sábado, 15 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 29 YA MWAKA-C



 

Somo I: Kut 17:8-13

Zab/Kit: 121:1-2, 3-4, 5-6, 7-8

Somo II: 2Tim 3:14-4:2

Injili: Lk 18:1-8

Nukuu

“Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda,” Kut 17:11

“Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa,” Kut 17:12

 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema,” 2Tim  3:16-17

 “lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho,” 2Tim 4:2

“Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa,” Lk 18:1

 “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?” Lk 18:7

“Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Lk 18:8

TAFAKARI: “Waweza kutoa bila kupenda, ila huwezi kupenda ukaacha kutoa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuumbwa kwetu wanadamu halikuwa hitaji la Mungu, bali kwa upendo wake alichakugua kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kwa hiyo lengo la kwanza la uumbaji wetu ni kuishi milele. Kwa tendo hili ni wazi kwamba lengo la pili la uumbaji wetu ni kuwa na mahusiano na Mungu na sisi kwa sisi. Mahusiano haya msingi wake ni upendo. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor 13:3. Kadhi kama tulivyosoma na kusikia Injili ya leo anampa mama mjane haki yake si kwa kupenda bali kwa kulazimika kutokana na usumbufu. Naye anasema, “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4b-5. Hivyo unaweza kutoa bila kupenda.

Tunapokuwa na mahusiano mazuri na Mungu kamwe hawezi kutuacha katika mahangaiko yetu. Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia uhakikisho huyo. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?” Lk 18:7. Uvumilivu wa Mungu kwetu ni Imani ile tuliyo nayo juu yake. Kwa imani thabiti tunauhakika kwa kuyapata yale tumwombayo Mungu wetu aliye huruma na upendo. Ukweli huu unajidhihirisha pia katika historia ya ukombozi wetu, kama  somo letu la kwanza linavyo simulia kisa kile cha wana wa Israeli na Waamaleki.

Kwa imani na matumaini makubwa waliyokuwa nayo Waisraeli chini ya uongozi wa Musa, Mungu haachi kutoa huruma yake kwa sababu aliwapenda. Musa ni kielelezo cha uvumilivu huo ambao Mungu anataka tuwe nao hasa katika mazingira yale ya sintofahamu. Hivyo “Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda,” Kut 17:11. Kwa upande mwingine hili ni jaribu la Mungu kwetu hasa pale tunapozingirwa na hali tatanishi. Lakini ukweli ni kwamba, pasipo njia Mungu huifanya njia. Hakuna jaribu lolote tulipatalo katika maisha Mungu akashindwa kutuonyesha njia ikiwa tutadumu katika uthabiti wa Imani. “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13. Na jaribu alilolipata Musa ni mikono yake kuwa mizito ilhali walitegemea ushindi kutoka kwa watesi wao-Waamaleki.

Tendo la kuishusha mikono yake ilimaanisha kushindwa, na walizidiwa nguvu na Waamaleki. “Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa,” Kut 17:12. Na walipodumu katika jaribu hili Mungu alifungua neema na baraka zake. Na ndipo  “Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga,” Kut 17:13. Imani ya kweli hujaribiwa. Na lengo la jaribu ni kuimarisha imani hiyo ile kesho uwe shuhuda na shahidi kwa wengine walio na imani haba.

Yesu anatupa pia uhakika wa jambo hili, ila imani ni moja ya kielelezo kikuu kwa kile tuombacho. Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Lk 18:8. Je, unayoimani kwa hayo uyaombayo?

 Kwa upande mwingine uwezi kupenda bila kutoa. Yesu anasema, “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:11. Yesu kwa kutupenda yupo tayari kutua uhai wake kwaajili yetu. Upendo ndiyo amri yenyewe. Kristo ndiye kielelezo chetu juu ya upendo na kupenda. Hili ndilo lile neno lililofanyika mwili nalo likakaa kwetu.

Wapendwa wana wa Mungu, Ufalme wa Kristo ni tokeo la Yeye mwenyewe kujitoa msalabani kwa hiari, awe sadaka safi iletayo amani, ili atimize mafumbo ya ukombozi wa watu. Naye Yesu anasema hivi juu ya utayari wake katika kujitoa, Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu,” Yoh 10:18.  Hakika hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Ni Yesu tu na wale wote aliowaridhia.

Ufalme wa Kristo na sifa zake, yaani, ‘ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, amani na mapendo’ ni kinyume kabisa na ulimwengu wenye kufurahia ‘uovu,’ na mbaya kabisa pale mwanadamu kwa kulijua hili ni ‘ovu’ anakufa ganzi, na kutokufanya chochote. Kufa ganzi huku ni moja ya dalili ya kifo cha ile dhamiri hai ndani ya mtu. Na hapa ndipo leo tunaposema kwamba watu siyo kwamba tu hawana imani, bali hawataki kusikia kabisa habari za Mungu na habari njema.

Ni wazi kabisa kwa hali hii yeyote yule atakaye ishi ufalme wa Kristo, katika maana ya maisha ya utauwa, awe tayari kuudhiwa. Ni vita kati ya mwanga na giza. Ni katika mazingira haya Mtume Paulo anasema, “wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa,” 2Tim 3:12. Leo kuwa Mkristo kweli kweli, yakupasa kujipambanua vizuri. Jamii yetu ya leo kila kona wafikiri na kuishi kwa ‘dilidili.’ Ni maisha ya ujanjaujanja yasiyo na kweli ndani yake. Huu ni uthibitisho pia wa kufa ganzi kwa miimili ya dola. Hali ya ‘udiliudili na ujanjaujanja’ inapoikumba miimili ya dola, sumu ile ushuka hadi mtu wa chini kabisa, yaani akina siye ‘maisha heri ya jana,’ akina kabwela na kapuku. Je, tukubaliane na hali hiyo na kuutupilia mbali ufalme wa Kristo, yaani, kuishi maisha ya utauwa? La hasha!

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba, kwenye dhiki nyingi, sintofahamu nyingi, na miingiliano isiyo na utarajibu katika masiha, ndiyo mwisho na mwanzo wa tumaini jipya na lenye heri. Kinachotakiwa ni kusimama katika kweli, haki, mapendo, na amani bila kupoteza tumaini ile lililo mbele. Katika ukweli huu Mtume Paulo anatushuhudia kwamba, “kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote,” 2Tim 3:11b. Mtume Paulo anamtaka Timotheo na sisi leo kutokupoteza tumaini juu ya Yesu Kristo. Yesu naye anatuambia, Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mk 13:13. Kuishi maisha ya utauwa ni kuliishi jina la Yesu, ambalo kwalo ulimwengu utatuchukia ila tumaini halitaondolewa kwetu.

Ndugu yangu,watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika,” 2Tim 3:13. Kuendelea kwao sio kwamba Mungu hana nguvu tena, Zab 77:7-9, bali tukumbuke kuwa Mungu ni Upendo, Subira, Huruma, na Msamaha. Yupo tayari kuanza upya na yeyote yule ilimradi tu aiache njia yake ovu, Isa 55:7. Je, tabia hii ya Mungu inakukwaza? La hasha! Yanibidi kufanya iliyo sehemu yangu kwa nguvu na ukamilifu wote. Katika hali hii, Mtume Paulo anamuasa Timotheo, na sisi pia kwamba, ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu,” 2Tim 3:14-15. Na kama huyafahamu Maandiko Matakatifu, huu ni wakati wa kuyatafakari. 

Neno la Mungu ni uzima wetu. Ni kwa namna hiyo, Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema,” 2Tim 3:16-17. Kristo hukaa ndani yetu nasi ndani yake tulishikapo neno lake, Lk 11:28. Na hakuna mauti tulishikapo neno la Bwana. “Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele,” Yoh 8:51. Je, waamini hilo?

Ni vyema mtu ajue vizuri kile akiaminicho, na siyo kukimeza tu bila kukicheua. Usipo kijua vizuri kile ukiaminicho ni vigumu pia kukitetea au kuwa sehemu ya maisha yako. Mtume Paulo anampa angalizo Timotheo, ambalo leo tungelihusiha na utoaji wa Katekesi ya kina. Naye anasema,lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho,” 2Tim 4:2. Tusipo jali leo kuwapa waamini katekesi ya kina juu ya imani ya kweli, muda si mrefu nasi tutakumbana na hiki kinachoendelea katika Kanisa la Magharibi-kutokuamini uwepo wa Mungu. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo,” 2Tim 4:3-4. Sambamba na kutoa katekesi ya kina, tuliopewa dhamana hiyo na Kanisa yatupasa kujifunza kwa kina juu ya ‘teolojía ya mawasiliano.’ Pasipo mawasiliano katika uinjilishaji vyote uvurugika. Ni sawa na kuujenga mnara wa babeli.

Waamini wanapaswa kushirikishwa vizuri maswala ya uinjilishaji kadiri ya nafasi zao. Makleri hawawezi kufanya mambo yote. Tujifunze historia ya Kanisa la mwanzo na changamoto zake. “Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2. Hii ni faida ya kujifunza Teolojía ya mawasiliano. Kielelezo cha Teolojía hii ni uwepo wa Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja nafasi tatu. Na kweli hii ya mawasiliano inajidhihirisha katika uumbaji wa mwanadamu. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Mungu anayafanya haya na kuyatoa hayo yote kwa mwanadamu kwa sababu anatupenda.

Paulo Serereka mwenye ulemavu wa miguu ni mwana Parokia ya Huruma ya Mungu. Kila siku mapema asubuhi huwahi Parokiani na ushinda hapo hadi jioni. Lengo na madhumuni yake kuwepo hapo parokia ni kupata msaada kwa watu wanaofika hapo parokiani kwa sababu mbalimbali.

Omba omba yake kwa watu ilikuwa kero kwa uongozi wa parokia, na hata kwa Baba Paroko. “Kila mara upo hapa tangu asubuhi hadi jioni na hakuna unachoweza kufanya hapa zaidi ya kuomba,” Mhasibu wa Parokia alimkaripia Paulo Serereka. Kwa maneno hayo Paulo alijikokota na gongo lake kuelekea geti kuu la Parokia.

Baada ya muda wa nusu saa hivi, zilisikia sauti mwizi, mwizi, mwizi…, kutoka ofisi za Parokia na mtu mmoja akiwa na mfuko fulani huku akikimbia kuelekea getini. Paulo Serereka aliyekuwa getini alilitega gongo lake na mtu yule alidondoka. Ndipo wahudumu wote wa parokia walikusanyika pale na kuanza kumpa kipigo mwizi yule. Mfuko ule mdogo wa kaki ulikuwa na fedha. “Angalau leo nami mtaninenea lililo zuri midomoni mwenu,” Paulo Serereka aliwaambia wale wahudumu wa Parokia.

Ndugu yangu, naye Paulo Serereka ‘alitoa’ mchango wake kadiri ya hali na uwezo wake kwa sababu ‘aliipenda’ Parokia yake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Lk 18:8b

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie nguvu ndani yetu ili tudumu katika imani thabiti

No hay comentarios:

Publicar un comentario