miércoles, 19 de octubre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 29 YA MWAKA-C


ALHAMISI WIKI YA 29 YA MWAKA-C

Somo: Efe 3:14-21

Zab/Kit: 33:1-2, 4-5, 11-12, 18-19

Injili: Lk 12:49-53

Nukuu:

“Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu,” Efe 3:17-19

“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina,” Efe 3:20-21

Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano,” Lk 12:51 

Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52 

Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53

TAFAKARI: “Kwa uwepo wangu kwenu kwa ubinadamu wenu ni mfarakano.”

Wapendwa wana wa Mungu, uzima wa milele ndani na katika Kristo Yesu tunausikia leo kutoka katika kinywa chake mwenyewe Yesu Kristo, hasa kwa maneno haya ya kuchukua hatua tukiwa tunajitathimini maisha yetu ya kiroho. Naye anatuambia, Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano,” Lk 12:51. Ni mafarakano katika maana ya vita dhidi ya ubinadamu wetu. Kumfuata Kristo katika ukamilifu yakupasa kuushinda ubinadamu wako kwa kulenga ukamilifu ingawa udhaifu upo.

Ni kwa kupitia Kristo aliyeushinda uovu kwa wema, yaani kuwa tayari kufa kwa ajili yangu na wewe waweza kuishinda vita hii. Msalaba ni ishara ya huo ushindi wa wema dhidi ya uovu. Mimi na wewe,  nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14.  Je, watambua nguvu ya msalaba katika maisha na wokovu wako?

Wapendwa kama upo tayari kufanywa upya katika ukamilifu ndani na katika Kristo Yesu, uwe tayari kupokea sintofahamu kwako na wale waliokuwa nawe karibu kwa sababu ya ubinadamu wako na yale waliyokuwa wakiyafurahia kutoka kwako. Ukiwa rafiki wa kweli na karibu wa Yesu, giza la uovu litakuwa na vita kubwa na mwanga wa Kristo ndani ya maisha yako. Hivyo Yesu anatupatia changamoto hii kwa kusema, Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52. Hii ni vita Takatifu ya kiroho yenye kulenga ukamilifu wa kweli utupelekao kwenye uzima wa milele. Yesu hakuishia hapo tu. Anatuambia vita hii huenda hata kwa ndugu zetu wa damu. Je, upo tayari kufarakana na familia yako, Baba, Mama, na ndugu zako katika kweli na haki juu ya Kristo Bwana na mwokozi wako?

Katika ukweli huo wa kuelekea ukamilifu na uzima wa milele, Yesu anatuambia, watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53. Unapoamua kumfuata Kristo hakuna mbadala wake ikiwa ni pamoja na kutazama nyuma. Ni heri kuwa baridi au moto kuliko kuwa vuguvugu katika Imani. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22. Kwa maana nyingine, hakuna utukufu pasipo msalaba. Mtihani mkubwa kupita yote kwa mwanadamu ni kushindwa kufanya maamuzi ya kina kuhusu hatma ya maisha yake. Pale tunaposhikwa kigugumizi cha kuacha mazoea yetu na kufuata njia mpya na mwelekeo mpya katika maisha, mwanadamu huishia kuwa masikini wa mwili na roho.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, Mkristo bila Kristo ni kupoteza muda. Dira na dhima ya Mkristo ni kuishi ndani na katika Kristo hasa maisha ya ufufuko. Na maisha ya ufufuko ni kulenga mara zote juu pale Kristo alipo, Kol 3:1-2. Hivyo mara zote, “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu,” Efe 3:17-19. Haya ndiyo maisha ya ufufuko ndani na katika Kristo Yesu.

Hivyo tunakila sababu ya kumtukuza Kristo Yesu “awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina,” Efe 3:20-21. Kanisa ikiwa ndilo Mwili wa Kristo nasi viungo vyake, kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake yampasa kuishi kwa uaminifu ahadi zake za ubatizo.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52

Tusali:- Ee Yesu na Mkombozi wangu, nijalie uthabiti katika imani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario