domingo, 23 de octubre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 30 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 30 YA MWAKA-C

Somo: Efe 4:32-5:8

Zab/Kit: 2:1-2, 3, 4, 6

Injili: Lk 13:10-17

Nukuu:

“tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32

“Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,” Efe 5:1-2

“Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru,” Efe 5:3-4

 Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako,” Lk 13:12.

TAFAKARI: “Sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru.”

Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo inatupa maisha mapya ndani ya Kristo pale tunapomwamini. Maisha ni mali na zawadi ya Mungu kwetu, kwani mbingu na vyote ni mali yake Mungu, Zab 24:1. Hakuna mbadala kuhusu uhai wa mtu. Yesu analithibitisha hili kwa kuvunja taratibu za kisinagogi na kisabato kwa kumponya  mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.

Mateso na mahangaiko yetu ufikia kikomo chake tukiwa na imani pasipo shaka juu ya Mwana wa Mungu. Yesu hakuweza kukaa kimya anapoona udhaifu wa mama yule licha ya kwamba taratibu za kisinagogi na kisabato hazikumruhusu kufanya aliyoyafanya. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako,” Lk 13:12. Tendo hili linaibua mjadala mkubwa kuhusu uhalali wa Yesu kutoa huduma ile.

Jambo la ajabu Wayahudi waliheshimu taratibu zao hizo, bila kuona upendo na huruma ya Mungu kwao na watu wengine. Je, kwa nini basi mimi na wewe tunajisikia vibaya mmoja wetu atendapo jambo jema na lenye kumpendeza Mungu? Ndugu uliyesafiri nami katika tafakari hii kama unataka kuishi ndani na katika Kristo fuata lililo jema na tenda mema siku zote.

Ikiwa kwa upendo na furaha yake Mungu ilimpendeza kutuumba kwa sura na mfano wake, ni jukumu la kila mmoja wetu kuona fahari hiyo ndani yake na kwa wale wote wanaomzunguka. Tunadumu katika kweli hiyo ya kufanana naye Mungu pale tunapoendeleza upendo na furaha hiyo kwa wengine. Naye Mtume Paulo katika kweli hii anatuwasa kwamba, “iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi,” Efe 4:32. Kumbe yanipasa kuumia ndani yangu naposhindwa kuona shida na mahangaiko ya jirani yangu, ambao ni wale wote wenye uhitaji.

Ukristo wetu wapaswa mara zote kufanana na tabia ya Yesu Kristo. Pamoja na mambo mengi aliyoyafanya Mkombozi wetu Yesu Kristo, Kristo Yesu alikuwa karibu na rafiki ya wadhambi, waliotengwa, wezi, wazinzi, wanawake na watoto. Aliyafanya haya siyo kuwafariji na kuwapa moyo ili waendelee katika matendo yao ya giza au hali zao za kutokuwa na matumaini, bali aliyafanya haya ili wamjeukie Mungu na wauone uso wa wake wa upendo na huruma. Hivyo nasi kama wafuasi wake Kristo na ‘kama watoto wanaopendwa; tuenende katika upendo, kama Kristo naye alivyotupenda sisi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato,’ Efe 5:1-2. Upendo ndiyo kila kitu ndani na katika Kristo Yesu.

Hata hivyo, kama wana wa Mungu yatupasa kuishi katika matendo ya mwanga kila wakati. Hivyo tuyapige vita matendo ya giza kama asemavyo Mtume Paulo; “uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru,” Efe 5:3-4. Matendo haya ya giza hayana uzima ndani yake zaidi ya kifo na kutokuuridhi ufalme wa Mungu, Gal 5:19-21. “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu,” Efe 5:5. Kuepukana na kadhia hii ni kufuata alilotufundisha Kristo Yesu kwamba, ‘yatupasa kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu,’ Mt 5:48. Ni hatua muhimu sana ya kukua kiroho kila siku.

Leo katika mazingira haya ya utandawazi, ipo mifumo mingi sana ya maisha yenye kubeba unafuu na uboreshaji. Ila unapozama ndani zaidi ya hayo yabebayo mifumo hiyo utagundua kwa kiasi kikubwa ni udanganyifu mtupu. Wito kwako na kwangu ni kwamba, “Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao,” Efe 5:6-7. Ni vyema tukajikatalia yale yote yasiyotupeleka katika uzima wa milele.

Ni wito kama Kanisa-wabatizwa wote, kuisha maisha ya ufufuko pamoja na Kristo, yaani, “tuyatafute yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi,” Col 3:1-2. Tu ngali bado katika giza kama hatuishi maisha ya ufufuko na pamoja na Kristo, na mwisho wa siku ukombozi wetu ni bure. “Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru,” Efe 5:8. Ndugu yangu, zama ndani ya wito wako na jikatalie yote yale ya giza.

Tumsifu Yesu Kristo!

"Zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru," Efe 5:8

Tusali:-Ee Yesu, tufanye vyombo vya upendo na huruma yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario