtia mtu unajisi, na yaliyo maovu yatoka ndani ya mtu, Mk 7:23. Ni katika mazingira haya Yesu anapenda tujue ni wapi kwa kuweka mkazo kama tunataka kukua kiroho.

Yesu alipokaribishwa nyumbani kwa mfarisayo mmoja alionekana akila bila ya kunawa mikono. Na “Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula,” Lk 11:38. Mafarisayo waliyapa mambo haya ya nje nafasi ya pekee sana. Lakini pamoja na kufanya hayo yote ndani ya mioyo yao walikuwa wakavu sana. Naye Yesu anawaambia, “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu,” Lk 11:39. Ni kama asemavyo Mzaburi kwamba, “kwa kinywa chao hubariki; kwa moyo wao hulaani,” Zab 62:4b. Hakika hili ndilo chukizo kwa Mungu, na maigizo kwa mwanadamu.

Yesu haachi kutukaripia katika maigizo haya tuyafanyao mbele za Baba yake wa Mbinguni. Naye anasema, “Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?” Lk 11:40. Huu ukinzani na mpasuko wa nafsi unatoka wapi? Na tunafanya hayo yote kwa faida ya nani, au kumfaidia nani? Kumbe ni muhimu sana kuwa makini na yale tuyatoayo ndani ya mioyo yetu. Mtakatifu Agustino anasema, “onja moyoni utamkayo mdomoni.” Na Yesu katika hili anatuambia,  “toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” Lk 11:41.

Haya mambo ya nje ndiyo anayoyakemea Mtume Paulo kwa jumuiya ile ya Galatia. Tendo la kutahiriwa lilibeba tafsiri kubwa sana kwa Wayahudi, Rej, Mwa 34:17, Yos 5:5, 8. Lakini Mtume Paulo anasema, “kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu,” 1Kor 7:19. Kumbe kuzishika kwa uaminifu amri za Mungu kwa sema zaidi kuliko mambo haya ya nje. “Basi ikiwa yeyé asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?” Rum 2:26. Wakati mwingine tunapoteza muda sana kwa haya ya nje na ya kibinadamu zaidi na yasiyo na utakatifu ndani yake.

Je, kutahiriwa kwa sema nini ndani na katika Kristo Yesu? Mtume Paulo anasema,  “mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno,” Gal 5:2b. Kwa maana nyingine Mtume Paulo anatuambia kwa kufanya hivyo tu (kutahiriwa) hakuna thawabu yoyote zaidi ya mambo ya kimwili na kiafya. Hakuna uhusiano wowote ule na swala zima la kiroho. Na katika hili (kutahiriwa), Mtume Paulo hapingi kama watu watafanya hivyo, ila kwa kufanya hivyo hakuna uhusiano wowote ule na swala la kiroho. Naye anasema, “Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote,” Gal 5:3. Ila angalizo lipo hapa: “Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema,” Gal 5:4. Matendo haya ya sheria, mfano, wa hili la kutahiriwa, ni ‘kweli ya Mungu iliyopotoshwa,’ linapohusishwa na swala la kiroho. Matendo hayo ya nje wakati mwingine ni mateso pasipo neema ndani yake.

Ndugu yangu tuyesafiri sote katika tafakari hii, mimi na wewe, “kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani,” Gal 5:5. Na kwa mantiki hiyo, “katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo,” Gal 5:6. Haya ya nje yasipoteze muda wako, na kuukosa Utakatifu ule ambao ndio cheo chako cha pekee.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani,” Gal 5:5

Tusali:-Ee Yesu na Mwalimu wetu, tujalie mwanga wa Roho wako tuyajue yale ya uzima wa milele. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario