martes, 4 de octubre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 27 YA MWAKA-C


ALHAMISI WIKI YA 27 YA MWAKA-C

Somo: Gal 3:1-5

Zab/Kit: Lk 1:69-70, 71-72, 73-75

Injili: Lk 11:5-13

Nukuu:

“Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?” Gal 3:1

“Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:2

 “Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:5

“Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa,” Lk 11:9

“Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11:10

 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Lk 11:13

TAFAKARI: Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:2

Wapendwa wana wa Mungu, maneno haya ya Yesu kwetu leo ni uzima kwani yeye ndiye njia, kweli na uzima wetu. Naye anasema, kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11.10. Tokeo la tendo hili utegemea sana kina cha imani yako.  Hata hivyo mara nyingi hatuyapati yale tuyaombayo si kwa sababu Mungu hasikii maombi yetu, bali Yeye mwenyewe anajua ni wakati gani ufao kutupatie kile tuombacho.

Kwa hiyo yatupasa kudumu katika maombi tukiwa na imani thabiti bila kukata tamaa. Kwa upande mwingine yawezekana hatuyapati yale tuyaombayo kwa sababu hatujui kuomba vizuri. Mtume Yakobo anatuambia hivi; “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe kwa maana nyingine kuomba kwetu kusilenge tu katika ubinafsi wetu. Sala uombayo ilenge pia makundi mengine yenye mahitaji kama yako na hata yasio na mwelekeo na ya kwako.

Pamoja na imani dhabiti, jambo linguine katika sala ni kuwa na msimamo endelevu na komavu. Kutokuwa na msimamo katika sala ni tatizo kubwa sana katika kufunguliwa kwetu kwa yale tuyaombayo. Uvumilivu katika sala ni muhimu sana, na huonyesha ukomavu katika maisha ya kiroho. Tunapokosa utulivu wa ndani ni rahisi kubebwa na kila wimbi au upepe. Mtu yeyote anayeruhusu hali hii maombi yake huwa ya majaribio na kumfanya kuhama kutoka Kanisa moja kwenda lingine. Hali hii inapoota mizizi humfanya muhusika kutoka imani moja na kwenda nyingine. Mtu huyu anachotafuta ni kile kiitwacho ‘upako’ kwa kubahatisha bahatisha. Mungu wetu sio wa kubahatisha na wala si wa majaribu.

Mwisho wa siku mtu mwenye mwelekeo huu wa Imani huishia kutokuamini kabisa. Hukosa imani kabisa na Mungu aliyekuwa anamwamini hapo mwanzo na kuishia kuwa asiyeamini chochote. Somo letu la Injili linafafanua vizuri dhana nzima ya wanyofu wa moyo na kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Hawa ndio waliomfanya Mungu kuwa kimbilio lao. Hawa ndio wale wasiokuwa na mbadala wa maisha yao zaidi ya Mungu katika shida zao. Hawa ndio Yesu anaowaambia, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa,” Lk 11:9. Huu ndio uhusiano wa Mungu na aliyemnyofu wa moyo.

Mungu kamwe hatosita kutokumhesabia haki katika kweli aliye mnyofu wa moyo. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11:10. Ni kweli hata aliyekatili aweza kutoa bila upendo kwa yule anayemsumbua, lakini mwenye kupenda hawezi kuacha kutoa. Mungu wetu ni upendo na anajua mahitaji yetu yote. Naye Yesu anaufunua upendo huu wa Mungu kwetu kwa kusema, Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Lk 11:13. Ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii,  jisalimishe kwake aliye Mungu wa kweli, upendo, haki na amani.

Hata hivyo, Mtume Paulo katika somo letu la kwanza anaendelea kuweka wazi kwamba kazi yoyote ya sheria yoyote ile haina uwezo wa kumhesabia  mtu haki kwa ajili ya dhambi zake za zamani. Mungu anataka wewe na mimi na tulio wakristo kushika sheria zake na amri katika dhamira iliyo hai, kamili, na ya kiroho. Kwa maana hiyo,  hakuna sheria yenye uwezo wa kusamehe dhambi, au kumhalalisha kiroho mtu na Mungu, kutoa Roho Mtakatifu, au kumpatia mtu uzima wa milele.

Kazi ya sheria za Mungu na amri zake ni kufafanua dhambi: Gal 3:1-5, ‘Enyi Wagalatia, nani aliyewaloga msitii kweli, ambao mbele ya macho ya Yesu Kristo, aliyesulibiwa, ilikuwa imeelezwa katika maandishi na tangazo la wazi? Hii tu nataka kujifunza kutoka kwenu: Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:2.  Je, mu wajinga kiasi hicho?  Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?” Gal 3:3,  [kwa kutii sheria za kimwili za kiyahudi]... Kwa hiyo, fikiria hili: “Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:5

Wapendwa wana wa Mungu, matendo ya sheria ni ‘kweli ile ya Mungu iliyopotoshwa ili kukidhi matakwa ya kibinadamu.’ Na nyakati zile za Yesu na hata kipindi kile cha jumuiya ya kwanza ya Wakristo, Wayahudi walifuata tafsiri ya Torati na masimulizi yake-Talmud ambayo ilikuwa imejaa mbwembwe nyingi za kibinadamu bila utakatifu wa Mungu ndani yake. Hivyo kwa kuyafuata matendo hayo ya sheria ni kupotea muda ikiwa ni pamoja na chukizo kwa Mungu na maigizo kwa mwanadamu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?” Gal 3:5

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie heri na baraka katika maisha yetu ya kila siku kadiri ya wema na huruma yako kwa sababu watujua vyema. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario