IJUMAA WIKI YA 28 YA MWAKA-C
Somo:
Efe 1:11-14
Zab/Kit:
33:1-2, 4-5, 12, 13
Injili:
Lk 12:1-7
Nukuu:
“na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku
tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo
yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:11
“Ndiye aliye
arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu
wake,” Efe 1:14
“Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata
wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya
Mafarisayo, ambayo ni unafiki,” Lk 12:1
“Lakini
nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza
wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:5
TAFAKARI:
“Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.”
Wapendwa wana wa Mungu, hatuwezi
kujihesabia haki kwa matendo yetu wenyewe na kujiinua pasipo kweli na haki. Hii
ndiyo tahadhari anayotuambia Yesu katika Injili ya leo. Kujiinua kwa ubinafsi
wako kwa lengo la kupata mastahili mbele
za watu na Mungu ni chachu mbaya sana. Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “jilindeni
na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki,” Lk 12:1b. Unafiki ni kuishi kwa
uhakika kile ambacho sicho ulicho. Ni kuishi kwa kuwapendezesha watu kuwa wewe
ni kitu fulani ilhali sivyo ndivyo.
Ndugu yangu
tunayesafiri sote pamoja katika tafakari hii, ni ushauri wangu kwako hata kama
hauna maana kwako ni kwamba, ‘ishi kile ulicho katika kweli na haki yake.’ Ni
katika kweli hiyo na haki Mungu utunyanyua na kutupeleka pale alipo. Huku ndiko
kuhesabiwa haki na Mungu. Na kuishi
katika kweli na haki ni kutambua kwanza kabisa mimi ni mwanadamu niliyeumbwa
kwa sura na mfano wake Mungu, na amependa niwe kama nilivyo na kuishi katika
kweli hii.
Hakuna haja ya kuogopa
kuishi ukweli huu hata ikibidi kufa kwa ajili ya ukweli huu. Yesu ananiambia
mimi na wewe kwamba, “nami nawaambia ninyi
rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo
kutenda zaidi,” Lk 12:4. Ndugu yangu, kuuishi ubinadamu wako kwa mapaswa ya
Mungu aliyetuumba si kazi rahisi. Wengi wetu hatupendi kujipokea kama tulivyo
ikiwa ndiyo sharti la kwanza kuuishi ubinadamu wako. Je, nina hoja nzito na ya
kweli ya kutokujipokea? Ni nani basi ninayemwogopa? Je, ni nani yanipasa
kumwagopa katika ubinadamu wangu na ulimwengu huu?
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Yesu ananipatia jibu mimi na wewe ni nani tupasaye kumwogopa. Naye anasema,
“mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu
ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk
12:5b. Ni Mungu mwenye uwezo wa kuua na kumtupa mtu Jehanum. “Bwana huua, naye
hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu,
naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7. Hivyo wa
kumwogopa ni MUNGU peke yake. Huyu ndiye tunayepaswa kuwa na hofu naye na si
vinginevyo. Huyu ndiye anayejua kwenda na kutoka kwetu.
Wapendwa, ni Mungu wetu
huyu kwamba “hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora
ninyi kuliko mashomoro wengi,” Lk 12:7. Mungu wetu ndiye yote katika yote.
Saratani mbaya na inayolimaliza Taifa letu leo ni unafiki. Na unafiki huo upo
hapa; ‘hatupendi kuona uhalisia wa kitu kama ulivyo, na badala yake tunaona
uhalisia wa kitu kama tulivyo.’ Ndiyo maana siyo jambo la kushangaza leo
kusikia mipishano ya taarifa kwa kitu kile kile.
Hii ni ishara ya
anguko, tena kubwa sana. Katika kweli hii Yesu anasema, “kila ufalme
uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba
huanguka,” Lk 11:17. Mipishano ya kauli kama tokeo la unafiki, ni ashirio kubwa
la anguko! Je salama yetu ipo wapi?
Salama yetu kama
familia na Taifa ipo katika kweli. Ni katika kweli tunawekwa huru, Yoh 8:32.
Jamii yetu leo na hasa kwa maswala ya umma, ipo tayari kutumia gharama na nguvu
kubwa sana kuubatiza uongo kuwa ukweli, kuliko kukiri kweli. Udhaifu wa mtu au
taasisi inayoongozwa na watu, ni uthibitisho wa ubinadamu wa watu ambao kwayo
kama wanadamu siyo wakamilifu. Jambo la kufanya katika ubinadamu wako ni
kulenga mara zote katika ukamilifu hata kama udhaifu upo. Unapokiri udhaifu
katika kweli na haki, tendo hilo ukupa nguvu, na mwanzo mpya wa tumaini jipya.
Ni katika udhaifu
tunakuwa na nguvu kama asemavyo Mtume Paulo, kwamba, “napendezwa na udhaifu, na
ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo
dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10. Ni kweli pasipo shaka kwamba,
mwalimu mzuri ni ‘mang’amuzi yale tuliyoyapata na tuyapatayo katika mapito ya
maisha katika kweli na haki, na zaidi pale tunaposhikamana na Kristo Yesu.’
Na ndani yake (Kristo
Yesu) “sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na
kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe
1:11. Tupo katika ulimwengu huu kama warithi na wana wa Mungu kuyafanya mapenzi
yake Mungu na siyo ya kwetu hata kama hali na mazingira tuliyo nayo yanaruhusu.
Hivyo kufikiri kwangu,
kuamua kwangu, na kutenda kwangu kusukumwe mara zote na hofu ya Mungu ndani
yangu. Kristo Yesu awe kielelezo cha kila kitu katika maisha yangu. Huyu “ndiye
aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya
utukufu wake,” Efe 1:14. Maisha bila Kristo Yesu msingi wake ni dhaifu sana!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwogopeni yule ambaye akiisha
kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni
huyo,” Lk 12:5b
Tusali:-Ee
Yesu na Mwokozi wangu, niweke huru katika kweli na haki yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario