JUMAMOSI WIKI YA 30 YA MWAKA-C
Somo:
Flp 1:18b-26
Zab/Kit: 42:2, 3, 5abc
Injili: Lk 14:1, 7-11
Nukuu:
“Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni
kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi,”
Flp 1:18b
“Kwa
maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21
“Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti
cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule
aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa
haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:8-9
“Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye
ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11
TAFAKARI:
“Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo katika somo la Injili Yesu anatupa angalizo hasa tunapoalikwa kwenye
tafrija mbalimbali. Tukizama ndani zaidi tunaona kwamba uhai tulionao na maisha
tunayoyaishi ni sawa na kualikwa kwenye furaha ya Mungu na Utukufu wake. Basi
ni vyema mimi na wewe kutambua duniani hapa tunapita tu, na tupo kwa maandalizi
ya maisha ya umilele. Yesu anatuwasa hivi kuhusu ukweli huu; “Ukialikwa
na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu
mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na
kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk
14:8-9.
Kama sote tumealikwa harusini ni wazi
tumepewa mastahili yaliyo sawa na yule aliyetualika. Basi yatupasa kujua kuwa
sote ni waalikwa na siyo ‘mgeni rasmi.’ Kwa utaratibu wa kawaida mbele
palipoandaliwa si mastahili yangu. Kumbe ni vyema na busara kutafuta nafasi
nyingine. Ili kuwa sehemu salama zaidi, Yesu anatuasa hivi; “Bali ukialikwa, nenda
ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu,
njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi
pamoja nawe,” Lk 14:10. Huku ndiko kwa maneno mengine kupungua ili Mungu awe na
nafasi juu ya maisha yako.
Ndugu yangu unaye
safiri nami katika tafakari hii utakubaliana nami kwamba kati yetu kwa nafasi
tulizokuwa nazo na madaraka tuliyonayo yaliyopitiliza hututia upofu na
kutufanya kuwa ndiyo fimbo ya kuchapia wengine. Jeuri hii ndugu yangu tunaipata
wapi wakati Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Siku
za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi
chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10.
Jinyenyekeshe basi na kuwa kile Mungu alichokusudia katika maisha yako.
Mfano
mzuri wa unyenyekevu huu tunaupata kutoka somo letu la kwanza, na hasa juu ya
maisha ya Mtume Paulo. Paulo mara tu baada ya kuongoka kwake, dira ya maisha
yake yote ni kupungua ili Kristo aliye Njia, Kweli, na Uzima awe na nafasi juu
ya maisha yake. Na hii ndiyo njia sahihi ya kufuata kama waja na wana wa Mungu.
Na kauli mbiu ya Mtume Paulo ni hii; “Kwa maana kwangu mimi
kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21. Kwa mtazamo huu, Paulo hana cha
kujisifia wala kujikweza zaidi ya neema ile ya Mungu ifanyayo kazi ndani ya
maisha yake.
Mpendwa katika Kristo,
mimi na wewe yatupasa kupungua ili Kristo aongezeke kwa wanyonge, mayatima,
wajane, masikini, wafungwa, wagonjwa, waliokata tamaa, wanaoonewa kwa ajili ya
haki, wafiwa, wadhabi, wanaodhulumiwa, na wale wate walitengwa kwa kusimama
katika kweli na haki. Watu hawa ndio waliokuwa karibu na zaidi, marafiki wa
Yesu Kristo kama asemavyo mwenyewe kwamba, “sikuja kuwaita wenye haki, bali
wenye dhambi, wapate kutubu,” Lk 5:32. Leo mimi ninayepumua na kufurahia afya
njema nione wajibu huo mkubwa wa Kristo mbele yangu.
Na kwa kutambua wajibu
huo mkubwa na mwendelezo wa kazi ile ya wokovu wetu, ndani na katika Kristo
Yesu, nijue kwamba, “kwa njia zote,
ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo
nafurahi, naam, nami nitafurahi,” Flp 1:18b. Kama ilivyo kwamba hakuna
aliyekuwa masikini kwa kutoa kile alichonacho, vivyo hivyo hakuna atakayepoteza
muda wake kwa kulihubiri neno la Mungu kila siku, na zaidi kwa maisha yake ya
kumcha Mungu.
Tendo la kupeleka
habari njema kwa wengine, ni tendo la neema na baraka. Kuna furaha kubwa sana
kwa Mungu na Watakatifu wake siku moja ukiwa mbele ya Mungu, na mmoja kati ya
wale waliohesabiwa haki na Mungu kutoa ushuhuda juu yako kwamba, ‘utakatifu
wake ulitokana na kuijua siri hiyo ya mbinguni na kwa kumjua Mungu kupitia
wewe.’
Na hii ndiyo maana ya
maneno haya ya Paulo ambaye sasa kwa ajili ya Injili hakuna alichopoteza, anachopoteza,
na atakachopoteza. Naye anasema, “Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa
wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo;
kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa
uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika
mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu,” Flp 1:19-20.
Hakika Mtume Paulo katika hatua hii hana alichokibakiza kwa ajili yake
mwenyewe, yote kesha yakabidhi kwa Kristo Yesu na yeye Kristo ni yote katika
yote.
Hata hivyo, Mtume Paulo
anatupa leo angalizo, tena zito sana. Kamwe mimi na wewe tusijilinganishe na
yale tuyafanyayo, na kamwe kwayo kama yalivyo yasiwe ndiyo chanzo na mwisho wa
furaha yetu. Hilo likiwa ndilo lengo la maisha yako, basi ujue bado
hujajitambua na kutambua kusudi lako la kuumbwa na uwepo wako hapa duniani.
Hapa na pale unaweza kupewa pongezi na hata kupigiwa makofi. Lakini mara
uonavyo hivyo, usibaki na pongezi hizo na makofi hayo, bali mara mrudishie
Mungu sifa na shukrani hiyo, na kuwabariki wale wote waliotambua kweli hiyo
ndani yako, nawe uwe wa mwisho katika kundi hilo la stahili ya baraka hiyo. Ni
kwa maana hii Mtume Paulo anasema juu ya kuishi maisha yanayoongozwa na
malengo, kwamba, “ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi;
basi nitakalolichagua silitambui,” Flp 1:22.
Ndugu yangu, maisha
yako katika hali salama lazima yasukumwe na mambo mawili; kukaa na Kristo, na
kudumu katika huduma kwa ajili ya watu. Naye Mtume Paulo anasema hivi katika
kweli hii, “Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae
na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa
zaidi kwa ajili yenu,” Flp 1:23-24. Kumpenda Kristo na kuishi ndani na katika
Kristo Yesu kutakulazimu kutumika kwa ajili ya wengine, tena bila faida
binafsi.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa maana kila
ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
neema ya kudumu ndani na katika wewe tu kwa sababu kwako kuna furaha ya kweli.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario