Sikukuu ya watakatifu Simoni na Yuda, Mitume
Somo: Efe 2:19-22
Zab: 19:2-3, 4-5
Injili: Lk 6:12-16
Nukuu:
“Mmejengwa juu ya
msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,”
Efe 2:20
“Katika yeye jengo
lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,”
Efe 2:21
“Katika yeye ninyi
nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho,” Efe 2:22
“akachagua kumi na
wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni,
aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na
Filipo na Bartolomayo, na Mathayo
na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa
msaliti,” Lk 6:13b-16
TAFAKARI: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, Kristo ni
jiwe la pembeni.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu
ya Mitume Simoni (Mkananayo-Zelote) na Yuda (Tadei-wa Yakobo).
Simoni
Mkananayo alikuwa mmojawapo kati ya Mitume wa Yesu. Ili
kumtofautisha na mtume mwenzake Simoni Petro anaitwa Mkananayo, yaani Mwenye
juhudi kwa ukombozi wa Israeli kutoka ukoloni wa Roma. Jina lake linapatikana
katika orodha zao zote, lakini hatuna habari zake zaidi, isipokuwa masimulizi
mbalimbali yasiyo na hakika. Inasadikika kuwa kaburi lake liko Komani
(Georgia).
Yuda
Tadei ni jina la mmojawapo kati ya Mitume wa Yesu, ambalo
Injili zinajitahidi kumtofautisha na Yuda Iskarioti, msaliti wa Yesu. Habari
zake za hakika zinategemea Agano Jipya ambamo anatajwa katika orodha ya
Thenashara ambao waliteuliwa na Yesu Kristo kama msingi wa taifa jipya la Mungu
wakatumwa naye kuhubiri na kuponya.
Injili ya Yohane tu
inaripoti neno lake moja, katika simulizi la karamu ya mwisho, alipomuuliza
Yesu imekuwaje atajifunua kwao lakini si kwa ulimwengu (14:22). Yesu alimjibu
kwamba yeyote anayempenda atashika neno lake, na Baba atampenda na kufanya
maskani yake kwake pamoja na Mwana. Anafikiriwa na wengi kuwa mwandishi wa
Waraka wa Yuda, lakini hakuna hakika kwa sababu jina hilo la babu wa Wayahudi
wote lilikuwa la kawaida mno.
Mitume kwa ujumla wao, yaani, wale kumi na mbili, kwa maisha
yao na ushuhuda wao wa Imani ndiyo msingi Imara wa Kanisa letu kama tunavyoliona
hii leo. “Akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina
la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na
Bartolomayo, na Mathayo na
Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa
msaliti,” Lk 6:13b-16. Sadaka yao kwa maisha yao ya Imani juu ya Kristo Yesu,
Kanisa linaendelea kutimiza wajibu wake kama Sakramenti ya wokovu wetu. Kristo
Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.
Ukristo wetu na Imani yetu imejengwa juu ya msingi wa Mitume
na Manabii, na Kristo Yesu akiwa jiwe kuu la pembeni. “Mmejengwa juu ya
msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,”
Efe 2:20. Ni fahari ya kila aliyebatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo na
kuendeleza msingi huu imara wa Imani. Hivyo kila mmoja wetu kwa njia ya Kristo
na kwa sadaka ya maisha yake na wito wake, ameunganishwa na hekalu la Mungu. “Katika yeye jengo
lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,”
Efe 2:21.
Mitume
tunaowasheherekea leo ni mfano wa kuingwa kwetu. Mitume hawa walikuwa mashahidi
na manabii katika kipindi chao. Maisha hayakuwa rahisi tunapolitazama Kanisa la
Mwanzo. Wengi wao walikufa kwa kuuwawa kikatili, ila hakuna aliyemsaliti Kristo
zaidi ya Yuda Eskariote. Leo miongoni mwetu akina Yuda wapo wengi sana. Ni ni
changamoto ya Kanisa na maisha yetu ya kijamii.
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Kanisa linachangamoto nyingi sana. Ili kuzikabili changamoto
hizi, yampasa kila mbatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo. Pili, kila mmoja wetu
kadiri ya wito wake ajitahidi kila siku kufanana na Kristo ambaye ndiye jiwe
kuu la pembeni ambapo maisha yetu na sadaka yake upewa maana. Huu ni ushuhuda
tosha wa ukimya hata pale ambapo Kristo hakubaliki kutokana na mitazamo tofauti
ya Kiimani.
Matendo
yetu mema humwakilisha vizuri Kristo popote kuliko kile tukiaminicho kwa
nadharia tu. Mtume Yakobo anatupatia changamoto hii kwa kusema, “Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo.
Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya
matendo yangu,” Yak 2:18.
Wapendwa
wana wa Mungu, tuwe waaminifu kwa wito wetu kila mmoja kadiri ya namna
yake, na upendo uliobeba matendo yetu
mema kwa watu wote.
Mitume
wa Yesu: Wa kwanza, Simoni Petro, Andrea, Yakobo Mkubwa, Yohane,
Filipo, Bartholomayo, Tomaso, Mathayo, Yakobo Mdogo, Simoni Mkananayo, Yuda
Tadei, Yuda Iskarioti; ambaye baada ya
kifo chake, nafasi yake ilishikwa na Mathiya
Tumsifu
Yesu Kristo!
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tujalie moyo ya Kitume na Kimisionari kuanzia pale tulipo. Amina
Watakatifu Simoni, na
Yuda Mitume, Mtuombee. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario