domingo, 30 de octubre de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA WATAKATIFU WOTE


Sikukuu ya Watakatifu Wote

Somo I: Ufu 7:2-4, 9-14

Zab: 24:1bc-2, 3-4ab, 5-6

Somo II: 1Yoh 3:1-3

Injili: Mt 5:1-12a

Nukuu:

Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,” Ufu 7:11

“Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b

Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1

Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3 

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12

TAFAKARI: “Utakatifu ndiyo Cheo chako.”

Wapendwa katika Kristo, leo Mama Kanisa kwa furaha kubwa anaadhimisha sikukuu ya Watakatifu wote. Kwa namna ya pekee kabisa mimi na wewe leo tunakumbushwa kwamba ‘Utakatifu ndiyo Cheo chetu.’ Malengo ya Mbatizwa yeyote ni kuwa mkamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ndio wito wa kila mbatizwa ili kuifikia taji ile la Utakatifu ambayo ndilo cheo chako. Ni kuwa na matumaini na Mungu na kila siku kujitakasa na kuepuka kuishi katika hatia. Nakila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3 

Ndugu yangu, tungali hapa dunia wengi wetu hupenda kujipambambanua na ubora wa familia zetu, koo zetu, makabila yetu, itikadi zetu za kisiasa na kidini, na hata utaifa wetu. Tukiishi katika ngazi hii tu bado hatujajua hatma ya uwepo wetu hapa duniani. Huko Mbinguni hatutajulikana kwa hayo niliyoyataja, bali tutajulikana kwa  usafi wetu uliotokana na UTAKATIFU wetu tuliouishi hapa duniani ikiwa ni mahali tu pa maandalizi na kupita, na kwa muda mfupi tu.

Kila mmoja wetu aweza kuwa Mtakatifu. Utakatifu wako ni matokeo ya kuwa mwaminifu kwa mambo madogo madogo ya kila siku, na kuyafanya hayo kwa ukamilifu wake. Ni kuwa tayari kumpa Kristo nafasi ya ndani ya moyo wako ili atende kazi nawe kwa yale yanayompendeza Mungu na jirani yako. Utakatifu wako ni tokeo pia la kufungua milango kwa wote wenye uhitaji bila kujali historia zao na mapungufu yao. Ni kujaribu kufanana na Yesu katika kuwaza, kutathmini, na kutenda. Tunapokuwa karibu na Kristo ndivyo tunavyofunuliwa siri za Baba yetu wa mbinguni na Ufalme wake.

Ukaribu huu niliousema, utufanya kuwa watoto wapendwa wa Mungu katika utii usio shuruti. Tunatii kwa sababu Mungu anatupenda na anatutakia mema katika ukamilifu wake. Ndugu yangu, Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1. Maisha haya ya utakatifu yatatudai na yanatudai kila siku kusimama katika kweli na haki, na wakati mwingine tutapimwa katika kweli hiyo, yaani,  Imani yetu.

Kupimwa huku kwa Imani kwa weza pia kutuondolea uhai wetu ambao ndio kitu cha thamani kupita vyote tungali hapa duniani. Basi, hili litakapotokea yatupasa kuyasema maneno haya pasipo shaka yoyote, “kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21. Ni kuyaona yote yaliyofaida kwako ni hasara kwa ajili ya Kristo, Flp 3:7. Tunapoyaachia maisha yetu katika kiwango hiki, Kristo kamwe hawezi kutuacha katika taabu hizo. Kristo hubaki kuwa faraja kubwa kwetu katika dhiki na taabu hizo. Naye anatuambia nyakati kama hizo tuwe watu wa kufurahi kwa sababu tunamruhusu Mungu kutenda mambo katika hali yetu ya uduni na Mateso. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12. Je, wayafurahia mateso yako?

Mtawa mmoja wa kiume katika Monasteri fulani alijijengea ukaribu sana na Yesu wa Ekaristi Takatifu. Mtawa huyu alikuwa mpishi wa muda mrefu katika Monasteri hiyo. Aliipenda sana kazi yake na kwake ilikuwa moja ya kumtukuza Mungu kupitia huduma hii kwa wanajumuiya wenzake. Kamwe hakuwahi kunung’unika hata pale ambapo kazi zilikuwa nyingi kupita uwezo wake.

Kila asubuhi Mtawa huyu mara baada ya masifu ya asubuhi, na Misa Takatifu, huenda bustanini kuchuma mboga, na vitu vingine kama maandalizi ya chakula cha Mchana na jioni. Bustani ile ilikuwa baada ya kulipita Kanisa. Hivyo alijiwekea ahadi ya kuongea na Yesu wa Ekaristi Takatifu kila siku kabla ya kufika bustanini.

Siku moja akiwa na kikapu chake na kisu aliingia Kanisani na kuanza kusali na kutafakari mbele ya ‘Terbenakulo,’ Sehemu zinapohifadhiwa Hostia Takatifu. Mara alishtushwa na sauti ya kengele ya Malaika wa Bwana, iliyoashiria pia ni muda wa chakula cha mchana. Mtawa huyu aliingiwa na hofu kubwa sana kwani alikuwa bado hata bustanini hakuwa amefika.

Mtawa huyu aliondoka kwa haraka ili awahi kuomba msamaha kwa watawa wenzake kwa kutokuandaa chakula kile cha mchana. Maajabu ni kwamba alipofika tu eneo la jikoni alikaribishwa na harufu nzuri sana ya chakula na kusikia watawa wenzake wakimsifu kwa chakula kitamu alichoandaa. Kila mmoja alitaka kuongea naye na kumpa asante kwa kazi nzuri aliyofanya.

Akiwa ameshika kikapu chake na kisu ndani yake, alionekana akitokwa na machozi ya furaha huku akisema “asante Yesu kwa kuniona na kuniondolea aibu hii.” Watawa wote walibaki midomo wazi! Ndugu huyu alisimulia yote yaliyotokea. Jumuiya yote ilijawa na furaha na kumtukuza Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapokuwa karibu na Mungu, kamwe hawezi kutuacha. Mungu atatupigania hadi mwisho. Hivyo tuwe waaminifu na kufanya yote kwa ukamilifu tukimtanguliza Mungu kwa kila kitu. Mtume Yakobo anatuambia siri hii kwa kusema, Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili,” Yak 4:8. Haya ndiyo maandalizi ya cheo chako, yaani, Utakatifu wako.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b

Tusali:-Ee Yesu, na Bwana wangu, kwako yote yawezekana. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario