JUMAMOSI WIKI YA 27 YA MWAKA-C
Somo:
Gal 3:22-29
Zab/Kit: 105:2-3, 4-5, 6-7
Injili: Lk 11:27-28
Nukuu:
“Lakini andiko
limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile
ahadi kwa imani ya Yesu Kristo,” Gal 3:22
“Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa
tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa,” Gal
3:23
“Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke
mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na
matiti uliyonyonya,” Lk 11:27
“Lakini yeye alisema,
Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika,” Lk 11:28
TAFAKARI:
“Heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kutokana na ishara nyingi alizokuwa anafanya
Yesu mbele za watu, mama mmoja hakuweza kuizuia furaha yake. Hivyo alitamka kwa
furaha na kusema, “Heri tumbo
lililokuzaa, na matiti uliyonyonya,” Lk 11:27b. Nani kama Mama? Ni uthibitisho ulio wazi kwamba
Yesu alipata malezi mazuri kama mwanadamu. Sifa na utukufu kwanza kwa Mungu na
kwa Mama Bikira Maria.
Pamoja na furaha hii
ya huyu Mama, Yesu anatutaka tuende ndani na mbali zaidi. Kila mmoja wetu
yampasa kulisikia neno la Mungu na kulishika. Kulishika neno la Mungu ni kulitafakari na kulifanya sehemu
ya maisha yako. Maandiko Matakatifu yanaonyesha dhana hii ya maisha ya mtu
kufanywa mapya baada ya kulisikia neno la Mungu na kulishika. Mungu wetu huyu
aliye na subiri kwa kila mmoja wetu, utupatia muda wa kutosha kabisa. Tatizo
letu kubwa ni pale tunaposhindwa kutumia fursa hiyo.
Hii ndiyo furaha
kubwa sana ya Mungu na wateule wake, yaani, Watakatifu wote huko Mbinguni. Naye
Yesu alimjibu mama yule, “Afadhali,
heri walisikiao neno la Mungu na kulishika,” Lk 11:28. Ndugu unaye safiri nami
katika tafakari hii, neno la Mungu lina nafasi gani katika maisha yako ya kila siku?
Je, ni kitu gani kinachokupa uzima wako kila siku? Na mwisho, siku yako kila
siku huanza na kitu gani? Jibu maswali hayo vyema. Majibu yako ndiyo ukaribu au umbali wako na
Mungu anayekupa uhai kwa hayo unayofikiri ndiyo uhai wako.
Wapendwa wana wa Mungu,
imani yetu bila Kristo Yesu ni sawa na kupanga safari katika kiza kinene na
kwenda tusipopajua. Kristo Yesu ambaye ndiye Neno aliyefanyika mwili na kukaa
kwetu Yoh 1:14, ndiye kielelezo cha kila kitu kwetu, ikiwa ni pamoja na uzima
ule wa milele tunaoutafuta kila siku. Ukweli ni kwamba, “Hata ulipowadia
utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili
sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Maisha yetu kama wafusi wa
Kristo bila Kristo ni sawa na samaki kuishi jangwani. Na “andiko limeyafunga
yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani
ya Yesu Kristo,” Gal 3:22. Je, wamwamini Yesu Kristo?
Alipo Kristo Yesu kuna
Imani, na katika Imani hiyo watu upokea neema na baraka. Torati-sheria ilikuwa
maandalizi ya kuipokea Imani hiyo ya kweli, yaani, Neno huyo wa Mungu
aliyefanyika mwili na kukaa kwetu. Ni kwa mantiki hiyo kwamba, “kabla ya kuja
ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani
itakayofunuliwa,” Gal 3:23. Kristo Yesu kwa kuja kwake kayafunua yote
yamuhusuyo Mungu Baba, na hakuna ufunuo mwingine zaidi ya huu. “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa
Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani,” Gal 3:24. Ni katika kweli hii
tunajiunga na Mtume Petro na kusema, “Wewe (Kristo Yesu) unayo maneno ya uzima
wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa
Mungu,” Yoh 6:68b-69
Ikiwa Kristo ndiye kila
kitu katika maisha yetu, hatuna sababu yoyote ya kuwa na hofu. Hivyo “iwapo
imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi,” Gal 3:25. Kiongozi hapa
imetumika kama ‘mamlaka za kibinadamu.’ Kwa maana hiyo kama tumempokea Kristo
na kuwa ndiye kielelezo cha maisha yetu, hakuna binadamu yeyote kwenye mamlaka
ya kupora imani hiyo ndani yetu kwa sababu kwake huyo mwanadamu hakuna uzima
huo wa milele bila Kristo mwenyewe. Ni kwa sababu hiyo, “sisi sote tumekuwa wana wa Mungu kwa njia ya
imani katika Kristo Yesu,” Gal 3:26. Na tumefanywa wana na warithi wa ufalme wa
Mungu kwa njia ya Sakramenti ya ubatizo.
“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo,” Gal 3:27.
Hivyo ni jukumu la kila mbatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo kwa uaminifu.
Kwa Sakramenti hii ya Ubatizo
ambayo kwayo tumefanywa wana na warithi wa Ufalme wa Mungu, tu sawa wote mbele
za Mungu. Tofauti zetu zilizozama katika ubinadamu wetu hazina tena nafas
imbele ya Mungu ndani na katika Kristo Yesu. Hivyo, “Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu,” Gal 3:28. Huu ni upendeleo mkubwa sana
kwetu. Huu ni upendo usio na kipimo kwetu ambao Yesu kampa kila kwenye hofu
naye. “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi
sawasawa na ahadi,” Gal 3:29. Na ahadi alizopewa Ibrahimu ni hizi: Ibrahimu
atakuwa taifa kuu, hodari na katika yeyé
mataifa yote ya dunia watabarikiwa, Mwa 18:18.
Tumsifu Yesu Kristo!
Heri tumbo lililokuzaa, na matiti
uliyonyonya,” Lk 11:27b
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie neema na baraka zako sawasawa na ahadi zako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario