sábado, 29 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 31 YA MWAKA-C



Somo I: Hek 11 :22-12:2

Zab/Kit: 145:1-2-3, 8-9, 10-11, 13cd-14

Somo II: 2The 1:11-2:2

Injili: Lk 19:1-10

Nukuu:

 “ulimwengu wote mbele zako ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja katika mizani, na mfano wa tone moj ala umande lishukalo asububi juu ya ardí,” Hek 11:22

“Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako,  Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote,” Hek 11:26

“jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo,” 2The 1:12

“kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo,” 2The 2:2

Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” Lk 19:5

 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9 

TAFAKARI:Hata wewe na mimi wadhambi, leo wokovu umefika nyumbani mwetu, tuikimbile nuru ambaye ndiye Kristo Yesu, na tuachane na giza la umauti.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 31 ya Mwaka “C” wa Kanisa. Ujumbe wa leo kwetu na kwa kila mmoja wetu ni kwamba, “hata wewe na mimi wadhambi leo wokovu umefika nyumbani mwetu, tuikimbile nuru ambaye ndiye Kristo Yesu, na tuachane na giza la umauti.” Hivyo masomo ya leo yanaonyesha ukaribu huo wa Mungu kwetu, na ukuu wake usio na kipimo kwetu kwa sababu anatupenda upeo.

Ukuu wa Mungu wetu ni waajabu sana. Hatuwezi kuupima wala kuukisia. Naye ndiye Mungu kwa maana, “ulimwengu wote mbele zako ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asububi juu ya ardí,” Hek 11:22. Ukuu huu wa Mungu na katika upendo wake usio na kipimo, ndiyo ukubwa wa huruma na msamaha wake kwetu. Na kwa namna hiyo katika kweli na haki, Mungu huwahurumia, ‘watu wote, kwa sababu anao uwezo wa kutenda mambo yote, naye huwaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu,’ Hek 11:23

Ndugu yangu, hakuna aishiye leo katika ulimwengu huu kwa hali yoyote ile, iwe ya dhiki au ya heri kwa bahati mbaya. Mimi na wewe ni kusudi la Mungu, kwa maana Mungu ameviumba “vitu vyote vilivyopo, wala hukichikii kitu chochote ulichokiumba,” Hek 11:24. Mimi na wewe na vyote tulivyonavyo iwe mali na utajiri wa dunia hii, au vipawa mbalimbali, vyote ni mali yake Mungu kama asemavyo Mzaburi 24:1. Kile ulicho na unachomiliki katika kweli na haki, uifunua sura, utukufu, na furaha ya Mungu kwako na kwa ulimwengu mzima. Na kwa sababu hiyo, Mungu huviachilia ‘vyote, kwa kuwa ni vyake, ndiye Mfalme Mkuu mpenda roho za watu; maana roho yake isiyoharibika imo katika vyote,’ Hek 11:26

Na katika upendo huu wa ajabu wa Mungu, tunaona katika Injili ya leo makutano kati ya Yesu na Zakayo. Zakayo hamwoneyi Yesu aibu pamoja na watu kuyajua madhaifu yake na ufupi aliokuwa nao. Bado anaona salama yake ipo kwa Kristo tu na siyo mitazama ya wale walikuwa wanamzunguka. Ili amwone Yesu, Zakayo alipanda juu ya mkuyu. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” Lk 19:5.

Ni wazi kwamba huwezi kuwa mrefu zaidi ya wewe mwenyewe. Na kwa kuwa huu ni ukweli wa lazima, kumbe kuvijua na kuviona vile vilivyo nje ya uwezo na kimo chako yakupasa kufanya juhudi ili kuujua ukweli ule ulio nje vya vimo yako. Hivyo Zakayo anatufundisha kwamba hata kama ulimwengu ushatuhukumu, na hali na mazingira yetu yanatukwamisha, bado tunaweza kukutana na upendo na huruma ya Mungu tufanyapo bidii. Mtakatifu Agustino wa Hippo katika kweli hii anasema, “aliyekuumba wewe pasipo wewe, hataweza kukusaidia wewe pasipo wewe.” Hizo Zakayo kwa juhudi zake, na mpango mahususi wa Mungu, anafanikisha ndoto yake, na Yesu anakuwa mgeni wake.

Tendo hili la Yesu linawashangaza wengi na wengine wananung’unika. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi,” Lk 19:7. Hapa tunakumbushwa pia moja ya kazi ya Yesu Kristo katika safari na historia hii ya wokovu kama asemavyo yeye mwenyewe kwamba, “sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu,” Lk 5:32.

Kwa utayari wa Yesu kwenda nyumbani kwa Zakayo, kwa furaha aliyokuwa nayo Zakayo hakuweza kuificha. Hivyo Zakayo anayaweka yote wazi mbele ya Yesu.  Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne,” Lk 19:8. Hii ni toba ya kweli na maungamo ya wazi mbele ya Yesu aliye sasa njia, kweli na uzima.

Maungamo haya ya kweli toka moyoni mwa Zakayo yanaifunua furaha na upendo wa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo na kuonyesha kile hasa Yesu alichokijia ulimwenguni. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9. Wokovu ni kwa kila mmoja na hasa pale tunapouridhia wokovu huo kwa utashi wetu wenyewe na kwa dhamiri iliyo hai na safi. 

Mungu anatazama utayari wako katika upya wa kuyaanza yote nawe na siyo historia ya maisha yako mabaya yaliyopita. Tu wapya mbele ya Mungu siku na muda wowote. Ni wewe na mimi tu kujisalimisha mbele ya uso wake wau pendo, huruma, na Mtakatifu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea,” Lk 19:10. Ndugu yangu, afadhali kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa unajisi.

Nafasi ndiyo sasa kusimama katika kweli na haki, na kuchukia uovu wa aina yoyote ile kwenye maisha yako na jamii inayotuzunguka. Hivyo kwako na kwangu ni mwito tunaopatiwa leo kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake pale alipo. Kwa yeyote aliyepewa dhamana na umma kwake vitahitajika vingi pia. Naye Yesu anasema, “Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48b

Kwa namna hiyo, kiongozi licha ya kuwa tumaini kwa watu, kiongozi ni mwonyesha tumaini hasa pale tumaini hilo linapotoweka. Na katika hali na mazingira haya ambayo tumaini hilo hutoweka, Mtume Paulo anatuwasa na maneno haya ya uzima, msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno,” 2The 2:2a. Ndugu yangu, hapa na pale tunapoona kusalitiwa kwa wale tulio waamini tusiiache kweli na haki, bali ni wakati wa kusimama imara katika kweli na haki hiyo.

Hivyo, “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo,” 2The 2:3a, 4. Matumaini yetu tuyaweke kwa yule atutiaye nguvu, Flp 4:13. Kila mtu kadiri ya imani yake ayashike maadili yaliyo mema na kuupinga uovu kwa nguvu zake zote.

Masumbuko Mponda Kokoto kila siku mapenda alfajiri huondoka na nyundo yake na kurudi jioni. Huondoka akiwa nadhifu na kurudi akiwa nadhifu. Ni mke wake tu katika familia ile wa watoto wanne aliyekuwa anajua kazi ya mumewe.  Kwa kazi hii nzito na ngumu, watoto wake wake walisoma, kula vizuri, kuvaa vizuri na kuwa na makazi mazuri.

Siku mmoja Jumamosi, kama kawaida yake, Masumbuko alijidamka na kuchukua nyundo yake na kuondoka. Mtoto wake wa kwanza wa kiume-Immanuel,  kwa muda mrefu alikuwa anapenda kujua alichokuwa anafanya  Baba yake na nyundo ile. Basi kwa siri alimfuata nyuma polepole hadi eneo lile la kazi.

Mara baada ya kufika Masumbuko alibadili nguo zake na kuvaa nguo za kazi zilizokuwa chafu na kuukuu. Na mara alianza kuyaponda mawe moja baada ya lingine hadi kupata umbo dogo sana, yaani, kokoto. “Dah! Kumbe kula, kuvaa, na kusoma kwetu kwa raha kunatokana na kazi hii ngumu ya Baba? Hakika tunamkosea haki sana pale tunapompigia kelele akiwa amepumzika,” Immanuel alisema kwa masikitiko makubwa.

Hivyo kijana wake-Immanuel baada ya kuyaona yale, alisogea karibu, na Baba yake alipoinua kichwa alikutana na uso wa mtoto wake. “Mbona hupo mahali hapa? Ilikupasa uwe nyumbani unafanya kazi leo jumamosi,” Masumbuko alimuuliza mtoto wake kwa mshangao. “Imenilazimu kujua kila siku huko uendapo na nyundo yako. Na leo nimeona ukweli wote. Baba pole sana kwa kazi ngumu hii,” kijana wake alimjibu Baba yake huku machozi yakimtoka.

“Mwanangu, maisha ni wito, kuchagua, na kuyapenda. Niliona na kujisikia wito huu wa familila, nikachagua kuwa na familia, na hiki ninachokifanya ni ishara ya kupenda kile nilichokichagua. Hivyo katika hali zote nawapenda na nitawapenda daima. Nafurahi kwa sababu mnafuraha kila mara nirudipo nyumbani,” Baba yake alimjibu mwanaye huku akiyapangusa machozi yake.

Ndugu yangu, huu ni upendo wa kweli kwa Wazazi wetu kwa familia zao. Baba yetu wa Mbinguni anatuwazia mazuri zaidi kwa sababu uwepo wetu  uifunua Furaha na Utukufu wake. “Maana  najua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako,  Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote,” Hek 11:26

Tusali:-Ee Yesu, asante kwa kutuona hata sisi wadhambi kwa sababu kwako tu upo usalama. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario