Somo
I: 2Fal 5:14-17
Zab/Kit: 98:1-2, 3ab, 3cd-4
Somo II: 2Tim 2:8-13
Injili: Lk 17:11-19
Nukuu
“Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani,
sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa
kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14
“Akamrudia yule mtu wa
Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa
tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi
nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako,” 2Fal 5:15
“Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana
na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu,
Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:12-13
“Alipowaona aliwaambia,
Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,”
Lk 17:14
“Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote
kumi? Wale kenda wa
wapi?” Lk 17:17
“Mkumbuke Yesu
Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu,”
2Tim 2:8
“Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda
mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9
TAFAKARI: “Kujishusha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa
na siri ile ihusuyo uzima ule wa milele.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 28 ya mwaka “C” wa Kanisa. Na kwa
namna ya pekee, Mama Kanisa leo anatutaka kwa pamoja tutafakari, “unyenyekevu
ukiwa ndio msingi wa Fadhila zote, ndio ufunguo wa maarifa na siri ile ihusuyo uzima
wa milele.” Na tufanyavyo hivyo na kuishi, Mungu atatenda. Masomo yote matatu
ya leo yanatuwasa kutafakari sana tendo hili la unyenyekevu na kujinyenyekesha.
Bila shaka wote twafahamu vizuri habari za Jemadari Naamani, na uponyaji wake
kupitia Nabii Elisha. Safari ya uponyaji wake haikuwa rahisi, kutokana na njia,
na namna ya uponyaji ule ulivyokuwa uwe kwa namna Mungu alivyopenda.
Hata hivyo mara nyingi
hatuyapati yale tuombayo, na hata uponyaji wa yale yatusumbuayo kutokana na
mitazamo yetu kimaisha, na namna tutakavyo Mungu kufanya huruma na upendo wake
kwetu. Mtume Yakobo anasema hivi, “hata mwaomba, wala hampati kwa sababu
mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe niwapo mbele ya
Mungu, ni jambo la msingi na muhimu sana kujishusha na kujinyekesha huku
nikitambua ubinadamu wangu, na kwa huo ubinadamu sote ni wahitaji na waja wa
Mungu.
Mungu utukweza tu pale
tunapojishusha na kujinyenyekesha kwake na kuukubali ubinadamu wetu. Mungu
daima anabaki kuwa Mungu. “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, na ajidhiliye
atakwezwa,” Lk 14:11. Mtoza ushuru katika sala yake hekaluni, kinyume na
Mfarisayo, sala yake (Mtoza ushuru) ilisikika mbele ya Mungu kwa sababu
alijishusha na kusema kwa unyenyekevu na kwa uchache wa maneno kabisa, “Ee Mungu,
uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa tendo hili la unyenyekevu la
mtoza ushuru, Yesu anasema, “Nawaambia,
huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; (Mfarisayo)
kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:14
Jemadari Naamani
anapata uponyaji wa ukoma wake baada tu ya kujishusha na kufanya kadiri ya
mapenzi ya Mungu. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani,
sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa
kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Ndugu yangu,
Mungu ana njia nyingi na mbalimbali za kufikishia ujumbe wake kwetu kadiri ya
hitaji letu, na kwa kupitia jambo hilo au uponyaji huo iwe au liwe somo la
maisha.
Mwanzoni tunaona
Naamani anashindwa kupokea njia ya uponyaji ule, yaani, kujichovya mara saba
katika mto Jordani, kwa kujitazama historia yake, na ufahamu wake. Mpendwa,
“Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mipaka,” Zab 147:5.
Hatuwezi kumpangia Mungu namna ya kufanya hata kama tukiwa na nia njema afanye
yale tumwombayo na tunayotamani.
Ndugu yangu, hata Yesu
mwenyewe, alimwachia Baba yake-Mungu atende kadiri ya mapenzi yake. “Akaenda
mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana,
kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo
wewe,” Mt 26:39. Kama huyu, yaani, Mwana wa Mungu na Mwenye Uweza wote
anajinyenyekeza na kujiachia mikoni mwa Baba yake, mimi na wewe tuna nini cha
kujikweza hata kama historia yetu inaonyesha hatujawahi kushindwa?
Naamani Jemadari,
anapojishusha, jinyenyekeza, na kumwachia Mungu atende kadiri ya neno lake
kupitia Mtumishi wa Mungu Nabii Elisha, Mungu anatenda mara moja. “Ndipo
akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu
wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa nyama ya mwili wa mtoto
mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Kujinyenyekesha na kujishusha ni kukiri Ukuu
wa Mungu kabla na baada atendapo mema yake kwako. Uponyaji wa Naamani Jemadari,
unaibua hisia za uchaji na utambuzi wa Mungu huyu wa Ajabu, na kusema,
"Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika
Israeli,” 2Fal 5:15.
Ndugu yangu,
tunachojifunza katika maisha yetu ya sala na unyenyekevu ni kwamba tunapokuwa
mbele ya Mungu yatupasa kujua kwamba sisi ni viumbe tu, na wahitaji na waja
wake Mungu. Mungu haitaji kujua mazuri yetu kwa sababu hayatampunguzia Wema,
Upendo, Uzuri, na Ukuu wake. Mungu pia haitaji historia ya yale tuyafanyayo
kama alivyofanya Mfarisayo, bali tusiache kutenda mema kwani Yeye aliye Mwema
katika yote na uzuri wote ataonekana katika matendo hayo mema, na hasa
tunapoyatenda kwa wale aliowaumba kwa sura na mfano wake.
Naamani baada ya
kutendewa tendo hili kuu na Mungu kupitia Nabii wake Elisha, anataka kumtolea
Elisha kitu kama tendo la shukrani. Elisha anakataa tendo lile kwani kwa
kufanya hivyo ni sawa na kujifananisha na Mungu. Elisha kwa unyenyekevu
anatambua nafasi yake kama mtumishi tu, tena asiye na faida. Katika tendo hili la
Nabii Elisha, tunajifunza pia kile anachotufundisha Kristo Yesu kuhusu
utumishi. Naye Yesu anasema, “vivyo
hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa
wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Hakika yatupasa
kutumika na siyo kutumikiwa.
Kutokana na msimamo
wake Elisha, tendo lile la kukataa kutolewa kitu linagusa mtima wa Naamani,
naye anaweka ahadi yake kwa Mungu aliye hai. Naye anasem, “Kama sivyo
(kutokupokea kitu), lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala
wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu
kwa miungu mingine, ila kwa Bwana,” 2Fal 5:17. Tumwache Mungu aitwe Mungu, na
ndivyo alivyo.
Ni kwa upendo wake
Mungu katuumba kama tulivyo, yaani, kwa sura na mfano wake, na ndivyo tulivyo
wanadamu. Na kuishi ubinadamu wetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu kwa lengo lile
alilotuumba, yaani, tumjue, tumpende, tumtumikie, na mwisho turudi kwake
mbinguni, ndipo lilipo taji letu, yaani, utakatifu wako. Ni utakatifu huo ambao
ndio cheo chako ndio wezesho la wewe kuuona uso wa Mungu. Bila utakatifu huwezi
kumwana Mungu, kwa sababu Yeye ni Mtakatifu.
Hivyo ni mwaliko kwako
na mwangu leo na kila kutenda kama wa watoto wachanga. Watoto wachanga ndiyo
hufunuliwa mambo ya Mungu kutokana na kujiaminisha pasipo shaka kwa wazazi wao.
Katika hili Yesu anasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa
mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga,” Mt
11:25. Utendaji huu kama watoto ndio utupao fursa ya kuurithi ufalme wa Mungu. “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala
msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 19:14.
Mwisho wa siku ndugu
yangu, “tutahukumiwa au kutathminiwa kwa upendo wetu,” kama asemavyo Mtakatifu
Yohana wa Msalaba. Kwa hiyo, yale yote tufanyayo na tujihesabie tu kuwa
tumefanya yale yampendezayo Mungu. Hatuna chochote za kujivunia mbele ya Mungu
zaidi ya kujishusha na kujinyeyekesha. Mafanikio yetu ni moja ya uzuri wake
Mungu. Mapungufu yetu ni sababu ya ubinadamu wetu, na katika kujishusha na
kujinyenyekeza mbele zake Mungu hatachoka kuzifungua neema na huruma yake
kwetu. Mtume Paulo anasema, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho
chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Kumbe mimi kama Mkristo
kujivuna kwangu iwe Msalaba wake Kristo kwani hakuna Utukufu pasipo Msalaba.
Katika jambo hili ndugu
yangu, yatupasa kujua kwa uhakika kwamba Yesu Kristo ndiye kielelezo cha
UNYENYEKEVU. Kifo cha Msalaba na cha Aibu ni kwa sababu yangu na wewe. Basi,
tujivunie tu Msalaba kwani kwayo kuna Utukufu. Vingine vyote ni vya kupita tu.
Mtume Paulo anatuambia makusudi ya Yesu kufanya hayo yote ni kwamba, “ambaye yeye
mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni
kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya
mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp
2:6-8. Je, ndugu yangu, una cho chote cha kujivunia na na kukufanya kutokushuka
na kujinyenyekesha kwa Mungu?
Katika Injili ya leo tunaona ‘fanya zaidi’ ya waleo
wakoma kumi walivyo yakazi macho yao kwa Kristo Yesu, na kwa ummoja wao, “wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:13. Ndugu yangu, lazima ufahamu msaada wako
unatoka wapi hasa pale unapoona giza tupu katika maisha yako. Uponyaji wa
wakoma hawa ni tofauti kabisa na ponyaji nyingine alizokwisha kuzifanya Yesu.
Yesu anawataka ‘kufanya zaidi’ na kuwaambia, “Enendeni, mkajionyeshe kwa
makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14. Wakoma hawa wanatakasika wakiwa njiani. Kumbe
wakati mwingine kupona kwako kwaweza chukua hatua kwa lengo la kukuimarisha
kiimani, na kukupatia utakaso kamili. Kumbe yote ni neema na heri, na kamwe
nisilitoe tumaini langu kwa yule anipaye uzima huo, yaani, Mungu muumba wangu.
Katika tendo hili la
uponyaji lililo la baraka na neema, unyenyekevu unajidhihirisha kwa tendo la
shukrani. Ni mambo mangapi tunakutana nayo njiani ya neema na baraka ila
hatuoni sababu ya kushukuru? Ni mmoja tu kati ya wale kumi aliyekuja kwa Yesu
na “akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye
alikuwa Msamaria,” Lk 17:16. Tendo hili
linamshangaza sana Yesu, naye akamjibu, “Hawakutakaswa
wote kumi? Wale kenda wa wapi?,” Lk 17:17.
Ona jinsi tunavyomshangaza Mungu tunavyokoswa moyo wa shukrani kwa yale
anayotutendea. Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, bado tu
hauna cha kumshukuru Mungu?
Jambo
lingine la pekee katika tukio hili la uponyaji ni kile mtu apatacho mwisho wa
uponyaji huo. Wale tisa ambao hawakuja kutoa shukrani walipokea uponyaji wa mwili,
na kuwa huru kutoka mateso yale ya ukoma. Ni huyu mmoja tu, tena Msamaria aliyepata vyote, yaani, uponyaji wa mwili na
wokovu. Katika kweli hii Yesu anamwambia, “Inuka,
enenda zako, imani yako imekuokoa,” Lk 17:19. Hakika moyo usio na shukrani ukausha
mema yote! Tunapoutazama kwa ukaribu uhusisano kati ya Wayahudi na Wasamaria,
katika uponyaji huu unaweka wazi maneno haya ya Yesu, kwamba, “vivyo hivyo wa
mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho,” Mt 20:16. Mungu
wetu hana upendeleo, Mdo 10:34-35, hasa pale tunapomwelekea kwa hofu na uchaji
wa kweli.
Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu kwa kuumbwa kwake, Mwa 1:27, na
uwepo wake hapa duniani, mara zote hutafuta maana ya maisha yake. Hufanya hivyo
si kwa bahati mbaya, au udadisi fulani usio na mwalekeo, bali kama alivyo,
mwanadamu usukumwa kufanya hivyo kama tokeo la historia yake kijamii na jamii anayoishi leo na sasa.
Hivyo, mwanadamu huyu hapo alipo kadiri ya imani na maadili yake, hakosi
kuifikiria kesho ambayo bado kuiishi akiwa na matumaini kuwa ipo na yaja.
Na kama ni Mkristo achoki kuyafikiria maisha yale ya umilele na hukumu
yake ya mwisho, kwa sababu anatambua wazi maisha ya hapa duniani ni jukumu la
muda mfupi tu. “Kwa
maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo,
ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda,
kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10. Kwa hali hii, mazingira haya, na mtazamo
huo, mwanadamu hakosi kutafuta maana ya maisha yake. Utafutaji wa maana juu ya
maisha yake humpa pia maana ya mahangaiko na mateso yake.
Katika hali hii Mtume
Paulo anasema, “Nami katika hiyo nimeteswa
hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9.
Neno la Mungu ni hai, na pia ni uhai. Tulisadiki neno kama alivyofanya Diwani
yule wa Kana ya Galilaya, Yoh 4:46, mwanaye aliyekuwa hajiwezi, naye akapata
uponyaji. “Yesu
akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na
Yesu, naye akashika njia,” Yoh 4:50
Maisha yakikosa maana, binadamu hujikabidhi katika ‘ovu’ lolote lile
bila kujali chochote kwa sababu maisha yake kesha yahesabu kuwa si chochote.
Huku ni kutaka tamaa pale tunapokosa tumaini la kweli. Matendo ya uovu
tunayoyashuhudia kila siku katika jamii yetu ni ishara ya watu kukata tamaa na
kupoteza tumaini la kweli katika maisha yao. Ni vyema kama jamii tukajiuliza ni
wapi tulipoupoteza ufunguo huo wa tumaini la kweli. Utoaji wa matamko kila siku
na kwa kila tukio bila ukomo kamwe hatuta upata ufunguo huo wa tumaini la
kweli. Kumbe yatupasa kila mmoja na kwa nafasi aliyokuwa nayo katika jamii,
ikiwa ni pamoja na wale wenye weledi wa mambo haya ya kijamii kufanya tathmini
ya kina kuhusu mwenendo mzima wa jamii yetu leo. Swali ni hili: Kwa nini
tunafanya kama tunavyofanya?
Tunapo mtazama Mtume Paulo tunagundua kuna kitu tofauti. Yesu Kristo
ndiye nahodha wa maisha yake, na kwake, yaani kwa Kristo, maisha yake (Paulo
Mtume) yamepata maana halisi. “Kwa
ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate
wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama
tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama
tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana
sisi; Kama sisi hatuamini, yeye
hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13. Huyu
ndiye Kristo ambaye kwake kama wafuasi wake, kuna tumaini la kweli.
Hata pamoja na ukweli
huo, “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa
na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno
la kweli,” 2Tim 2:15. Ndani na katika Yesu Kristo hakuna sababu ya kuishi kwa
hofu. Na kujishusha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu ndio ufunguo wa maarifa
na siri ile ihusuyo uzima ule wa milele.
Basi nikuache na mfano
huu: ‘kwa wale ambao ni madereza, na hata sisi ambao ni wasafiri tu, bila shaka
tumewahi kukutana na kitu kinachoitwa “shokamzoba.” Shokamzoba ni aina ya chuma
fulani imara na chenye umbo la kujisokota katika mtindo wa duara na kufanya
mnaso fulani.
Pamoja na kazi kubwa ya
shakamzoba kuzuia uharibufu au uvunjikaji wa vitu vilivyo kwenye mwendo,
shokamzoba utujengea hisi fulani tofauti ya pale tulipo na kile kinachoendelea
nje ya mazingira yale tuliyopo. Mara nyingi katika kweli hii wengi hatuguswi
kwa sababu utulivu tulionao wakati huo upoteza kweli hii. Katika hali hii ya
utulivu ilhali tupo kwenye mwendo kasi, shokamzoba huwa mwimili wa kila kitu.
Hivyo vyote vibebwavyo
juu yake hubaki salama tu iwapo shokamzoba hizi zitabaki katika hali yake ya
usalama. Katika maisha ya mwanadamu, shokamzoba ndiyo fadhila kuu ya
unyenyekevu. Bila unyenyekevu, yote tuyajengayo juu yake, yaani, fadhila
nyingine zote, hukosa msingi imara. Kuijenga jamii mpya na yenye mwelekeo
chanya, mimi na wewe lazima yatupasa pasipo shuruti kuwa shokamzoba.’
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nami katika hiyo nimeteswa hata
kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9
Tusali:-
Ee Yesu Mwema, nijalie fadhila ya Unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario