JUMANNE WIKI YA 27 YA MWAKA-C
Somo:
Gal 1:13-24
Zab/Kit: 139:1-3, 13-14ab, 14c-15
Injili: Lk 10:38-42
Nukuu:
“Maana mmesikia habari
za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la
Mungu kupita kiasi, nikaliharibu,” Gal 1:13
“Nami naliendelea
katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu,
nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14
“Lakini Mungu,
aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,” Gal 1:15
“Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa
utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu
alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie,” Lk 10:40
“Bwana akajibu
akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi,”
Lk 10:41
“lakini kinatakiwa kitu
kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk
10:42
TAFAKARI:
“Jenga Urafiki na Kristo Yesu, na kaa naye daima. Kujisalimisha kwako kwa
Kristo kuna uzima wa milele.”
Wapendwa wana wa Mungu,
somo la Injili ya leo, Mariamu ndugu yake Martha
anajielewa na kumfahamu yule anayemtumikia aliye kweli katika yote, na mwisho
anajisalimisha kwake. Yawezekana mimi na wewe tumeyapa maisha yetu kipaumbele
chake cha kwanza katika kujishughulisha katika mambo mengi yasiyo na mwelekeo.
Maisha yetu hayajengwi kwa wingi wa vitu tunavyofanya, bali uelewa wa yale
tunayoyafanya, na kwa nini tunafanya kama tunavyoyafanya.
Martha
kama tulivyo wengi anajilinganisha na yale anayofanya na kukosa muda wa kujua
chanzo ya yale yote tunayoyafanya na kwa nini tunayafanya kwa namna hiyo, na ni
nani anayeyaratibisha. Martha anamlalamikia Yesu kwa nini Mariamu ndugu yake
hamsaidii. Yesu anamkumbusha Martha jambo la muhimu na kusema, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu
vingi,” Lk 10:41. Furaha yetu haitokani na vitu tunavyofanya. Kujishughulisha
huku katika maana ya kufanya hivyo tu, kutatuletea mfadhaiko mkubwa sana.
Maisha
yetu yanamaana kwanza kabisa tunapojitambua na mwisho kujisalimisha muda wote
kwa yule atupaye uzima wa milele. Huyu ndiye chanzo cha furaha yetu na umilele
wa maisha yetu. Kwake yatupasa kutumia muda mwingi naye. Huyu ndiye Kristo;
njia, ukweli, na uzima wetu, Yoh 14:6. Kuwa na Kristo ni kuchagua fungu lililo
jema ambalo kwalo hatuwezi ondolewa.
Ukweli
huu ndio Yesu anaomwambia Martha na sisi leo kwamba pamoja na yote tuyafanyayo,
“lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na
Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42. Kukaa
chini ya miguu ya Yesu ni ule utayari wa kulishwa neno la uzima, na kujazwa
ufahamu na kufunuliwa siri ya uzima wa milele.
Kujisalimisha
ndani na katika Kristo Yesu hukupa maana ya maisha yako. Mtume Paulo
anathibitisha kweli hiyo kwa kusema, “Sasa
nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili
wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani,
Kanisa lake,” Kol 1:24. Kristo ndiye uzima ule
uupiganiao kila siku. Na hii ndiyo siri iliyofichwa kwa wamchao Mungu, yaani
Watakatifu wake. Ni “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote
na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake,” Kol 1:26. Na
kwa siri hii, Mtume Paulo amefanywa ‘mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa
Mungu, aliyopewa kwa faida watu, akilitimize neno la Mungu,’ Kol 1:25.
Ndugu yangu, Kristo ndiyo njia ile sahihi unayoitafuta kila siku
na mara nyingine kupotea kabisa. Na Kristo ndiye kweli yenyewe kwa sababu ndiye
ufunuo wa kweli ya Mungu Baba. Ni katika kweli hii “ambayo
Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa Utukufu wa siri hii katika
Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la Utukufu,” Kol 1:27. Kumbe wito
wako na wangu kama wabatizwa na wafuasi wa Kristo walio hai kama asemavyo Mtume
Paulo ni “kuhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha
kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo,”
Kol 1:28. Na huu ndio ushuhuda wa kweli.
Wapendwa wana wa Mungu,
hatutaweza kutoa ushuhuda huu wa Mungu kama hatupo tayari kulishirikisha kwa
ukarimu neno la Mungu. Ushirikishaji huu wa Neno la Mungu kwa ukarimu tumeona
leo ukifanyika kwa vitendo kutoka kwa Mariamu kwa kujisalimisha chini ya miguu
ya Yesu, na kutoka kwa Mtume Paulo kwa kujitoa bila kujibakiza kwa Kanisa la
Kristo na watu wake.
Hata hivyo tutaweza tu
kulishirikisha neno la Mungu kwa ukarimu kama tutaweza kulitafakari kwa kina
Neno la Mungu. Kulitafakari kwa kina neno la Mungu kunahitaji utayari bila
shuruti wa kulipokea Neno la Mungu. Na tutaweza kulipokea Neno la Mungu bila
shuruti pale tu tutakapokuwa tayari kulisikia Neno la Mungu.
Mtume Paulo
anatufundisha tumaini la kweli pale tupatwapo na sintofahamu nyingi katika
maisha. Mtume Paulo hakuwa na historia nzuri katika maisha yake kabla ya
kuongoka. Bila shaka nawe pia ukiitazama historia yako na hayo yanayokutokea
leo unakata tamaa na kujihukumu kila kukicha. Tazama tumaini lililo mbele yako,
na hasa ukitazama historia ya Mtume Paulo na kuongoka kwake.
Katika hili, Mtume
Paulo mwenyewe anatusimulia kwa ufupi historia ya maisha yake. Naye anasema, “Mimi
ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji
huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi,
nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata
kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake,” Mdo 22:3.
Historia hii ya Mtume Paulo inasema chochote kuhusu hali na maisha yako?
Kama haitoshi, mtazame
Yesu pale msalabani, kwani kaubebe ujumbe mzito sana juu ya maisha yako. Kwa
kuwambwa kwake Msalabani anakuambia hivi; “ona nilivyo hapa. Nimeyafanya haya
yote kwa sababu na kupenda upeo.” Hakika hakuna sababu ya kujiona mnyonge na
mtu aliyetengwa ninapoutafakari Msalaba Mtakatifu. Kristo ndilo tumaini la
kweli, na Yeye ndiye njia, kweli, na uzima wetu, Yoh 14:6.
Mtume Paulo baada ya
kuongoka kwake, ikiwa ni msukumo wa moja kwa moja wa Kristo mwenyewe baada ya
kutupwa chini, Mdo 9:4-5, tumaini lake lote alilielekeza kwa Kristo Yesu. Naye
kwa kutoa ushuhuda wa kweli hiyo anasema, “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo
niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu,” Gal 1:11. Kwa
maneno mengine ni kwamba kile alicho na anachokihubiri Mtume Paulo siyo tokeo la nguvu zake au maarifa yake
binafsi, bali ni neema ya Kristo iliyo ndani yake.
“Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu (Injili hiyo) wala
sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo,” Gal 1:12. Mtume
Paulo hafichi historia yake mbaya na kuona aibu kuisema mbele za watu.
Mtume Paulo anataka
mimi na wewe tuelewe kwamba misimamo yetu iliyojengwa na inayojegwa na mila na
desturi zetu potofu, ndani yake hakuna uzima. Naye anasema, “Maana
mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba
naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu,” Gal 1:13. Ndugu yangu,
kama wewe ni mmoja wa kujipambanua kwa ubora wa kabila lako, misimamo ya kabila
lako isiyo na mwono wa Kimungu, na hata umaarufu wake, basi elewa haupo njia
sahihi kama wataka kuwa mfuasi wa Yesu.
Mtume Paulo anakuambia
wewe na mimi kwamba, “Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi
kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika
kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14. Hata kwa kufanya hayo yote, Mtume
Paulo anagundua hapakuwa na tumaini lolote, zaidi ya kupotea kwa misimamo isiyo
na mwelekeo wa Kimungu na kuikosa njia ile sahihi.
Wapendwa katika Kristo,
usipotambua uwepo wa Mungu katika maisha yake, chochote ujengacho juu yake
hukosa msingi imara, na mwisho wake uporomoka. Baada ya kuongoka kwake, Mtume
Paulo anagundua nguvu na uwepo wa Mungu katika maisha yake. “Mungu aliyenitenga tangu tumboni
mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,” Gal 1:15. Hivyo kile alicho Paulo
baada ya kuongoka kwake, yaani, kurudi katika njia iliyo sahihi, Kristo ndiye
kila kitu kwake.
Ni kwa sababu hiyo
Paulo anasema kwamba, Mungu “alipoona
vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake;
mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda
kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu
Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski,” Gal 1:16-17. Je, umeyapitia machungu na
mahangaiko kama Mtume Paulo?
Pamoja na kulihujumu
Kanisa la Kristo Yesu, Mtume Paulo hakuona haya kulijenga na kujumuika na
wenzake na kuwa sehemu ya mwili wa Kristo, yaani, Kanisa. Naye anasema, “Kisha,
baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa
kwake siku kumi na tano,” Gal 1:18. Tunakumbushwa pia kama wasemavyo waswahili
kwamba, ‘kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa ni kosa.’ Kwa mara ya kwanza
waweza kutenda kosa kwa kutokuwa na ufahamu kuhusu kile ukitendacho. Ila
kutenda kosa lilele ilhali una ufahamu nalo, kosa hili ujeuka na kuwa dhambi.
Kuongoka kwa Mtume
Paulo kunayabadili maisha yake yote kwa sababu kesha kutana na kweli ambayo
ndiye Kristo mwenyewe. Mtu mwingine anayeyagusa maisha yake huko Yerusalemu ni
Mtume Yakobo. Na hivi ndivyo ilivyokuwa; “Lakini sikumwona mtume mwingine, ila
Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu,
sisemi uongo,” Gal 1:19-20. Ukweli ndani na katika Kristo unamweka huru Mtume
Paulo, Yoh 8:32.
Kuchangamana kwake
Mtume Paulo na Wakristo wenzake hakukuwa rahisi kutokana na historia yake juu
ya Kanisa la Kristo aliyolitesa, na kumbukumbu walizobaki nazo vichwani mwao
Jumuiya ile ya kwanza ya Wakristo. Na katika kweli hii Mtume Paulo anasema, “sikujulikana
uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo,” Gal 1:22. Na sababu
ya kutokujulikana kwake kulitokana na matendo yake juu ya Jumuiya ya kwanza ya
Wakristo, na kuogopa pia kuuwawa na Wayahudi wenzake ambao kwas asa anaonekana
kama kuwasaliti.
Hata hivyo Wakristo wa
Uyahudi kama asemavyo Paulo, “wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo
kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani,” Gal 1:23. Na kwa neema
na tendo hilo “Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu (Paulo Mtume),” Gal 1:24.
Ndugu yangu, badili mwenendo wa maisha yako, na jenga urafiki na Kristo Yesu
kwa sababubu ndani na katika Kristo Yesu kuna uzima. Mariamu na Paulo Mtume
wameweza nawe na mimi tunaweza pia.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bwana akajibu akamwambia, Martha,
Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi,” Lk 10:41
Tusali:-Ee
Yesu na Mwokozi wangu, napenda daima kuwa rafiki yako. Niwezeshe hilo toka
ndani ya Moyo wangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario