martes, 25 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 30 YA MWAKA-C


JUMATANO WIKI YA 30 YA MWAKA-C

Somo: Efe 6:1-6

Zab/Kit: 145:10-11, 12-13ab, 13cd-14

Injili: Lk 13:22-30

Nukuu:

“Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki,” Efe 6:1

“Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3

 Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,” Lk 13:23

Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze,” Lk 13:24

Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu,” Lk 13:27 

Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho,” Lk 13:30 

TAFAKARI: “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, masomo ya leo yanatualika tutafakari kwa kina mwenendo wa maisha yetu na wito wa kujitahidi kila mara kuingia katika mlango ulio mwembamba. Bila shaka wembamba wa mlango huu ni mwaliko wa kuishi kadiri ya yale yanayompendeza Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake. Ni kuishi upendo wa Mungu Baba kweli na kuwa na hofu ya Mungu kwa kushika na kuziishi vyema amri za Mungu na Kanisa lake kama familia yake.

Utii katika amri za Mungu ni kumpenda Mungu pasipo shaka. Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Kuzishika na kuishi katika amri zake ni pamoja na kutambua ukweli huu kwamba kwa kupitia Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo tutaiona njia ya kuelekea kwake, tunapata uzima wa kweli, na ndani na katika Kristo mwanaye ndipo penye ukweli wa Mungu Baba na maisha ya umilele. Yesu anathibitisha ukweli huu kwa kusema, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6.

Upendo wa Yesu, ikiwa ni pamoja na mahusiano yake na Mungu Baba, na Roho Mtakatifu (Famili ya Utatu Mtakatifu, na Umoja usiogawanyika), kwa kiasi fulani katika mawasiliano yake, unafanana na umoja na mawasiliano katika familia. Famili katika ukamilifu wake ujidhihirisha na uwepo wa Baba, Mama, na Watoto, ingawa katika ndoa watoto ni tunda la ndoa, na bila watoto ndoa ubaki kuwa ndoa katika ukamilifu wake. Ili kufikia hazma yake, yaani, ule utakatifu katika familia, kila mmoja katika familia lazima atimize wajibu wake. Na moja ya nyajibu hizo ni heshima katika familia (KUHESHIMIANA)

Familia isiyo na utaratibu, ikiwa ni pamoja na kutokuheshimiana, upoteza; tunu, lengo, na utakatifu ule iliyoitiwa. Hivyo ni wajibu wa watoto kuwatii wazazi wao kama Mtume Paulo anavyotufundisha, “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki,” Efe 6:1. Kuwatii wazazi wetu si jambo la shuruti, bali ni haki yao. Wazazi wetu ni Viumbe shirikishwa vya Mungu katika uumbaji pamoja na Mungu. Nafasi na hadhi hii yaliyopewa Wazazi wetu hata malaika hawakupewa ingawa muda wote Malaika humzunguka Mungu wakiwa wanamwabudu na kumsifu. Hivyo, kuwaheshima Baba na Mama yako, “amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3. Furaha waipatayo wazazi wako kwa wewe kutimiza wajibu wako katika kweli na haki, ndiyo baraka na neema kwako.

Hata hivyo, wazazi wetu yawapaswa kutimiza wajibu wao, ikiwa ni pamoja na kuwapatia malezi mema watoto wao na yenye kumpendeza Mungu, yaani, watoto na hata walelewa wao kuwa na hofu ya Mungu. Hivyo, “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana,” Efe 6:4. Leo kuna mporomoko wa kasi ya ajabu katika malezi na familia kwa sababu tu wazazi wa leo hawapendi kufanya na kutimiza majukumu na nyajibu zao. Hii sayansi na hili ‘teke linalotujia kila siku kwa kasi ya ajabu, bila kujiandaa, na bila kufahamu’ limetupumbaza, badala ya kutufanya kuwa werevu katika majukumu yetu ya kila siku na familia kama sababu ya jana yetu, leo yetu, na kesho yetu. Leo hakuna tena ule muda na uwanja wa wazazi kuwafunda watoto wao kila mmoja kadiri ya jinsia yake. Simu ya mkononi imechukua asilimia 75 ya malezi katika familia. Je, kizazi kijacho na Kanisa kwa ujumla wake litakuaje?

Nasi sote kwa ujumla wake, ikiwa kila mmoja na wito wake, ndani na katika wito huo yupo yule tunaye mtumikia. Na kwa namna hii na mwono huu, sisi sote tu watumwa wa yule tunayemtumikia katika kweli na haki. Na ujumbe ni uleule kwamba, “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo; wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo,” Efe 6:5-6. Na tunapotambua kweli katika utumwa huu, basi tuyafanye hayo yote kwa hofu ya Mungu.

Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, ukweli wa Kristo na Mungu tunaupata katika Maandiko Matakatifu, uzima wake tunaupata katika Masakramenti, na njia ya wokovu wetu ni Utukufu tuupatao kupitia njia ile  aliyoichagua Kristo Yesu, yaani, Msalaba. Hivyo tunampenda Mungu tunapolishika vyema neno lake. Yesu anatuambia kweli hii kwa kusema, “Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24.

Kuishi upendo wa kweli, kuzitii na kuzishika amri za Mungu na Kanisa, na kuwa na hofu ya Mungu katika yale yote tunayofikiri, tenda, na kuishi ndiko kuchaguliwa kwetu toka asili. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza,” Rum 8:30. Hii ndiyo sababu ya Mungu kama ilivyo mpendeza na kuchagua kutuumba kwa sura na mfano wake.

Mungu anapenda tuwe wakamilifu kama Yeye alivyo Mkamilifu. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Hii ndiyo furaha ya Mungu kwetu. Mungu hupenda kufanya kazi na wale wampendao pasipo shaka yoyote. Mtume Paulo anathibitisha jambo hili kwa kusema, Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake,” Rum 8:28. Kila mwenye hofu ya Mungu ndani yake ameitwa kwa kusudi lake. Ni vyema ukaanza sasa kuelewa ukweli huu ndani yako na kuishi kadiri Mungu apendavyo.

Katika safari hii ya kuelekea uzima wa milele tumepewa Roho wa Mungu kutuongoza katika kweli na haki na kutusaidia katika udhaifu wetu kama wanadamu.Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa,” Rum 8:26. Hatuombi jinsi ipasavyo kwa sababu tunaomba kwa ajili ya tamaa zetu na mara tupatapo kile tulichokiomba tunatumia vibaya.

Ombi la mtindo huu haliwezi jibiwa kwa sababu hatumruhusu Roho atuongoze. Mtume Yakobo anatupa sababu ya kushindwa kwetu. Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Mungu anatupenda kweli na hutupatia yale tuombayo kadiri ya  mahitaji yetu. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka mara tumwendeapo na kuomba yale tunayohitaji. Mashaka katika maishi hututia hofu na mwisho wa siku tunatawaliwa na mambo mengi na yasiyo ya msingi na kukosa dira ya malengo ya maisha yetu hapa duniani.

Katika Injili ya leo tunamwona mtu mmoja mwenye mashaka anamuuliza Yesu, “Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache?” Lk 13:23. Jibu la Yesu linaturudisha kwenye msingi na malengo ya maisha yetu hapa duniani kama nilivyokwisha elezea hapo mwanzo. Yesu anatujibu kwa pamoja hasa sisi tulio na mashaka, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze,” Lk 13:24. Mlango huu mwembamba unatuwajibisha kujua lengo la maisha yetu hapa duniani, namna ya kuishi ili kufikia lengo hilo, na ni mambo gani ya msingi yatupasa kuyapa umuhimu katika maisha.

Tusipozingatia jambo hilo kama nilivyokwisha elezea hapa mwanza, tusishangae siku ya mwisho kuambiwa maneno haya, “Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu,” Lk 13:27. Udhalimu wa kwanza kwa mtu utakuwa hali ile ya kutokutumia muda wake vizuri na neema anazopatiwa bure na Mungu kupitia Mama Kanisa.

Tutashangaa na kupigwa butwaa tutakapoona wale waliotumia vyema muda wao na neema walizojifunua kwao wakiingia katika maisha ya umilele. Wengi wao ni wale leo tunaowaona wamwisho kwa kila kitu kwa sababu tu hawaendani na mambo ya ulimwengu huu na tamaa zake. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho,” Lk 13:30. Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, ni wakati sasa wa kuzama ndani yako na kuhoji nafsi yako kwa hili Yesu alilotuambia leo, “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba.”  Je, lina ukweli wowote juu ya maisha yako?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia,” Efe 6:2-3

Tusali:-Ee Yesu, tuimarishe kila mmoja wetu kadiri ya wito ule uliomwitia. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario