ALHAMISI
WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 3:18-23
Zab/Kit: 24:1-2,
3-4ab, 5-6
Injili: Lk 5:1-11
Nukuu
“Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa
mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa
mwenye hekima,” 1Kor 3:18
“Maana
hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye
awanasaye wenye hekima katika hila yao,” 1Kor 3:19
“Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni,
akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali
chomboni,” Lk 5:3
“Hata
alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu
zenu mvue samaki,” Lk 5:4
“Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu,
akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8
“Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa
utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b
“Hata
walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata,” Lk 5:11
TAFAKARI: “Nanyi
ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu. Tweka
mpaka kilindini.”
Wapendwa wana wa Mungu, kwa
uzoefu aliokuwa nao Simoni kama mvuvi wa samaki, isingekuwa rahisi kuuchukua
ushauri wa Yesu wa kurudi tena ndani ya maji na kuvua samaki. Elewa kwamba
usiku kucha Simoni na wenzake walikesha wakivua bila kupata chochote. Usiku
ndio muda muhafaka wa kuvua samaki. Leo kwa namna ya kushangaza Yesu anamwambia
Simoni azitupe nyavu zake ndani ya maji mchana kweupe, na kwenda kinyume kabisa
na utaratibu wa uvuvi. “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka
kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4. Simoni akitambua
alichokifanya usiku kucha bila kupata chochote, “akajibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate
kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5. Maneno haya ya Simoni
“lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” yanaonyesha kujisalimisha kwa Simoni
pasipo shaka mbele ya Yesu. Ni kwa njia ya neno
hili: “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho
chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa
nuru ya watu,” Yoh 1:3-4. Je, bado unamashaka na Neno wa Mungu, yaani Yesu
Kristo?
Maneno
hayo ya Simoni yenye kuonyesha kujisalimisha kwake, ndiyo roho na uzima. Katika
hili Yesu anasema, “Roho
ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena
ni uzima,” Yoh 6:63. Na neno lile Yesu alilomwambia Simoni “tweka mpaka
kilindini,” ndiyo uzima na ponya yake Simoni. Ndugu yangu tunayesafiri sote
katika tafakari hii, tuzame kidogo ndani na tuone maana halisi ya kujisalimisha
kama siri na ufunguo wa mfanikio yote katika maisha yako.
Kujisalimisha ni neno
lisilotumiwa sana, halipendwi kama vile neno kunyenyekea. Lina maana ya
kupoteza, na hakuna mtu yeyote anapenda kupoteza. Kujisalimisha kunaonyesha
picha isiyopendeza ya kukubalika kushindwa katika vita, kupoteza katika
michezo, au kukubali kushindwa na mpinzani mwenye nguvu zaidi. Neno hili
linatumiwa mara nyingi katika hali isiyokubalika. Wahalifu waliotekwa
hujisalimisha kwa mamlaka.
Katika mila ya leo ya
ushindani tunafundishwa kutokuacha au kutokukubali tu. Hivyo hatusikii sana
kuhusu kujisalimisha. Kama kushinda ndiyo kila kitu, basi kujisalimisha hakupo.
Labda tuongelee kushinda, kufanikiwa, kuzidi nguvu, na kushinda vita kuliko
kujitoa, kunyenyekea, kutii, na kujisalimisha. Lakini kujisalimisha ni kiini
cha kuabudu. Ni mwitikio wa asili wa huruma na upendo wa ajabu wa Mungu. Tunajitoa
nafsi zetu kwake, si kwa hofu au kwa kuwa ni wajibu. Lakini kwa upendo, “kwa
sababu alitupenda kwanza.” I Yn 4:9-10, 19.
Kujisalimisha kwa Mungu
si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu
hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo.
Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili
kubadilisha yanahitajika kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu
waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa uoga au
mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe
kama mitambo (robots) ili kumtumikia.
Kujisalimisha siyo
kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha huutia nguvu.
C. S Lewis alisema, “kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi
kuwa sisi wenyewe-kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali
za watu wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa…. Ni pale
ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na
ule utu wangu halisi.” Naye Mtume Paulo anasema, “nanyi
ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu,” 1Kor 3:23
Kujisalimisha
kunadhihirika vyema katika kutii. Unasema ‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote
anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu
Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata
samaki, Simoni alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena”
“Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na hatujakamata samaki yeyote.
Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini.” Lk.5:5. Watu waliojisalimisha
hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.
Hapa Simoni Petro
anauvua uelewa wake, anaweka pembeni uzoefu katika jambo analolijua tangu udogo
wake, na kuruhusu hekima ya Mungu ifanye kazi ndani yake. Kwa maneno mengine,
Simoni anaiweka pembeni hekima na busara yake ya kibinadamu na kuruhusu neema
na hekima ya Mungu ifanye kazi ndani yake. “Maana
hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye
awanasaye wenye hekima katika hila yao,” 1Kor 3:19. Kuiacha hekima ya dunia na
kuruhusu hekima ya Mungu ndani yako kutakuhitaji ujisalimishe.
Jambo lingine katika
kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu alifuata maelekezo ya Mungu bila kujua
alikokuwa akienda. Hana alisubiri wakati wa Mungu bila kujua ni lini. Mariamu
alitarajia muujiza bila kufahamu utatendekaje. Yusufu aliamini lengo la Mungu
bila kujua kwa nini mazingira yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa
amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea. Katika kweli hii Mtume Paulo
anatuambia, “Mtu asijidanganye mwenyewe;
kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe
mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18. Kuwa mpumbavu ili upate
kuwa mwenye hekima kutakuhitaji kujisalimisha.
Utafahamu
umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu akutengenezee mambo yako badala ya
kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha jambo lako, na mwisho ukatawala
mazingira hayo. Unamwachia Mungu afanye, Huhitaji wakati wote kuwa,
“mwangalizi.” Maandiko matakatifu yanasema, “Jisalimishe nafsi yako kwa Bwana,
na umsubiri kwa uvumilivu.” Zab.
37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia unafahamu kwamba
unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo
iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilii mbali
wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.
Na tazama huu ndio
uzima juu ya neno lile la Yesu na kujisalimisha kule kwa Simoni: “Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno,
nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia
mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja,
wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama,” Lk 5:6-7. Ndugu yangu,
yawezekana umekata tamaa kabisa katika maisha yako kutokana na jambo fulani
ambalo kwa uelewa wako na uzoefu wako hakuna pa kutokea. Leo Yesu anakuambia
neno hili, “‘tweka mpaka kilindili,” yaani
jaribu tena kile kilichobaki katika ukamilifu wake, na hadi mwisho wake kabisa,
nawe utaona uwezo wangu.’ Hakika hakuna jambo lolote linaloweza kumshinda
Mungu.
Yawezekana wakati
fulani ulikuwa tajiri sana kwa kuwa na mali na pesa nyingi, na leo huna
chochote. Usijifungie ndani kwa kuona aibu au kuchekwa na watu, na wala
usiendelee kuishi jana ambayo ilishapita. Itazama kwa kina leo yako ambayo
ndiyo uliyo nayo ili iwe tumaini lako la kesho. Jana yako ya ‘utajiri wa mali
na pesa’ ibaki kuwa kumbukumbu tu na rejea ya kuwa karibu zaidi na Mungu. Jana
yako iliyokuwa na mafanikio mengi ikukumbushe kiini halisi cha maisha, yaani, Maisha
ni jaribu, Maisha ni dhamana, na Maisha ni jukumu la muda mfupi.
Matokeo ya nguvu na
uwezo wa Yesu katika muujiza huu, unamfanya
Simoni kuyaona maisha yake ya ndani. “Simoni
Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa
kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8. Ndugu yangu, hutoweza kujiona ulivyo kama
hutojiachia ndani na katika Kristo Yesu. Kuiona vizuri chunusi iliyoko kwenye
paji la uso wako, yakupasa kusimama mbele ya kioo. Kumbe kujiachia mbele ya
kioo kunakuwezesha kujiona vizuri. Yesu ni kioo kwetu, na ndivyo Simoni
alivyojigundua kuwa yu mdhambi.
Pamoja na udhaifu ule
aliokuwa nao Simoni bado Mungu anampango na maisha yake. Tena mpango mahususi
kabisa. Naye “Yesu akamwambia
Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b. Yesu anaifanya njia katika maisha ya Simoni. Huyu
ndiye baadaye aliyejulikana kama Simoni Petro, na juu yake ndipo lilipo jengwa
Kanisa. Mtume Paulo anatuambia, “Jaribu
halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni
mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile
jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13.
Amina! Mruhusu Yesu ndani yako pasipo shaka naye atayatengeneza maisha yako
upya.
Wapendwa wana wa Mungu,
ukiyatazama maisha yako na jinsi Mungu alivyoendelea kuwa upendo na huruma
kwako, hakika yote ndani yako ni kwa neema ya Mungu. Hakika, “Bwana, kama Wewe
ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Ndugu yangu, mahangaiko katika maisha yako ya kila siku
yasiwe ukuta wa kutokuona uwepo na nguvu ya Kristo Yesu ndani ya yale uyafanyayo
hata kama uzoefu wako unathibitisha kutokuwezekana tena.
Kama
kweli wasadiki Kristo ndiye Mwokozi, basi ni kwa namna hiyo hiyo huyaweza yote
yaliyo chini ya miguu yake kwa sababu, “amevitia vitu vyote chini ya miguu
yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo
mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:22-23.
Yesu Kristo analiweka jambo hili hadharani anapowakuta Simon Petro na wenzake
waliokuwa mahodari wa kuvua samaki usiku kucha bila kupata chochote. Ni Kristo
Yesu huyo huyo aliye hai atakayeyabadilisha maisha yako. Jisalimishe kwake
mara!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Hata
walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata,” Lk 5:11
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
yatengeneze upya maisha yangu. Naamini pasipo shaka yoyote, Wewe kwangu ndiye
Njia, Kweli, na Uzima. Amnia