jueves, 29 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 27 YA MWAKA-C


JUMATATU WIKI YA 27 YA MWAKA-C

Somo: Gal 1:6-12

Zab/Kit: 111:1-2, 7-8, 9, 10c

Injili: Lk 10:25-37

Nukuu:

“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine,” Gal 1:6

“Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal 1:8

 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25

“Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27

TAFAKARI: “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na mbwembwe zote za mwanadamu hapa duniani, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiuliza swali hili la msingi alilouliza mwana-sheria mmoja wa Kiyahudi kwa Yesu kuhusu uhai. Mwana-sheria huyu anamuuliza Yesu hivi; “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25. Msingi wa swali hili haupo kwenye uhai tu wa leo na kesho, bali uhai katika umilele wake. Tuelewe kwamba mwanadamu ameumbwa kuishi milele, na hayo ndiyo makusudi ya Mungu katika uumbaji wa mwanadamu.

Tatizo kubwa la mwanadamu ni mbwembwe nyingi alizonazo akisahau kuwa muda aliopewa hapa duniani hausimami kumsubiri. Mhubiri anatuwasa na kusema, “mwanadamu hadumu katika heshima, bali amefanana na wanyama wapoteao,” Zab 49:12. Fahari ya mwanadamu ni yule aliyemuumba, yaani Mungu wake. Mengine yote ni mbwembwe tu! Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake. Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako,” Kumb 10:20-21. Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba utajiri wako, ufahamu wako (kiwango cha elimu ulicho nacho), umaarufu wako, nk, bila Mungu ni bure kabisa.

Yesu kabla ya kumjibu vizuri mwana-sheria yule wa kiyahudi alitaka kujua uelewa wake wa Maandiko Matakatifu (Torati) yanasema nini kuhusu uhai wa Milele. Mwana-sheria yule akamjibu kwa staha, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27. Yesu anaridhika na jibu hili na anamwambia hivi; “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28. Kuishi kwetu hapa duniani ambapo kunatupelekea kuishi milele baada ya kifo, kama wanadamu kwatuwajibisha kufanya kwa weledi mkubwa mambo makuu mawili.

Moja, mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, roho yako yote, na nguvu zako zote. Kwa maana nyingine ni kutumia vyote Mungu alivyokujalia ili umpende na ubaki kumpenda daima. Afya yako njema, akili yako ya pekee, utajiri wako, na umaarufu wako hapa nduniani isiwe sababu ya kujitenga na upendo huu wa Mungu. Hayo Mungu aliyokujalia kwa namna ya pekee isiwe sababu ya kuwakejeli wenzako ambao kwa mtazamo wako wa kibinadamu waona hawastahili mema yoyote mbele ya uso wa Mungu.

Ndugu yangu, hata yale tunayoyaona kwa macho yetu kama udhaifu wa mtu na wengine, Mungu wakati mwingine utumia udhaifu huo kutufundisha siri ya maisha na uhai tuliopewa na Mungu mwenyewe. Maisha  na uhai tuliyonayo ni mali na zawadi yake Mungu. Mimi na wewe tumepewa uhai huu na kuazimwa kwa muda tu hapa duniani kama sababu ya kuutumia vyema uhai huu ili tuishi milele baada ya muda ambao kila mmoja wetu kapewa kadiri ya mapenzi yake Mungu. “Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga,” Zab 102:3.

Pili, nimpende jirani yangu kama nafsi yangu. Jirani yangu ni yeyote yule ninayekutana naye na wale wote wanaonizunguka, yaani, wahitaji na wasio wahitaji. Jirani yangu ni kama kioo cha kujitazama ukamilifu wangu mbele ya Mungu. Je, udhaifu wa jirani yangu unasema nini kuhusu maisha yangu mimi niliyejiinua na kujiona safi na mwema kuliko wengine? Yesu, anakemea hali hii kwa Mafarisayo na Waandishi, na kwetu pia. Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Mtazamo huu wa ugeugeu na kujiinua mbele za Mungu pasipo mastahili yoyote ndio sababu ya mfano wa Msamaria mwema.

Wafarisayo ambao kwa kiasi kikubwa walijiinua na kuwa wepesi kuwahukumu wengine, wanashindwa kuokoa uhai ambao ni mali na zawadi ya Mungu kwa vile tu muhitaji huyu na mhusika huyu hakuwa Myahudi. Wakati mwingine tunashindwa kusimama katika kweli kwa vile tu mhusika siyo kutoka familia yetu, ukoo wetu, kabila letu, au kutoka Kanda yetu. Wenye mitazamo kama hii ilihali wanajiita wafuasi wa Kristo, basi Kristo huyo huendelea kusulubiwa kwa matendo yao. Kristo huyo siyo fahari ya maisha yao. Mimi na wewe kama wafuasi wa Kristo hatuna kitu kingine cha kujivunia zaidi ya Msalaba wa Kristo.  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Je, tusikemee maovu? La hasha! Mkemeapo Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:1, 21, 23-24. Je, nauona udhaifu wangu ninapoutazama udhaifu wa mwingine?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anapomwambia mwana-sheria yule afanye tathimini kati ya wale wayahudi na yule Msamaria aliyetoa msaada kwa mhitaji yule aliyepata kipigo na wanyang’anyi, mwana-sheria anaelewa soma lile na kumjibu Yesu, “Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo,” Lk 10:37. Wapendwa katika Kristo, yatupasa kusimama katika kweli na haki, hivyo tutende yote kwa upendo na huruma ya kweli. Tusipolifanya jambo hilo basi tujiandae kusutwa na dhamiri zetu katika umiele wote.

Wapendwa wana wa Mungu, mamlaka aliyokuwa nayo Yesu ni vita dhidi ya uovu hapa duniani. Ni ukweli usiopingika kwa kupitia jina lake tunapata uponyaji wa kweli. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6.  Mamlaka ya Yesu yamejengwa chini ya mamlaka ya Mungu.

Hivyo hakuna jambo lolote alifanyalo Yesu Lisilo kuwa na uhusiano na Mungu, huku jambo lile likifunua siri ya Mungu kila kukichwa. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16. Kwa nini basi nakuwa na mashaka juu ya utendaji wa Kristo katika maisha yangu?

Wapendwa katika Kristo, Yesu anapotoa mfano wa vazi kuukuu na jipya, na kwa upande mwingine divai ya zamani na kiriba kipya anataka kutufundisha jambo hili; “kwanza kabisa lazima tujue sababu na malengo ya maisha yetu hapa duniani. Hatupo hapa duniani kwa bahati mbaya hata kidogo. Tupo katika ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu ambao ni dhahiri na mathubuti. Hivyo lolote lile lililo jema mbele ya Mungu huwiishwa na kufanya upya.

Somo letu la kwanza, linauelezea uhali wa jambo hili, yaani,  Mungu ili awe sehemu ya maisha yako na kielelezo cha yale yote uyafanyayo, yakupasa kuushinda ubinadamu wako na matamaniyo yake. Kuushinda ubinadamu wako, yakupasa kujipokea na kujikubali kwamba wewe ni binadamu katika maana ya mafanikio yako na mapungufu yako. Katika uwezekano huu, ikiwa ni mafanikio na mapungufu yake, binadamu anabaki kuwa binadamu, na Mungu anabaki kuwa Mungu katika ukamilifu wake.

Hivyo kuwa wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu kwake Yeye mwenyewe na kwetu sisi, twahitaji kuipokea hali yetu ya ubinadamu, na wakati huo huo kuushinda ubinadamu wetu huo kwa kuegemea ukamilifu ule tulioitiwa na Mungu. Naye Yesu katika kweli hii anasema, Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ndio wito wetu wa kila siku na kulingana na mazingira yoyote yale tutakayokuwa, yaani, kuwa wakamilifu kama ‘Baba yetu wa mbinguni alivyo makamilifu.

Kwa kuujua ukweli huo, Mtume Paulo analiweka jambo hili wazi kwa watu wake na kusema, Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia,” Gal 1:1-2. Ni wazi kabisa Mtume Paulo anataka tuwe makini kwa jambo hili: ‘kamwe tusijifananishe na matokeo ya mafanikio yetu, bali tuutazamie ule utukufu na ukamilifu tulioitiwa.’ Kuna anguko kubwa sana pale tunapojifananisha na kujilinganisha na mafanikio yetu binafsi.

Mazingira hayo ndiko kwenye chimbuko kubwa la majivuno, na penye majivuno hakuna ukuaji wa maisha ya kiroho. Mwenye majivuno hana nafasi ya Kristo ndani ya maisha yake. Nafasi ile ya Kristo imetawaliwa na ubinafsi wake na umimi wake. Katika hali hii kuna anguko kubwa sana la kurudi nyuma katika imani. Mtume Paulo haoni haya kuusema ukweli huu; Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine,” Gal 1:6. Ndugu yangu, yote yaliyo ya kibinadamu pasipo uhusiano na Mungu, hayana umilele.

Wapendwa wana wa Mungu, kilichohubiriwa na Kristo wakati ule katika historia ya wokovu wetu, na sasa kama kielelezo cha Kanisa lililo hai, na Sakramenti ya wokovu wetu ni habari njema ya wokovu wetu. Habari hii njema ya wokovu wetu hii hai muda wote na katika umilele wote.

Hivyo kwenda kinyuma na agizo hili la Yesu kabla ya kupaa kwake ili hali tunajua, ni kuipalilia ‘laana huku tukijua.’ Agizo hilo ndilo hili, ‘kwa Kanisa kama Sakramenti ya wokovu, na kwa Kanisa kama Mwili wa Kristo, yaani, kila aliyebatizwa na kuishi ahadi zake za ubatizo; Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,”’ Mk 16:15-16.

Hiki ndicho akisemacho Mtume Paulo wa Wagalatia kuhusu mahusiano ya Habari Njema ya wokovu na laani ipatikanayo kwa kutokuhubiri kweli iliyo katika habari njema hivyo. Naye anasema, Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal 1:8.

Kweli iliyo ndani ya habari njema ya wokovu wetu hubaki na kuhubiriwa kama ilivyo pale tunapoushinda ubinadamu wetu. Mtume Paulo anatutafakarisha kwa kusema, Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo,” Gal 1:10. Ndugu yangu, panapozidi ubinafsi wetu, Kristo hana nafasi.

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo aliye Njia, Kweli, na Uzima wetu, Yoh 14:6, anapokosa nafasi katika maisha yetu, ni kwa namna hiyo hiyo, Mungu hana nafasi katika maisha yetu. Je, twawezaje kumfikia Mungu bila kupita kwake Kristo aliye na mamlaka yote? Kristo Yesu anaweka wazi ukweli huu na kusema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 6:65. Kuupata au kuufikia Ufalme wa Mbinguni bila Kristo, ni sawa na samaki kuishi na kustawi bila maji. Je inawezekana?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe,” Gal 1:9

Tusali:-Ee Yesu, nitumie kadiri ya takwa lako, ili ujulikane pale usipojulikana. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario